Na. OWM, Morogoro.
Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kupitia kikosi cha 837KJ Chita, kilichopo
Wilayani Kilombero, Mkoani Morogoro kimeanza kutekeleza kwa vitendo Programu ya
Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kuanza ujenzi wa skimu
ya umwagiliaji ambayo kwa awamu ya kwanza skimu hiyo itakuwa na urefu wa Km 2.3, ambayo
hivi karibuni Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo ameweka jiwe la msingi la kuizindua.
Programu ya ASDP II inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, malengo yake
ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) kupitia
maeneo makuu manne ikiwemo eneo la Usimamizi Endelevu wa Matumizi ya Maji na
Ardhi ambalo moja ya kipaumbele cha uwekezaji ni kuendeleza
miundo mbinu ya umwagiliaji.
Akiongea mara baada ya kufanya ziara kwenye Kikosi cha Jeshi 837KJ
Chita, tarehe 21 Oktoba, 2020, Wilayani Kilombero lengo likiwa ni kufuatilia
utekelezaji wa Programu hiyo kwa wadau wa Programu ya ASDP II, Mratibu wa
Programu ya ASDP II Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Salim Nandonde, amefafanua kuwa ujenzi
wa skimu hiyo utasaidia Programu kulifikia lengo la Kitaifa kwa miaka mitano la
kuwa na eneo la umwagiliaji la hekta milioni moja na laki mbili.
“Jeshi la kujenga Taifa ni mdau muhimu katika utekelezaji wa Programu
ya ASDP II, na kwa kikosi hiki cha 837 KJ Chita, kuanza
ujenzi huu wa skimu ya umwagiliaji itasaidia kuongeza eneo linalohitajika la
kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo kwa sasa eneo lililopo la kilimo cha
umwagiliaji ni takribani hekta laki sita na alfu tisini na nne tu.
Ameongeza kuwa mradi huo pia umezingatia kuongeza thamani ya zao la
mpunga kwa kuanza ujenzi wa ghala la kuhifadhi mpunga sambamba na kuwa na
mpango wa kujenga kiwanda cha kusindika
mpunga huo ambapo hatua hiyo inaongeza wigo wa Kikosi hicho kuwekeza kwenye
eneo kuu la tatu la Programu ya ASDPII ambalo ni kukuza Biashara na Kuongeza
Thamani.
Kwa upande wake Afisa Utawala wa Kikosi cha 837 KJ Chita, Kapteni
Nyakohanda Rusuhi ameeleza kuwa ujenzi wa skimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
Programu ya ASDP II pamoja na mipango ya JKT inayosimamiwa na Mkuu wa Jeshi la
Kujenga Taifa, Meja Jenerali Charles Mbuge, ambapo Programu hiyo inawataka wadau wake kufanya
mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kulima kilimo chenye tija.
“Awali wakati tunategemea kilimo cha mvua tulikuwa tunavuna gunia sita
kwa hekari moja, lakini baada ya kukamilisha ujenzi wa skimu hii tunatarajia
kuvuna takribani ya gunia 35 kwa hekari moja. Tukifanikiwa kupata mavuno haya
tutakuwa tumezalisha chakula cha kutosha lakini pia tutakuwa tumefanikiwa
kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyelitaka Jeshi la
kujenga Taifa kujilisha.” Amesisitiza Rusuhi.
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya juu Kusini -Mbeya,
ambao wanashirikiana na JKT kujenga skimu hiyo, Mhandisi Elibariki Mwendo
ameeleza kuwa tayari wameanza kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kuanza
na ujenzi wa awali wa ekari 2,500 kati ya ekari 12,000 zinazolengwa kujengwa.
Mhandisi Mwendo ameongeza kuwa ujenzi wa skimu hiyo utakuwa na ujenzi
wa mifereji katika mito mitatu tofauti, ujenzi wa mifereji mikuu mama mitatu
yenye urefu wa mita 1,716 pamoja na vivushamaji kupita kwenye reli ya TAZARA,
pia ujenzi wa mabanio matatu, mifereji midogo ya kutoa maji shamba ipo 155,
matuta mawili ya kuzuia mafuriko yenye kina cha wastani wa mita mbili.
Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ilizinduliwa
rasmi mwaka 2018 na inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo inatekelezwa na
wadau wakuu wa tatu ambao ni Serikali, Sekta Binafsi na Washirika wa maendeleo.
Malengo makuu ya Programu ya
ASDP II ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo (kilimo, mifugo na uvuvi) ili
kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na
kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, usalama wa
chakula na lishe.
Mbali na maeneo makuu ya ASDPII
ambayo Kikosi cha JKT Chita kimeanza kutekeleza maeneo mengine ni Kuongeza Tija
na Faida kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija hasa kwenye mazao ya
kipaumbele; na Kuweka Mazingira Wezeshi ya Kuendeleza Sekta ya kilimo kwa
kuwezesha uratibu, ufuatiliaji na kufanya tathmini ya sekta ikiwa ni pamoja na
kuimarisha taasisi na kuweka mazingira wezeshi ya uratibu. Ni wazi kuwa Jeshi
la Kujenga Taifa lipo kwenye nafasi kubwa ya kutekeleza Programu ya ASDPII kwenye
maeneo yote makuu ya Programu hiyo.
MWISHO.
Mratibu wa Programu ya ASDP II Ofisiya
Waziri Mkuu, Dkt. Salim Nandonde,akifafanua umuhimu wa skimu ya umwagiliaji inayojengwa
na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kupitia kikosi cha 837KJ Chita, Wilayani Kilombero,
Morogoro wakati waziara ya kufuatilia utekelezaji wa Programu hiyo inayoratibiwa
na Ofisi hiyo. Kulia kwake ni Mhandisi wa Mradi, Meja Mbaraka
Magogo na kushoto kwake ni Afisa Utawala wa Kikosi cha 837 KJ Chita, Kapteni
Nyakohanda Rusuhi na Mratibu Msaidizi Programu Ofisi ya Waziri Mkuu,
MethewMwinuka.
Mratibu wa Programu ya ASDP II Ofisi ya
Waziri Mkuu, Dkt. Salim Nandonde, akiongozwa na Afisa Utawala wa Kikosi cha 837 KJ Chita, Kapteni Nyakohanda Rusuhi kukagua ujenzi wa skimu ya umwagiliaji inayojengwa
na kikosi hicho Wilayani Kilombero, Morogoro wakati waziara ya kufuatilia utekelezaji
wa Programu hiyo inayoratibiwa na Ofisi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.