Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Bwa. Kaspar Mmuya amepongeza maendeleo
ya ujenzi wa ofisi za msajili wa vyama vya siasa nchini
zinazojengwa eneo la Kilimani Jijini Dodoma zitakazogharimu zaidi
ya shilingi bilioni 20.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliyasema hayo alipofanya ziara ya
kutembelea na kukagua ujenzi huo unaofanywa na kampuni kutoka China
ya Group Six International Limited ukisimamiwa na mshauri kutoka Chuo
Kikuu cha Ardhi.
Alisema ujenzi unatarajiwa kukamilika baada ya miezi
12 akisisitiza kuongezwa kwa rasilimali watu, muda wa kazi pamoja na vifaa ili
kufanya kazi ndani ya muda uliopangwa.
“Niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya Ofisi ya
Msajili wa vyama vya sisisa kwa usmamizi mkubwa mnaoufanya lakini
endeleeni kuongeza umahiri na kuwasaidia wenzetu wa Group Six
International wafanye kwa matokeo zaidi,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Pia aliamuagiza mshauri wa ujenzi kufika mara kwa
mara katika eneo la mradi na kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji
wengine kufahamu hali ya ujenzi na kutatua changamoto pindi
zinapojitokeza kuhakikisha jengo linajengwa katika hali ya uimara, ubora na
usalama.
“Nimshauri mtaalamu wetu awe anatembelea mara kwa mara
jengo hili kujionea maendeleo ya kazi kama kuna shida yoyote inatatuliwa
kwa wakati na kufanya marekebisho yanayaotakiwa,”alisisitiza .
Aidha aliwahimiza kuongeza ubunifu wa utendaji kazi kwa
kugawa maeneo na muda wa kukamilika kwa kazi kwani itasaidia kuhamasisha kazi
kufanyika kwa mwamko na ubora zaidi kama njia ya kuendana na muda wa mkataba
unavyotaka.
“Waongeze mtindo wa kufanya kazi kwa kupewa kipande cha
kazi kwa muda inasaidia utendaji wa kazi na waangalie ubora usiathiriwe kwa
sababu mtu anapopewa eneo lake na muda wa kikomo inamfanya ajitume kwa kasi
kubwa,” alieleza Bwa. Mmuya
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.