Serikali imetoa rai kwa vijana
nchini kufanya juhudi za kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya
UKIMWI (VVU) pamoja na walio shuleni kuhakikisha wanazingatia masomo na
kujiepusha na tabia hatarishi zitakazosababisha kupata maambukizi na kushindwa
kuyafikia malengo yao.
Rai hiyo ilitolewa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe.
George Simbachawene wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ugawaji
Vishikwambi kwa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kupitia mradi wa Timiza
Malengo.
Mhe. Simbachawene alisema
lengo la mradi huo ni kusaidia vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 24 kutimiza
ndoto zao pamoja na kuwasaidia vijana walio ndani na nje ya shule
kwa kuwajengea uwezo wa fikra , maarifa na maadili ili wawe salama dhidi ya
maambukizi ya VVU.
“Kama Taifa tuna kila sababu
ya kulinda kundi la vijana kuimarisha nguvu kazi ya Taifa , kukuza uchumi pia
kujenga Taifa imara na lenye nguvu . Nia ya Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na
vijana wazalendo wanaotambua mchango wao katika jamii , wenye kujitolea katika
shughuli za maendeleo ,” alisema Mhe. Simbachawene .
Pia aliongeza kuwa mradi huo
unaogharimu takribani bilioni 55 unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa UKIMWI ,
Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) wasichana balehe na wanawake vijana
wapatao 1,000,000,000 watafikiwa na mradi huo.
“Niwapongeze wadau wa
maendeleo kwa kutambua umuhimu wa mapambano haya na udhibiti wa
maambukizi ya VVU hususani kwa vijana na ndani ya Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan inaridhishwa na utekelezaji wa
mradi kwani umefanikiwa kutoka mikoa mitatu hadi mitano na
Halmashauri 10 hadi 18 nchini,”aliongeza.
Aidha aliwataka Wakurugenzi
Watendaji wa Halmashauri zinazotekeleza mradi kusimamia kwa ufanisi pamoja na
kuanisha Klabu za UKIMWI shuleni, kusimamia na kufuatilia uwajibikaji wa
Maafisa Ugani katika usimamizi wa maendeleo ya utekelezaji wa mradi kwa
walengwa na kusimamia matumizi sahihi ya zana kwa uendelevu wa
mradi katika Halmashauri husika.
Kwa upande wake Waziri wa
Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda alibainisha kwamba kukithiri kwa
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia shuleni na katika maeneo mbalimbali
huchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi mapya ya UKIMWI na afya za watoto na
vijana kuathirika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dk. Leonard Maboko alieleza kuwa ni
kusudi la tume hiyo chini ya mradi wa Timiza Malengo kuwezesha wasichana balehe
na wanawake vijana kukaa shuleni kutimiza malengo yao na walio nje ya shule
kupatiwa elimu ya ujasiriamali na kupewa ruzuku kuanzisha miradi midogo midogo
kujikwamua kiuchumi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.