Tuesday, September 20, 2022

GLOBAL FUND YAUNGA MKONO SERIKALI KUKABILIANA NA MAGONJWA NCHINI

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amekutana na kufanya mazungumzo na Meneja Mkaguzi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Kupiga Vita UKIMWI, TB na Malaria (GLOBAL FUND) Bwa. Andrew Hammond ofisini kwake Jijini Dodoma.

Dkt. Jingu amesema mazungumzo hayo yalilenga kujadili masuala mbalimbali kuhusu sekta ya afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya katika maeneo yao.

Ameongeza kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kushirikana na mfuko huo kwani umekuwa na mchango mkubwa katika kuwezesha vifaa tiba kama ilivyo azima ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia  Suluhu  Hassan  ya kujenga miundo mbinu ya  na kuboresha masuala ya tiba kwa wananchi.

Naye Meneja Mkaguzi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa kusaidia mapambano  dhidi ya  UKIMWI, TB na Malaria (GLOBAL FUND) Bwa. Andrew Hammond ameishukuru Tanzania kwa kushirikiana na Mfuko huo katika kupiga vita maradhi ya Kifua Kikuu, Malaria na Ukimwi.

Ameahidi kuwa Mfuko wa Dunia utaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na magonjwa hayo hapa nchini kwa kuelekeza rasilimali fedha kwa ajili ya kununua dawa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma ya afya.

 

Tuesday, September 6, 2022

SERIKALI KUJA NA MAPENDEKEZO YA SHERIA MPYA YA USIMAMIZI WA MAAFA

 


Serikali imeandaa mapendekezo ya kutungwa kwa  sheria mpya ya usimamizi wa maafa ili kuweka mfumo  wa udhibiti na uratibu wa maafa  kwa ajili ya hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyokutana katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alisema  kutungwa kwa sheria hiyo  ni kuifuta sheria iliyopo sasa ya mwaka mwaka 2015 sura  ya 242. 

Mhe. Simbachawene alieleza kwamba awali masuala ya maafa hayakuwa na mfumo wa kisheria wa uratibu hali ambayo imekuwa ikisababisha mgongano wa majukumu hivyo kutungwa kwa sheria hiyo kutaainisha madaraka, wajibu, maamuzi, utunzaji wa rasilimali na muono unaozingatia taarifa za hali ya hewa.

“Awali masuala ya maafa yalikuwa na daraja fulani la watu, masuala ya kisheria yalikuwa kama yako juu hata ikitokea maafa ngazi ya Wilaya au Kijiji wanasema tumuone Mkuu wa Wilaya sasa tunataka sheria iseme yanapotokea maafa ijulikane kamati gani inahusika  na kuweka mfumo wa ugatuaji kuanzia; madaraka, maamuzi na utunzaji wa rasilimali,”Alisema Mhe. Simbachawene.

Pia aliongeza kwamba sababu nyingine ya kutunga sheria mpya ya Usimamizi wa Maafa ni kuimarisha mfumo wa kiutendaji wakati wa maafa na upatikanaji wa taarifa na takwimu za matukio ya maafa na kuweka mfumo mpya wa kitaasisi unaozingatia mfumo wa kiutawala utakaowezesha ushiriki wa wadau wote muhimu  kabla, wakati na baada ya maafa kutokea nchini..

“Eneo lingine ni kuhakikisha  kamati  hizi zinakuwa za kitendaji na siyo bodi ambapo itasaidia katika kutafuta ufumbuzi yanapotokea maafa pamoja na kuwezesha kurejesha hali ya awali baada ya madhara ya majanga kujitokeza,” aliongeza.

Aidha alieleza kwamba utungwaji wa sheria  utasaidia kutumia taarifa za hali ya hewa na majanga ambapo kamati zitatakiwa kukutana pamoja na utunzaji wa rasilimali ambazo hutumika kukabili na kurejesha hali pamoja na kuzingatia usalama wa wananchi na mali zao.

Kwa upande wake Makamu  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea  kushirikiana na Kamati  kuhakikisha  sheria mpya inatungwa kama hatua ya kuzuia na kukabili maafa ambayo husabababisha athari kubwa.

Naye Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Zainabu Katimba alishauri uundwaji wa Kamati Elekezi ya Kitaifa uzingatie sekta badala ya Wizara ambayo huwa na usimamizi wa jumla wa  utekelezaji wa maafa.