Serikali
imeandaa mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya ya usimamizi wa maafa
ili kuweka mfumo wa udhibiti na uratibu wa maafa kwa ajili ya hatua
za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa kukabili na kurejesha hali
pindi maafa yanapotokea.
Akizungumza
katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyokutana
katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa
Maafa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George
Simbachawene alisema kutungwa kwa sheria hiyo ni kuifuta sheria
iliyopo sasa ya mwaka mwaka 2015 sura ya 242.
Mhe.
Simbachawene alieleza kwamba awali masuala ya maafa hayakuwa na mfumo wa
kisheria wa uratibu hali ambayo imekuwa ikisababisha mgongano wa majukumu hivyo
kutungwa kwa sheria hiyo kutaainisha madaraka, wajibu, maamuzi, utunzaji wa
rasilimali na muono unaozingatia taarifa za hali ya hewa.
“Awali
masuala ya maafa yalikuwa na daraja fulani la watu, masuala ya kisheria
yalikuwa kama yako juu hata ikitokea maafa ngazi ya Wilaya au Kijiji wanasema
tumuone Mkuu wa Wilaya sasa tunataka sheria iseme yanapotokea maafa ijulikane
kamati gani inahusika na kuweka mfumo wa ugatuaji kuanzia; madaraka,
maamuzi na utunzaji wa rasilimali,”Alisema Mhe. Simbachawene.
Pia aliongeza
kwamba sababu nyingine ya kutunga sheria mpya ya Usimamizi wa Maafa ni
kuimarisha mfumo wa kiutendaji wakati wa maafa na upatikanaji wa taarifa na
takwimu za matukio ya maafa na kuweka mfumo mpya wa kitaasisi unaozingatia
mfumo wa kiutawala utakaowezesha ushiriki wa wadau wote muhimu kabla,
wakati na baada ya maafa kutokea nchini..
“Eneo
lingine ni kuhakikisha kamati hizi zinakuwa za kitendaji na siyo
bodi ambapo itasaidia katika kutafuta ufumbuzi yanapotokea maafa pamoja na
kuwezesha kurejesha hali ya awali baada ya madhara ya majanga kujitokeza,”
aliongeza.
Aidha
alieleza kwamba utungwaji wa sheria utasaidia kutumia taarifa za hali ya
hewa na majanga ambapo kamati zitatakiwa kukutana pamoja na utunzaji wa
rasilimali ambazo hutumika kukabili na kurejesha hali pamoja na kuzingatia
usalama wa wananchi na mali zao.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria
Mhe. Najma Giga aliipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea
kushirikiana na Kamati kuhakikisha sheria mpya inatungwa kama hatua
ya kuzuia na kukabili maafa ambayo husabababisha athari kubwa.
Naye Mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Zainabu Katimba alishauri uundwaji wa Kamati
Elekezi ya Kitaifa uzingatie sekta badala ya Wizara ambayo huwa na usimamizi wa
jumla wa utekelezaji wa maafa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.