Serikali imetoa rai kwa viongozi wa dini
kuendelea kuhimiza jamii kuepuka uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya na
kujenga uelewa kuhusu madhara ya madawa ya kulevya.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka
2022/23 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mjini
Dodoma.
“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa
za kulevya, itaendelea kushirikiana na Wizara nyingine katika kuona namna nzuri
ya kuandaa maudhui ya mtandaoni ili kuelimisha vijana kuhusu athari ya dawa za
kulevya kama ambavyo Tume ya Kudhibiti UKIMWI inavyofanya”.
Tupo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi
ya CCM ambayo imetoa maelekezo mahususi kuhusu kushughulikia dawa za kulevya,
Amesema Naibu Waziri.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Dkt. Alice Karungi ameipongeza serikali kwa
kiwango cha fedha kilichopelekwa kwenye Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za Kulevya kinachoendana na kwa kiwango cha fedha kilichokadiriwa wakati
wa bajeti.
“Zoezi la kuwasaidia vijana wetu waliopata
nafuu ya uraibu wa dawa za kulevya kwa kupatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi; kama
sehemu ya jitihada za Mamlaka, katika kudhibiti na kupambana na dawa za
kulevya, liwe endelevu”.
Naye Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila amesema mamlaka
imeweka msukumo mkubwa katika kukabiliana dawa zinazotoka nje ya
nchi, Heroin, Cocaine na Methamphetamine.
“Bangi imekuwa ikitumika kwa wingi kwa
sababu inapatikana kwa bei nafuu na zinalimwa katika maeneo ya kujificha sana”.
Tamaa ya kupata fedha imekuwa ikichochea
wananchi kulima bangi kulinganisha na mazao mengine hata hivyo udhibiti
unaendelea.
“Tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Klimo
waweze kushauri Mwananchi badala ya kulima bangi walime zao gani ambalo
litawasaidia kupata fedha nyingi.”
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Dkt. Leonard Maboko ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa
za Kulevya kwamba fedha za Global Fund zitatoka robo ya pili ya mwaka wa fedha
2022/23.
“Mradi
wa Umoja wa Mataifa wa Kuhusisha UKIMWI kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa
katika bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi 2,132,610,000.00, tayari kiasi cha
shilingi 1,090,849,597.00 zimepokelewa. Mfuko wa Udhamini wa
Kudhibiti UKIMWI (ATF) katika
bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi
1,880,000,000.00 fedha za ndani, tayari
kiasi cha shilingi 469,992,000.00 zimepokelewa mwishoni mwa mwezi
Septemba 2022 hivyo zitatumika katika robo ya pili ya mwaka (Oktoba – Desemba,
2022)”.
Naye Mhe. Asia Halamga ameomba serikali
kubadili baadhi ya Sheria zinazowazuia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana
na Dawa za Kulevya iweze kufanya kazi zake kikamilifu.
“Fedha tunazotumia kutibu ni vyema tukazitumia kudhibiti ili
tusiendelee kuumiza taifa na hasa vijana”.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.