Waziri wa Nchi Ofisi
ya waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George
Simbachawene amewataka watendaji wa Serikali kuendelea kutatua changamoto za
wananchi zinazowakabili ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.
Waziri ametoa kauli
hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kujenga uwezo kwa Menejimenti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Idara ya
Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za Serikalini yaliyofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi uliopo
Njedengwa Jijini Dodoma Januari 19, 2023.
Waziri alihimiza kila
mtendaji wa Serikali kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi huku
akitatua changamoto za wananchi katika eneo lake la kazi.
Aliongezea kuwa ni
muhimu kwa watendaji kuwajibika kwa kuyafikia malengo ya Serikali ya Awamu ya
Sita huku wakileta matokeo chanya yatokanayo na utendaji mzuri wa kazi zao za
umma.
"Hakikisheni
mnakuwa watu wa msaada kwa wengine katika kuyatekeleza majukumu yenu,
muwe watengeneza furaha na hii iwe kipimo kwa kila mwenye kukufikia huku
ukizingatia taratibu za utumishi wa umma na sheria zilizopo,"alisema
Waziri Simbachawene
Aidha aliwaasa
waendelee kutumia taaluma zao kuleta matokeo chanya kwa Serikali na jamii huku
wakijitathimini utendaji wa kila siku.
“Ni sahihi
kujitathimini kila iitwapo leo ili kuona namna unavyoleta matokeo chanya kwenye
utendaji wako wa kila siku, matokeo utayoyapata yatatusaidia kuongeza
tija ,” alisisitiza Waziri Simbachawene.
Akieleza umuhimu wa mafunzo
hayo aliwataka kuhakikisha mafunzo yanawafikia watendaji katika ngazi
zote ili kuendelea kuongeza uelewa kwa watumishi wa umma.
" Mafunzo haya
yawafikie watumishi wote katika Idara na vitengo vyetu bila kumuacha nyuma mtu
yeyote ili kuleta chachu katika utendaji na kuondokana na tabia ya
mazoea," alisema.
Aliongezea kuwa
matokeo ya Mafunzo haya yatumike kuboresha mifumo ya uratibu, usimamizi na
ufuatiliaji wa shughuli za Serikali ili kuwa na uwezo wa kupima utendaji wa
Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali kisayansi.
Aidha uwekwe utaratibu
ambao utawezesha uchambuzi wa Taarifa za kisekta na kutoa mrejesho wa maeneo
yanayohitaji kuboreshwa au kupewa msukumo zaidi.
"Ili kuendelea kuboresha shughuli za uratibu naamini uwepo Idara mpya ya Ufuatiliaji na Tathmini itasimamia hili na kuhakikisha kunakuwa na mrejesho kwa Wizara na Taasisi zote ili kuimarisha uwajibikaji," alihimiza.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu amesema mafunzo haya yanalenga
watendaji wa serikali kufanya kazi kwa ufanisi kwa weledi na kwa namna ambayo
itakidhi mahitaji pia yatajikita katika majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu
katika eneo la uratibu wa shughuli za serikali, na jukumu la kufanya kazi ya
ufuatiliaji na tathmini ya utendaji wa shughuli za Serikali.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.