Thursday, January 26, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE: IMARISHENI MIFUMO WA USHUGHULIKIAJI WA MATUKIO YA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO.

Serikali yahimiza jamii  kuanzia ngazi ya familia kuimarisha mfumo wa ushughulikiaji wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ndani na nje ya shule unaowajumuisha wasimamizi wa shule, wazazi, walezi na jamii kwa lengo kuendelea kutokomeza matukio ya ukatili nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano wa Kitaifa wa tafakuri ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) uliofanyika katika Ukumbi wa Saint Gaspar Jijini Dodoma.

Waziri ameeleza kwamba Mfumo wa Ushughulikiwaji wa matukio ya ukatili utasaidia Taifa kupunguza kwa kiasi kubwa changamoto iliyopo katika jamii ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa Watoto.

“tuendelee kuunga mkono juhudi za Serikali kwa hali na mali ili kuhakikisha makundi yote ndani ya jamii yanalindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto alisema,” alisema Waziri Simbachawene.

Akieleza kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989, wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto 2008 na Sheria ya Mtoto Na. 21, 2009, ambao unaoelezea masuala ya ukatili kwa watoto ni kinyume cha haki zao za msingi za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kutokubaguliwa.

Aidha umeeleza kuwa,vitendo vya ukatili vinarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 ambayo nchi imeridhia kutekeleza.

Waziri amehimiza kuendeleza juhudi za kukabiliana na ukatili huo katika zama za utandawazi kuwa na msukumo mpya na wa pamoja ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.

Amesema kuwa, athari za utandawazi zimedhoofisha mifumo ya ulinzi na usalama wa watoto hivyo kufanya kundi hilo kutokuwa salama kwani tatizo la ukatili bado ni changamoto katika ngazi zote.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake  na Makundi Maalum  Mhe. Dorothy Gwajima amesema wizara ya Maendeleo ya jamii imekuwa ikiratibu utekelezaji wa MTAKUWWA toka kuzinduliwa kwake mwaka 2016, na baada ya kukamilika kwake Wizara pamoja na Wadau wa maendeleo walifanya tathimini ya utekelezaji wake kuanzia 2017/2018 hadi 2021/2022 kupitia Mtaalam mwelekezi Chuo Kikuu cha Dodoma.

Waziri amesema taarifa ya tathimini imekamilika na imebainisha utekelezaji wa MTAKUWWA kwenye maeneo yote nane yalliyopo kwenye mpango huu, na imebainishwa maeneo muhimu yatakayoenda kutekelezwa kwenye mpango kazi ujao.

“Niwaombea wadau tuwe na subira tukiwa tunaendelea mapitio ya pamoja mpaka itakapotangazwa kwamba serikali pamoja na wadau,”aliomba Waziri Gwajima

Naye Mkurugenzi wa Shirika la ICS Tanzania Bwn.  Kudely Sokoine  Joram amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha mapambano haya yanatokomezwa huku akiipongeza Serikali kwa hatua inazochukua katika kukabiliana na changamoto ya ukatili wa makundi haya muhimu huku akitaja maeneo muhimu ikiwemo la kuimarisha mifumo ya ulinzi wa Wanawake na Watoto, kujenga uwezo wa Kamati za ulinzi wa Wanawake na watoto pamoja na kusaidia uratibu wa Masuala yote.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.