Imeelezwa kuwa uwepo
wa taarifa na huduma za hali ya hewa zinalenga kusaidia kuokoa maisha ya watu
na mali zao kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa, upepo
mkali na vimbunga nchini.
Hayo yameelezwa na
Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu, Idara ya Menejimenti ya Maafa,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine
Masalamado wakati akifungua mkutano wa 22 wa wadau wa utabiri wa msimu wa mvua
za vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) (National Climate Outlook Forum, Ncof-22
for October to December 2023 rain season) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli
ya Giraffe, Dar es Salaam.
Mkutano
huo wa Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa kwa msimu wa mvua za Vuli 2023, umebebwa
na kaulimbiu inayosema; “matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa
wote na kwa wakati”.
Alisema
kuwa mabadiliko
ya hali ya hewa ni halisi ambapo zimeshuhudia athari mbalimbali zinazotokana na
mabadiliko haya ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo,
kubadilika kwa misimu ya mvua hasa tarehe za kuanza na kuisha kwa mvua.
Pia
Mamlaka imeendelea kuboresha huduma ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa
maeneo madogo madogo (Downscaled forecast), kuwa utabiri huu wa Vuli
utaambatana na tabiri za wilaya zote (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za
juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na maeneo yanayozunguka Ziwa
Victoria.
Luteni Kanali
Masalamado ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuendelea kutoa
taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaosaidia kujiandaa na kujikinga na
viashiria vya maafa nchini hivyo kuifanya jamii kuwa na taarifa muhimu za hatua
za muhimu zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepuka madhara yatokanayo na maafa
nchini huku akisihi kuendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia mabadiliko ya hali
ya hewa.
“Ushirikiano huu ni
mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu
na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya
hewa,”alisema Luteni Kanali Masalamado.
Alifafanua kuwa,
Mamlaka inaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na wadau ili kuendelea
kukusanya maoni na taarifa mtambuka kwa ajili ya
kurahisisha ufungashaji wa taarifa hususani eneo la athari katika ngazi ya
wilaya. Hivyo wadau wote ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana na TMA ili
kufanikisha zoezi la upatikanaji wa taarifa za kisekta.
“Tunapojiandaa kupokea
taarifa ya utabiri wa mvua za Vuli, kwa mwezi Oktoba hadi Disemba, 2023; ni
muhimu sana kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu, kuelewa,
kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta yake”,
alisisitiza Luteni Kanali Masalamado.
Sambamaba na hilo
alihimiza na kuwasihi wadau wote kuzingatia sheria ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Namba 2 ya mwaka 2019, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vituo
vya hali ya hewa vinasajiliwa kama ambavyo sheria inaelekeza.
Vilevile kwa watumiaji
wa taarifa na huduma za hali ya hewa kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa za
hali ya hewa kwa mujibu wa sheria ili kuongeza tija na kupunguza athari za hali
mbaya ya hewa.
Kwa upande Wake Kaimu
Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Ladislaus Chang’a
alikieleza malengo ya mkutano huo wa wadau kuhusu Utabiri wa Vuli, Oktoba hadi
Disemba, 2023 alisema unalenga kujadiliana na kupata maoni ya wadau jinsi
utabiri wa mvua za Vuli utakavyoweza kutumika kwa tija katika sekta mbalimbali
hapa nchini.
“Kwa kuzingatia
umuhimu wa huduma za hali ya hewa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
imeendelea na jitihada za kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa
ikiwemo miundombinu na rasilimali watu. Hivyo, tunaishukuru Serikali
na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya
hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo,”
alisisitiza Dkt. Chang’a.
Aidha, akizungumzia
kuhusu msimu huu wa Vuli, 2023 mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwepo wa Hali
ya El Nino ambayo ilianza kujitokeza mapema mwezi Juni, 2023 na imeendelea
kuimarika. El Nino inatarajiwa kuendelea hadi mwanzoni mwa mwaka 2024.
“Sambamba na mifumo
mingine ya hali ya hewa, tathmini ya mwelekeo wa msimu wa Vuli 2023 itazingatia
pia uwepo wa hali hiyo ya El Nino na athari zinazoweza kujitokeza katika
maeneo mbalimbali nchini hivyo tuendelee kuchukua tahadhari muhimu ikiwemo kuzingatia
taarifa za utabiri zinazotolewa,” alisisitiza
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.