Tuesday, August 22, 2023

LUTENI KANALI MASALAMADO: TAARIFA NA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KUSAIDIA KUOKOA MAISHA YA WATU NA MALI ZAO

 


Imeelezwa kuwa uwepo wa taarifa na huduma za hali ya hewa zinalenga kusaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa, upepo mkali na vimbunga nchini.

 

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu, Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado wakati akifungua mkutano wa 22 wa wadau wa utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Disemba, 2023) (National Climate Outlook Forum, Ncof-22 for October to December 2023 rain season) uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Giraffe, Dar es Salaam.

 

Mkutano huo wa Wadau wa Huduma za Hali ya Hewa kwa msimu wa mvua za Vuli 2023, umebebwa na kaulimbiu inayosema; “matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa wote na kwa wakati”.

 

Alisema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni halisi ambapo zimeshuhudia athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko haya ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo, kubadilika kwa misimu ya mvua hasa tarehe za kuanza na kuisha kwa mvua.

 

Pia Mamlaka imeendelea kuboresha huduma ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo (Downscaled forecast), kuwa utabiri huu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.

 

Luteni Kanali Masalamado ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuendelea kutoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa unaosaidia kujiandaa na kujikinga na viashiria vya maafa nchini hivyo kuifanya jamii kuwa na taarifa muhimu za hatua za muhimu zinazopaswa kuchukuliwa ili kuepuka madhara yatokanayo na maafa nchini huku akisihi kuendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

 

“Ushirikiano huu ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa,”alisema Luteni Kanali Masalamado.

 

Alifafanua kuwa, Mamlaka inaendelea kuimarisha ushirikishwaji wa jamii na wadau ili kuendelea kukusanya maoni na taarifa mtambuka  kwa ajili ya kurahisisha ufungashaji wa taarifa hususani eneo la athari katika ngazi ya wilaya. Hivyo wadau wote ni wakati sahihi kuendelea kushirikiana na TMA ili kufanikisha zoezi la upatikanaji wa taarifa za kisekta.

 

“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa mvua za Vuli, kwa mwezi Oktoba hadi Disemba, 2023; ni muhimu sana kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa ukaribu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta yake”, alisisitiza Luteni Kanali Masalamado.

 

Sambamaba na hilo alihimiza na kuwasihi wadau wote kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Namba 2 ya mwaka 2019, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa vituo vya hali ya hewa vinasajiliwa kama ambavyo sheria inaelekeza.

 

Vilevile kwa watumiaji wa taarifa na huduma za hali ya hewa kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa mujibu wa sheria ili kuongeza tija na kupunguza athari za hali mbaya ya hewa.

 

Kwa upande Wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Ladislaus Chang’a alikieleza malengo ya mkutano huo wa wadau kuhusu Utabiri wa Vuli, Oktoba hadi Disemba, 2023 alisema unalenga kujadiliana na kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa mvua za Vuli utakavyoweza kutumika kwa tija katika sekta mbalimbali hapa nchini.

 

“Kwa kuzingatia umuhimu wa huduma za hali ya hewa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea na jitihada za kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwemo miundombinu na rasilimali watu. Hivyo, tunaishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo,” alisisitiza Dkt. Chang’a.

 

Aidha, akizungumzia kuhusu msimu huu wa Vuli, 2023 mifumo ya hali ya hewa inaonesha uwepo wa Hali ya El Nino ambayo ilianza kujitokeza mapema mwezi Juni, 2023 na imeendelea kuimarika. El Nino inatarajiwa kuendelea hadi mwanzoni  mwa mwaka 2024.

 

“Sambamba na mifumo mingine ya hali ya hewa, tathmini ya mwelekeo wa msimu wa Vuli 2023 itazingatia pia uwepo wa  hali hiyo ya El Nino na athari zinazoweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini hivyo tuendelee kuchukua tahadhari muhimu ikiwemo kuzingatia taarifa za utabiri zinazotolewa,” alisisitiza

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.