Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, amesema
mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, pamoja na Miradi mingine ya
kimkakati imeleta ajira na kuchangia kasi na chachu ya ukuaji wa uchumi hususan
katika Jiji la Dodoma.
Ameyasema hayoalipokuwa katika
ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Jengo la Mpigachapa Mkuu wa Serikali;
Jengo la Kituo cha Taifa cha Usimamizi na Uratibu wa Maafa, Jengo la Wizara
Mipango na Uwekezaji, na jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu).
Waziri Mhagama alisema kuwa,
ujenzi wa Mradi hiyo mikubwa ya kimkakati inayoendelea umewezesha vijana wengi
kupata ajira katika maeneo hayo, na kujiongezea pato binafsi sambamba na
kuchangia ukuajia wa uchumi kutokana na manunuzi ya bidhaa zinazotumika katika
mradi hiyo kufanyika katika viwanda vilivyopo nchini.
Alipokuwa katika jengo la
Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Waziri Mhagama alisema kuwa mradi huo, mkubwa
umefikia asilimia tisini na saba (97%) ambapo kiwanda hicho kitakapokamilika
kitakuwa na hadhi na sifa ya kuwa ni kiwanda kikubwa kimojawapo cha
Serikali,ambapo mashine mpya zimeagizwa na kiwanda hicho kitafanya kazi za ndani ya nje na nchi za
Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
"Sisi tumejipanga kwa
matumizi ya ndani na nje pia, nimefarijika kuona ujenzi kwa awamu, hii ya kwanza
umefikia hatua kubwa, na ujenzi wa Ofisi umeanza na unaenda kwa kasi."
Alisisitiza Waziri Mhagama.
Alipokuwa katika kituo cha
Taifa cha Uratibu na Usimamizi wa Maafa Mhe. Mhagama alisema, ujenzi wa awamu
ya kwanza ya kituo hicho pia umekamilika kwa Asilimia tisini na nne (94%) na
kufafanua kuwa maghala mawili makubwa na Ofisi za Watumishi zimeshakamilika.
"Tunalo jukumu la
kuhakikisha kwamba katika kituo hicho nchi inafikia malengo ya kitaifa na Maono
na maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa
Ujumla" Alibainisha Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama Alisema kuwa katika kituo hicho cha Maafa kutakuwa na vitu vingine
vingi ambavyo vinajenga dhana nzima ya uratibu na usimamizi wa Maafa, ambapo
kutakuwa na kiwanja ambacho, kitakuwa kinasaidia utuaji na uondokaji wa
Helkopta ambazo zitaweza kwenda kwenye shughuli za maafa, kutakuwa na kituo cha
tiba kitakachosaidia dharura za maafa hasa katika magonjwa ya milipuko na
kitatumika pia katika masuala ya utafiti na tiba na kituo cha mafunzo kwa wataalam
ambao watashughulika na usimamizi na uratibu huo wa dharura.
Waziri Mhagama pia alitembelea
na kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu)
pamoja na Jengo la Wizara ya Mipango na uwekezaji katika Mji wa Serikali
Mtumba, na kuagiza kuongezeka kwa kazi ya ujenzi ili majengo hayo yaweze
kukabidhiwa kwa wakati.
Kwa upande wake Naibu Katibu
Mkuu wa Ofisi Hiyo Bw. Anderson Mutatembwa, alisema Ofisi hiyo itasimamia
kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama, ikiwa ni pamoja na
kuzifanyia kazi chagamoto zilizojitokeza na kuhakikisha zinatatuliwa kwa
wakati.
Awali akizungumza katika ziara
hiyo, Mwakilishi na Msimamizi Mkuu wa miradi ya Ujenzi kutoka Chuo Kikuu cha
Ardhi Mhandisi Anania Saudeni, Alikiri kuyapokea maagizo ya Mhe. Waziri Mhagama
na kuyatekeleza kwa wakati, kimkataba na kukamilika katika ubora kulingana na
maelekezo na kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na Mchana na kuongeza nguvu kazi ya kutosha na usimamizi madhubuti.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.