IMEELEZWA KUWA, Suala la
Ufuatiliaji na Tathmini lina umuhimu mkubwa katika kuangalia utekelezaji wa
Mipango kuanzia ngazi ya mamlaka za chini hadi ngazi ya taifa katika utendaji
hususan kwenye miradi, ikilinganishwa na namna gani inakwenda sawasawa au
inatekelezwa kama ilivyopangwa.
Hayo yamesemwa leo jijini
Arusha na Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora Bw. Cosmas Ngangaji katika siku ya pili ya Kongamano la Pili la
Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea jijini humo ambapo amesema
kuwa Suala Ufuatiliaji na Tathmini linajikita zaidi katika vitendea kazi
vinavyotakiwa kutumika pamoja na michakato inayotumika kama inafanya kazi na
kuleta matokeo chanya hususan katika sekta ya Umma.
Akitolea mfano wa dhana ya
tathmini ya utoaji wa huduma za kijamii, Bw. Ngangaji alisema kuwa, miradi
mingi ya Serikali inatakiwa kuwekewa misingi endelevu ili wananchi waweze
kupata huduma sahihi na kwa wakati.
Akiongea katika kongamano hilo
Bw. Mussa Mshirazi Mbarouk kutoka Tume ya Mipango ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar alisema, suala la Ufuatilijai na Tathmini ni suala linalohitaji kujifunza
mara kwa mara ili kusaidia kujenga uwezo katika utendaji wa shughuli za kila siku.
Kongamano la Pili la Kitaifa
la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea Jijini Arusha limeingia katika
siku ya pili ambapo mada mbalimbali zimeendelea kuwasilishwa, ikiwa ni pamoja
na kuimarisha uelewa wa Tathmini, majadiliano bayana juu ya matokeo halisi na
mbinu muhimu za kuleta mbadiliko.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.