Wednesday, November 29, 2023

TAMWA YAHIMIZWA KUWEKA MKAZO AJENDA YA UHURU WA KUJIELEZA UNAOJUMUISHA SAUTI ZA WANAWAKE

 


Chama cha wahandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) kimetakiwa kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza unaojumuisha sauti za wanawake ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 36 ya chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Waziri, ametoa wito kwa (TAMWA) kuona umuhimu wa mijadala yenye mlengo wa kijinsia na uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, ulinzi na usalama wa waandishi wa Habari wanawake, na uhuru wa kujieleza kuwa kitovu cha kufanya maamuzi katika ngazi ya jamii kitaifa, na kimataifa.

“Tuadhimishe siku hii kutimiza ahadi zilizotolewa na kila Nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yote na hasa lengo namba tano linalozungumzia usawa wa jinsia,” alihimiza.

Aidha wadau mbalimbali wa habari watumie siku hii kusherehekea kwa kuungana na TAMWA kulinda na kuthamini haki za wanawake, haki za wasichana, haki za watoto, maadili ya kitanzania, na kupinga ukatili wa jinsia majumbani, hadharani na mitandaoni.

“Wamiliki wa vyombo vya Habari na waandishi wote kwa ujumla muungane katika jitihada za ulinzi na usalama wa waandishi wa Habari wanawake na hapa niwatie moyo waandishi wa Habari wanawake kuwa kazi yenu nzuri inaonekana pale mnapoweka jitihada ya kufanya kazi kwa weledi bila kukatishwa tamaa na vikwazo vya kimazingira.”Alifafanua

Waziri amesema kama kauli mbiu inavyosema, Uongozi Bora na Mchango wa Wanawake ni Chachu Kuelekea Tanzania yenye Maendeleo endelevu.

Hatuna budi kutambua kwamba suala la jinsia sio suala la wanawake peke yao bali ni suala la kuchochea maendeleo ya taifa letu miongoni mwa wanawake na wanaume, kwani ni jambo linalohimiza ushirikishwaji na ujumuishi usioacha kundi lolote nyuma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Technolojia ya Habari Bw, Selestine Gervas Kakele amesema inatambua Mchango wa (TAMWA) na wakati wote serikali itaendelea kuangalia ujumbe ambao TAMWA na asasi nyingine inatoa.

Tumepokea utafiti kuhusu unyanyasaji wa kijinsia: (TAMWA) kupitia utafiti huu imesaidia kuvunja ukimya, matokeo ya utafiti  hayalengi kunyoosha kidole kwa mtu, bali kushirikiana ili tuweze kuishinda vita hiyo.

“Tusimamie weledi na nidhamu ya kazi na pale vitendo hivi vinapojitokeza: wahanga wasikae kimya jitokezeni, pazeni sauti na serikali itasikia,” alifafanua.

Awali   Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Bi, Joyce Shebe amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mwaliko.

“Tumeona jinsi serikali ambavyo inapitia mifumo ya kisera na kisheria ilikuja na mipango inayopimika katika kuhakikisha ushirikishwaji na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na masuala yanayohusu usawa wa kijinsia inatatekelezeka” alibainisha

(TAMWA) tunaahidi kumuunga mkono kivitendo kwa sababu ni jukumu ambalo tumealianza tangu miaka 36 iliyopita

 

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.