Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi
kushirikiana na serikali kuwahifadhi waathirika wa Maporomoko ya Mawe na Matope
kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa
kikao na viongozi wa Serikali, Wazee na Waathirika wa Maporomoko hayo katika
Kijiji cha Gendabi Halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Mkoani humo.
Alitumia fursa hiyo
kuwakumbusha kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma zote muhimu kwa kila
aliyeathirika na maafa hayo na kipaumbele ni wale waliohifadhiwa katika Kambi
za muda zilizopo na endapo kuna mazingira rafiki ya kuhifadhiwa na ndugu, jamaa
na marafiki wanapaswa kufuata utaratibu zilizopo.
“Tunahitaji kupunguza
mikusanyiko mikubwa kwenye makambi kiafya siyo sahihi tutahakikisha
tunamhudumia kila Muathirika popote atakapokuwa amehifadhiwa na ndugu au Jamaa
na hakuna haki yake itakayopotea,” alibainisha
Aidha alishauri kuwa, Wananchi
wawapokee waathirika wa Maporomoko ya Mawe katika makazi yao na hata kama
nyumba itakuwa haitoshi serikali itawezesha kujenga mahema ili waweze
kujitosheleza.
Alifafanua zaidi kuwa lengo la
serikali ni kuhakikisha vifaa vya msaada wa kibinadamu vinawafikia waathirika
katika maeneo yao kwa kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu ikiwemo chakula,
magodoro pamoja na mablanketi.
“Sio kweli kwamba Muathirika
wa maporomoko ya Mawe na Matope akienda kwa ndugu zile stahiki zake atakosa,
cha msingi ni kuainisha eneo analokwenda kwa anuani, majina viongozi wake
pamoja na mawasiliano yao,”alifafanua.
Kwa upande wake Nyerere Izrael
Mwenyeji wa kijiji cha Gendabi ameomba serikali kutuma wataalamu kuangalia
tabia za Mlima Hanang’ ili janga hilo lisije likajirudia.
“Wataalamu watasaidia kutupa
taarifa za awali kama eneo ni salama au si salama kuendelea kuishi bila kuleta
taharuki kwa wananchi” alizungumza
Awali Bwana Steven Sulle
Mwenyekiti wa CCM Kata Gendabi, amemshaukuru, Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
amesema ni Rais wa kipekee kabisa ameonesha upendo na kutoa faraja katika
madhila haya.
“Niipongeze Serikali kwa
kutukimbilia sisi tunawashukuru sana, ila nashauri wale waathirika wenye uwezo
wa kwenda kwa ndugu , jamaa na marafiki watumie utaratibu uliopo na ni sahihi
kuwapokea kwa upendo, tunavyoendelea kuwaacha katika eneo la Kambi, wataendelea
kuwa wapweke zaidi,” alisema.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.