Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ameishukuru uongozi wa umoja
wa Makanisa ya Kipentencoste Tanzania (CPTC) kwa namna walivyoendelea kuonesha
upendo kwa kuchangia mifuko 500 ya saruji kwa waathirika wa maafa ya maporomoko
ya tope na mawe kutoka Mlima Hanang’ mkoani Manyara na kuendelea kuwaombea
waathirika hao.
Ameyasema hayo mapema katika
ibada iliyoandaliwa na umoja wa makanisa hayo iliyofanyika katika kanisa la
DNPC-Katesh.
Waziri Mhagama alishukuru
namna kanisa linavyoendelea kusaidia jamii katika malezi ikiwemo kuwalea kiroho
na kusema hii inasaidia Serikali kuwa na vijana na Taifa lenye maadili mema.
“Kanisa ni taasisi muhimu
sana, endeleeni kutushauri pale inapobidi na ninawashukuru namna mmeendelea
kuungana nasi katika maafa haya kwa kutoa mifuko ya Saruji nasi tutaiwasilisha
niwahakikishie itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa usimamizi mzuri wa
Serikali yetu,” alisema Mhe Mhagama
Mwenyekiti wa Makanisa ya
Kipentencoste Tanzania (CPTC) Dkt. Barnabas Mtokambali ameshauri jamii
kuendelea kuwaombea waathirika wa maafa hayo huku akitoa rai kuona umuhimu wa
kuwapa msaada kwa namna yoyote ili kusaidia na kuonesha upendo kwa matendo
lengo ni kuendelea kushikamana kama Watanzania.
“Ni wakati sahihi kuwakimbilia
ndugu zetu hawa, tuwaoneshe upendo na Serikali imechukua jukumu hili nasi
tuungane nao kwa kuwasaidia ndugu zetu na tukumbuke bado serikali inawahudumia
hata wakiwa katika makazi yetu,” alisema Mchungaji Mtokambali
Ametahadharisha uwepo wa
changamoto kadhaa zinazoweza kusababishwa na mikusanyiko ikiwemo magonjwa ya
milipuko, mmomonyoko wa maadili na tabia zingine zisizofaa na kuwaomba waumini
na jamii kwa ujumla kuendelea kuwaombea na kuwastiri kwa namna mbalimbali.
Naye Mbunge wa Hanang’ Mhe. Mhandisi Samwel Hayuma alieleza kuwa amefarijika kwa namna kanisa lilivyowakimbilia na kuendelea kuwaombea katika mapito ya maafa yaliyotokea Wilayani Hanang’.
Aidha alimshuku Mhe Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kutoa maelekezo kwa viongozi wake kuratibu na
kuhakikisha hali inarejea katika nafasi yake.”
“Mhe Waziri mhagama wewe ni mpambanaji kweli, umefanya kazi kubwa katika kuratibu maafa haya, hakika Serikali inafanya kazi nzuri sana na hii imetupa faraja kubwa kuona Serikali yote ipo hapa Hanang’ tunasema asanteni sana,” alisisitiza Mhandisi Hayuma
Aidha alitumia nafasi hiyo
kuwaasa Watanzania kuungana Pamoja kuendelea kumuombea mbeba maono wa nchi hii
ambaye ni Mheshimiwa Rais kwa namna anavyotuongoza Pamoja na wasaidizi wake
wote.
“Tuone umuhimu na haja ya
kuendelea kumuombea sana Rais wetu na viongozi wote wa nchi yetu, Tanzania ni
nchi nzuri yenye upendo wa hali ya juu, Tuendelee kuiombea Hanang’ yetu, Manyara
yetu na Nchi kwa ujumla,” alisema
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.