Sunday, January 21, 2024

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUREJESHA HALI KATIKA MIUNDO MBINU YA BARABARA ILIYOATHIRIKA NA MVUA

 Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulika na Sera, Bunge na Uratibu Mhe, Ummy Nderiananga amepongeza Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es salaam kwa jitihada mbalimbali za kurejesha hali katika maeneo ambayo miundo mbinu ya barabara imeathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake leo Mkoani humo alipotemebelea na kujionea athari za mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia tarehe 20/ januari/2024 na kuathiri maeneo mabalimbali ya wilaya ya Kindondoni, Temeke, Kigamboni, Ubungo na Jiji la Ilala.

Naibu Waziri Ummy alisema anampongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.  Abert Chalamila kwa uongozi ambao wameuonesha katika kurejesha halina kazi waliyofanya.

“Naomba tufanye kazi hii usiku na mchana ili tuweze kurejesha hali mapema bila kuathiri shughuli za biashara na shughuli nyingine za uchumi zinazofanyika katika Mkoa wa Dar es saalam,” alihimiza.

Sisi kama serikali tunawahakikishia wana Dar es salamu kwamba tutafanya kazi hii ya urejeshaji wa hali kwa nguvu bila kuchoka,

Naye Mkuu wa wilaya ya Kindondoni Mhe. Saad Mtambule amesema kazi waliyofanya ni kusimamia usafishaji wa mitaro na usawishaji wa mito na hivyo kusaidia maji kutotuwama kwa muda mrefu.

“Tumeendelea kuwaeleza wananchi walio katika maeneo ya pembezoni mwa mito kama; Mto Nyakasangwa, Mto Mpiji, Mto Tegeta, Mto Mlalakuwa na Mto Ng’ombe kuhamia maeneo ya juu ili kuepeuka athari za mvua,”alibainisha

Ujenzi wa nyumba holela umesababisha Watu kujenga mpaka kwenye mapito asili ya maji na kusababisha maji kukosa sehemu za kupita na kuingia maeneo ya watu

“Lakini pia tuna kazi ya kuendelea kuwaelimisha wananchi ili wafuate misingi ya ujenzi wa maeneo kulingana na ramani ya mipango Miji,” alisisitiza

Akizungumza katika ziara hiyo Mkazi wa Ununio Bw. James Koyi ameishukuru serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya urejeshajji wa hali katika maeneo yaliyoathirika mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoa wa Dar es salaam.

Hakuna aliyejua kama mvua itanyesha masaa ishirini na nne hata hivyo  serikali iendelee kufanya kazi katika kurejesha hali, alisema

Thursday, January 18, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA SERIKALI KWA USIMAMIZI MZURI WA KUKABILIANA NA MAAFA


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu kwa Usimamizi mzuri wa kukabiliana na  Maafa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama  wakati wa wasilisho lililohusu  namna Serikali ilivyojipanga katika kukabiliana na maafa pamoja na mfumo  wa usimamizi wa Uratibu wa maafa katika kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Vituo vya utoaji huduma za matibabu kwa waraibu wa Dawa za kulevya nchini lililowasilishwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama leo Bungeni Jijini Dodoma.

Mwenyekiti huyo  alisema Serikali ilifanya kazi kubwa  nayakupongezwa kutokana na jitihada zilizofanyika kuhakikisha waathirika wa mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanag mkoani Manyara wanaokolewa na kurejesha hali.

 “Tunapongeza sana Uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kazi mliyofanya ni kubwa ya kuokoa maisha ya wananchi na mal zao licha ya baadhi yao kupoteza maisha kama kamati tunawapongeza sana,” Alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Mhe. Dkt. Mhagama alisema, inatia moyo sana kuona Wizara ama idara inazozisimamia zinafanya kazi ambazo watanzania wanazitarajia kwa hiyo kamati nayo inajiskia kama ni sehemu ya hayo mafanikio makubwa yaliyopatikana.

“Maafa ni majanga lakini tunapokabiliana nayo na kuyafanyia kazi vizuri inatupa nguvu sasa, tunapenda tukupongeze Mhe. Waziri Jenista Mhagama, Katibu Mkuu  Dkt. Jim Yonazi na Watendaji wako wote kwa moyo wa uzalendo mliouonyesha katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilipitia,” Alieleza Mhe. Dkt. Mhagama.

Vilevile Kamati pia ilipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kukabilana na madawa ya kulevya kwa kazi nzuri inayofanya ya kujenga vituo vya Uraibu na kushauri kujengwa vituo zaidi kwa Mikoa ya kusini pamoja na kuendeleza mapambano ya uzalishaji na biashara ya Dawa za kulevya kama vile Bangi,Mirungi na dawa nyingine.

Akitoa maoni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Edward Olekaita Kisau, alifafanua kwamba namna Serikali ilivyokabiliana wakati wote wa maafa na baada ya maafa ili kuhakikisha inarejesha hali na shughuli kuendelea kama ilivyokuwa awali na janga la Hanang’ ni mfano mzuri unaoweza kuchukuliwa katika uratibu mzima wa masuala ya kukabiliana na majanga nchini.

Naye  Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Dkt Alice Kaijage  akitoa maoni kuhusu wasilisho la Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Vituo vya Utoaji wa Huduma za Matibabu kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya nchini  alibainisha kuwa  ni wakati mzuri sasa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) kuongozewa fedha za maendeleo kwani kazi inayofanywa na mamlaka hiyo ni kubwa na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.

Awali akiwasilisha taarifa hizo mbele ya kamati hiyo Waziri wa Nchi Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo  imeendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia majukwaa mbalimbali kwa lengo la kuijengea  uelewa na uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kupunguza madhara yanayotokana na maafa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu  kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa maafa kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na vifaa, Serikali imefanya manunuzi na kuratibu upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya msaada wakati wa dharura na kuvihifadhi katika maghala ya kuhifadhia vifaa vya misaada ya kibinadamu ili kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na maafa,” Alieleza Mhe. Jenista.

Aidha  Waziri huyo  alitoa wito kwa wananchi kutokudharau utabiri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwani mamlaka ina vifaa vinavyoendana na teknolojia ya kisasa ambapo  utabiri wa hali ya hewa  kwa wakati huu, umekuwa na  una usahihi wa asilimia 85% mpaka 95%.

 

Monday, January 15, 2024

WANANCHI WAOMBWA KUENDELEA KULINDA AMANI NA MSHIKAMANO WA KITAIFA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuzilinda tunu za umoja wa kitaifa za utulivu, amani  na ushirikiano. 

Rai hiyo ametoa wakati akimwakilisha Mheshimiwa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Katika Misa ya kuweka wakfu Askofu wa Jimbo la Njombe Dkt. Eusebius Samwel Kyando iliyofanyika Mkoani Njombe

Waziri amesema kuwa tunu hizo ndizo zinazotambulisha  Taifa letu la Tanzania duniani na ulimwenguni kote.

"Tunu hizi zilindwe kwa kuzingatia umuhimu wake, pia Serikali inashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa, tunaomba muendelee kuliombea bila kuchoka "  alifafanua Waziri 

Aidha  viongozi wa dini mmekua mstari wa mbele kuhakikisha Taifa hili linaendelea kuwa katika hali ya utulivu mstahimilivu na Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele Kati Jambo hilo.

"Niwaombe Sana Viongozi wa dini tuendelee kukemea pale tunapoona kuna viashiria vya watu wachache kuvunja amani, utulivu umoja na mshikamano wa Nchi yetu," alihimiza

Aidha aliitaka jamii kuungana na Serikali katika kupaza sauti juu ya matendo maovu na hasa mauaji na ukatili wa kijinsia, imani potovu ambazo zinapelekea mauaji na unyanyasaji wa watoto.

Aliongezea kuwa Falsafa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani ya 4R,  inalenga sekta zote na utendaji wote ndani ya serikali, na utendaji wa waumini na taasisi zake za kidini hivyo, aliwaombe viongozi wa dini kuunga mkono falsafa hiyo hasa katika ustahimilivu na maridhiano.

"Dhamira ya Mhe. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani ni njema na inahitaji kutiwa moyo ili iweze kusonga mbele hasa kwa vitendo," alisisitiza

Akizungumza kuhusu masuala ya uchaguzi na fursa zilizopo aliisihi jamii  kuwa tayari kuitumia kwa kushiriki vyema uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

“Uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka huu 2024, niwaombe wananchi tuweze kushiriki zoezi la uchaguzi huo kwa amani na utulivu,” aliongeza

 

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka ameomba viongozi wa dini kwa kushirikiana na serikali kwa pamoja kuunga mkono jitihada zinazofanywa katika sekta ya elimu hasa katika masuala ya lishe kwa wanafunzi mashuleni katika  kukabiliana na tatizo la utapiamlo.

"Hii itasaidia kuleta hamasa kuwaandaa watoto kwa kuwapatia lishe Bora ambayo itawasaidia kufanya vizuri katika maisha yao,"Alisema.

Kwa upande wake mmoja wa waumini wa kanisa hilo Bi, Naomi Nzota amesema waumini wa Jimbo la Njombe wamefurahi Sana kwa kupata Askofu Dkt. Eusebius Kyando baada ya Misa wa kuweka wakfu iliyoongozwa na Muasham Askofu Mstaafu wa Jimbo la Dar es salaam Polcapy Pengo.

"Ameueleza utumishi wa Askofu Dkt. Eusebius Kyando kwamba ni mtumishi, mnyenyekevu mnyoofu na mvumilivu," alieleza

 

 

Monday, January 8, 2024

VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUWEKA MKAZO KATIKA KUSIMAMIA MAADILI.

 



Viongozi wa dini wameombwa kuendelea kusimamia imara na kukemea matendo maovu yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hususan kwa vijana hasa katika mazingira ya yanayoendeshwa zaidi na ulimwengu wa kidijitali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan katika Ibada Maalum ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi, Mkoani Iringa.

Waziri amehimiza malezi bora kwa watoto na ikiwezekana jamii kurejea utamaduni wa kitanzania wa mtoto kulelewa na kuonywa na jamii nzima inayomzunguka.

“Serikali inatambua kuwa Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwahimiza wananchi maadili mema na maisha ya uadilifu,” Alifafanua

Waziri amenukuu maandiko Matakatifu kutoka Waraka wa Mtume Paul kwa Wagalatia Sura ya 6: 1-3 yanayosihi kuonya na pale inapobainika mmoja katika jamii amekwenda kinyume kwa kutenda kosa lolote. 

Amewaaomba viongozi hao kueendelea kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ili kulilinda Taifa dhidi ya janga la mmomonyoko wa maadili.

“Tunaamini kwa kupitia Imani yetu na kukua kwa kanisa, ni kukua kwa Imani ya dini, hivyo kutachochea maadili na kusaidia kupambana na vitendo vibaya vya rushwa na kuimarisha utawala bora” Alibainisha

Aliendelea kusema kuwa, Mambo mazuri yatakayofanywa na washirika wa Dayosisi hiyo yataleta ari na chachu kwa watu wengine ambao sio wanashirika Dayosisi.

Waziri amesema kwamba licha ya Nchi ya Tanzania kutoegemea upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) sehemu kubwa ya wananchi wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.

Aidha, Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutambua uwepo wa dini nchini na umuhimu wake katika kulinda tunu za amani na utulivu pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri ametumia nafasi hiyo kupongeza na kushukuru Kanisa la Kilutheri Tanzania hasa kwa wale waliopata Dayosisi mpya na Mhashamu Askofu Mpya, kuwana matarajio makubwa sana kwa Dayosisi hiyo Mpya.

 

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Mufindi Muhasham Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula, amesema kanisa linahitaji kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya kujitegemea ili kusaidia vijana kupata ujuzi.

Alisema, Elimu ya Ufundi ni muhimu sana kwa vijana hasa wanaomaliza elimu ya msingi bila kwenda sekondari na wanaomaliza elimu ya sekondari bila kwenda juu zaidi.

“Kanisa linajipanga kuendeleza elimu ya ufundi katika chuo chetu cha Mafinga Lutheran vocation centre ikiwezekana kuanza mchepuo ufundi kama tawi la chuo kikuu kisaidizi cha Iringa,” Alisema Baba Askofu

Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ameomba Viongozi wanaomsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa dhati na kuepuka kuunda makundi ya kumkwamisha.

Tunamuombea Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassani na tunamuunga mkono yeye pamoja na wengine wote wenye mamlaka na nafasi katika nchi yetu.

“Tunaomba kila mmoja asimame kikamilifu katika nafasi yake awatumikie watanzania wasasa na vizazi vijavyo,” alifafanua Mhashamu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.