Viongozi wa dini wameombwa
kuendelea kusimamia imara na kukemea matendo maovu yanayopelekea mmomonyoko wa
maadili hususan kwa vijana hasa katika mazingira ya yanayoendeshwa zaidi na
ulimwengu wa kidijitali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati
akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu
Hassan katika Ibada Maalum ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi, Mkoani Iringa.
Waziri amehimiza malezi bora kwa
watoto na ikiwezekana jamii kurejea utamaduni wa kitanzania wa mtoto kulelewa
na kuonywa na jamii nzima inayomzunguka.
“Serikali inatambua kuwa
Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwahimiza wananchi maadili mema na
maisha ya uadilifu,” Alifafanua
Waziri amenukuu maandiko
Matakatifu kutoka Waraka wa Mtume Paul kwa Wagalatia Sura ya 6: 1-3 yanayosihi
kuonya na pale inapobainika mmoja katika jamii amekwenda kinyume kwa kutenda
kosa lolote.
Amewaaomba viongozi hao kueendelea
kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ili kulilinda Taifa dhidi ya janga la
mmomonyoko wa maadili.
“Tunaamini kwa kupitia Imani
yetu na kukua kwa kanisa, ni kukua kwa Imani ya dini, hivyo kutachochea maadili
na kusaidia kupambana na vitendo vibaya vya rushwa na kuimarisha utawala bora”
Alibainisha
Aliendelea kusema kuwa, Mambo
mazuri yatakayofanywa na washirika wa Dayosisi hiyo yataleta ari na chachu kwa
watu wengine ambao sio wanashirika Dayosisi.
Waziri amesema kwamba licha ya
Nchi ya Tanzania kutoegemea upande wowote katika masuala ya dini (Secular
State) sehemu kubwa ya wananchi wanaamini katika Mungu kupitia dini na
madhehebu mbalimbali.
Aidha, Alifafanua kuwa
Serikali inaendelea kutambua uwepo wa dini nchini na umuhimu wake katika
kulinda tunu za amani na utulivu pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na taasisi
za dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Waziri ametumia nafasi hiyo
kupongeza na kushukuru Kanisa la Kilutheri Tanzania hasa kwa wale waliopata
Dayosisi mpya na Mhashamu Askofu Mpya, kuwana matarajio makubwa sana kwa
Dayosisi hiyo Mpya.
Kwa upande wake Askofu wa
Jimbo la Mufindi Muhasham Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula, amesema kanisa
linahitaji kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya kujitegemea ili kusaidia
vijana kupata ujuzi.
Alisema, Elimu ya Ufundi ni
muhimu sana kwa vijana hasa wanaomaliza elimu ya msingi bila kwenda sekondari
na wanaomaliza elimu ya sekondari bila kwenda juu zaidi.
“Kanisa linajipanga kuendeleza
elimu ya ufundi katika chuo chetu cha Mafinga Lutheran vocation centre
ikiwezekana kuanza mchepuo ufundi kama tawi la chuo kikuu kisaidizi cha
Iringa,” Alisema Baba Askofu
Akitoa neno la shukrani Mkuu
wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Askofu Dkt. Fredrick Shoo,
ameomba Viongozi wanaomsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa
dhati na kuepuka kuunda makundi ya kumkwamisha.
Tunamuombea Mhe. Rais Dkt,
Samia Suluhu Hassani na tunamuunga mkono yeye pamoja na wengine wote wenye
mamlaka na nafasi katika nchi yetu.
“Tunaomba kila mmoja asimame
kikamilifu katika nafasi yake awatumikie watanzania wasasa na vizazi vijavyo,”
alifafanua Mhashamu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.