Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama
ametoa shime kwa Baraza la Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na
sekta binafsi na wadau mbalimbali kutambua mawanda makubwa ya uwekezaji yaliyo
katika nchi yetu.
Kauli hiyo ameitoa wakati
akizungumza katika Kongamano la Nne la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika
Miradi ya kimkakati na uwekezaji lilofanyika katika ukumbi wa Benki kuu ya
Tanzania (BOT) Jijini Dar es salaam.
Waziri Mhagama amesema kuwa
sekta binafsi na wadau mbalimbali waendelee kutoa mapendekezo kwenye fursa
mbalimbali zinazojitokeza za kiuchumi ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya
kiuchumi kufikia malengo yaliyopo.
Ameongeza kusema wananchi wa
Tanzania wako tayari, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuwa ameonesha kwa vitendo kwamba yuko tayari hivyo ni vyema kumuunga mkono
kwa kufanya kazi ili kujenga uchumi wa Taifa.
Aidha jukwaa hilo litasaidia
kujenga uelewa wa pamoja juu ya mafanikio yaliyopatikana na katika uwekezaji na
ustawi wake wa kiuchumi.
Waziri aliongezea dhana ya
kongamano hilo lenye kauli Mbiu ya
“Wekeza Tanzania kuongeza thamani ya ziada” linatumika kujenga uchumi imara
ambao umeshirikisha Watanzania wengi.
“Na itatutengenezea mazingira
mazuri ya biashara ambayo yatachochea wananchi wengi katika uwekezaji na
ushiriki wao katika kujenga uchumi,"alisema Waziri Mhagama
Baraza la Uwekezaji wa
Wananchi Kiuchumi limeingia makubaliano na taasisi ya serikali inayosimamia
manunuzi ya umma, katika moja ya kipengele katika sheria ya manunuzi ya umma
kinachosisitiza kila asilimia 30 ya manunuzi ya umma ya kila mradi yaende kwa
vijana, wanawake wazee na watu wenye ulemavu ambayo ni sehemu ya uwezeshaji wa
wananchi kiuchumi.
Kwa upande wake Bibi, Beng’i
Issa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi wa Kiuchumi
(NEEC) amesema moja ya mambo wanayosimamia ni kuangalia kampuni zinazopata kazi
kwenye miradi ya kiuchumi na bidhaa zinazouzwa katika miradi hiyo zinatoka nchini.
Aidha kwenye ajira Baraza la
Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi linaangalia ajira za moja kwa moja na ajira
ambazo sio za moja kwa moja katika uhaulishaji wa teknolojia kwa kusimamia
teknolojia nchini na mipango ya kutoa mafunzo ya kuhaulisha inafanyika
Akizungumzia kuhusu kongamano
amesema kongamano hilo la Nne limelenga katika kujenga uelewa wa pamoja kuhusu
ushiriki wa watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa
nchini pamoja na kushirikishana mafanikio na changamoto zilizopo katika
ushiriki wa watanzania katika uwekezaji.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.