Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za tiba kwa waraibu
wa dawa za kulevya ili
kuhakikisha wanareejea katika hali zao za awali na kushiriki katika shughuli za
maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi kuhusu
Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya nchini kwa
mwaka 2023 katika Ukumbi wa Habari Bungeni Jijini Dodoma iliyoelezea
mafanikio yaliyopatikana katika vita dhidi ya dawa hizo.
Mhe. Jenista alisema, mwaka 2023, Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya dola vilifanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,965,340.52 za dawa
za kulevya aina ya heroin, cocaine, methamphetamine, bangi, mirungi, skanka na
dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuwakamata watuhumiwa 10,522.
“Takwimu
za mwaka 2023 zinaonyesha mafanikio makubwa, kwani kiasi cha dawa za kulevya
kilichokamatwa ni kiasi kikubwa kuliko kiasi kilichokamatwa wakati mwingine
wowote nchini. Kiasi hiki ni karibu mara tatu ya kile kilichokamatwa kuanzia
mwaka 2012 hadi 2022, ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa
wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kupambana na janga hili” alisema Mhe.
Jenista.
Alieleza kwamba hadi kufikia mwezi
Disemba 2023, vituo vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya
(MAT Clinics) vilivyohudumia waraibu 15,912 vilifikia 16, na nyumba za upataji
nafuu (Sober Houses) na 56 zilizohudumia waraibu 3,488.
Waziri Jenista aliendelea kubainisha
kwamba jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine
walipata huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini huku
akisema Serikali imeanza ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao kwa ajili
ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.
‘Kituo hiki kitajengwa katika eneo la Itega
Jijini Dodoma na kitasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya
waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na kuepuka kurejea kwenye matumizi
ya dawa za kulevya,”Alieleza.
Vilevile
ameeleza kuwa, serikali imeweka jitihada kubwa katika kuzuia matumizi ya dawa
za kulevya nchini kwa kuimarisha elimu na mikakati ya kukabiliana na tatizo
hili kupitia vyombo vya habari,
mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano, vilabu vya kupinga rushwa
na dawa za kulevya shuleni na vyuoni.
Akibainisha mafanikio yaliyopatikana Waziri
Jenista alieleza kwamba, mwaka 2023, Serikali ilianzisha kituo maalumu cha
Habari na Mawasiliano (Call Centre) kilichopo katika ofisi za DCEA ambapo
wananchi wanaweza kupiga simu namba 119 bila malipo na kutoa taarifa za
wahalifu wa dawa za Akikulevya au kupata elimu juu ya madhara ya dawa za
kulevya.
“Serikali imefungua Ofisi mpya tano za
Mamlaka katika ngazi ya kanda ambazo ni nyanda za juu kusini ambayo ofisi zake
ziko Mkoa wa Mbeya inahudumia Mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa Njombe na
Iringa. Kaskazini ofisi zake ziko Mkoa wa Arusha inahudumia Mikoa ya Arusha,
Manyara Kilimanjaro na Tanga,”Alitaja Mhe. Jenista.
Akiendelea
kutaja Mikoa hiyo alisema kuwa ni Pwani ambayo inatoa huduma katika Mkoa
wa Mtwara, Lindi, Ruvuma na Morogoro wakati Kanda ya ziwa ambayo ofisi
zake ziko Mkoani Mwanza inahudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu
na Shinyanga, pamoja na Kanda ya kati yenye ofisi Mkoani Dodoma inayohudumia
Mikoa ya Dodoma, Kigoma Singida na Tabora.
Pamoja na mafanikio hayo alifafanua
kwamba bado Serikali imeendelea kuwekeza katika udhibiti
wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2023 imenunua boti yenye kasi (Speed Boat)
itakayotumika kufanya doria baharini kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya
kama vile heroine na methamphetamine.
Katika hatua nyingine Mhe. Jenista
alisema Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa
za Kulevya ya Mwaka 2024 ili kuhakikisha ushiriki wa wadau wote katika
mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
“Sera hii itaimarisha udhibiti wa dawa za
kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi. Pia itatoa maelekezo
ya kufanya utafiti wa mazao mbadala katika maeneo yanayolima mazao haya ili
wananchi wapate kilimo cha mazao halali. Zaidi ya hayo, sera hii inaelekeza
kuwajengea uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ili
kuboresha ufanisi wa mapambano haya,” alisisitiza Mhe. Jenista.
Aidha Mhe. Jenista alitoa wito kwa jamii
kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza
kuwa elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya inapaswa kuanzia ngazi
ya familia pamoja na Wazazi na
walezi kushiriki katika kwa kuwajengea misingi bora watoto wao
ili wasijiingize kwenye vitendo viovu na makundi hatarishi yanayoweza
kuwaingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.