Saturday, June 29, 2024

SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MKAZO WA KUONDOA VIJANA KWENYE URAIBU WA DAWA ZA KULEVYA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inaendelea kuweka nguvu katika kuondoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya kwa kuhakikisha inawapa tiba vijana hao ili warudi katika hali zao za kawaida.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelea Mabanda ya Taasisi mbalimbali kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Dunia 2024 zinazofanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana.

"Tumeshuhudia vijana wengi waliotoka kwenye uraibu wa dawa za kulevya wamerudi kuwa rai wazuri wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na wameamua kujitokea kuokoa vijana wenzao," alisema Waziri Mhagama

Waziri Mhagama alifafanua kwamba, serikali imeshajenga kituo Jijini Dodoma cha urekebishaji ambacho kitakuwa kinatoa tiba ya kutoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya na kufundisha mafunzo ya ujuzi.

Aidha Serikali inaendelea kutekeleza kwa nguvu kubwa kwenye matamko ya kisera ili kuweza kuhakikisha inaokoa vijana kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

"pia tunaamini Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine tukifanya kwa pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa sana," alisema

Waziri Mhagama alisema  tafiti zilizofanyika mtumiaji akitumia dawa za kulevya anatumia masaa sita kwa kilevi ambacho kinamsababishia kulala na kutojitambua masaa sita, jambo ambalo linamnyima uwezo wa kufanya kazi, anapopata fahamu anakuwa dhaifu na hawezi ufanya kazi yoyote na anapokosa fedha ya kununua madawa inamsababisha kuingia kwenye matendo ya jinai.

Awali katika zoezi hilo Waziri Mhagama aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi.

 

 


Sunday, June 9, 2024

WAZIRI MHAGAMA AIPONGEZA SUKOS KOVA FOUNDATION KWA KUANDAA MAFUNZO YA UOKOAJI


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama amepongeza taasisi ya Sukos Kova Foundation na taasisi ya Peaceland Foundation kwa pamoja kwa kushirikiana taasisi za uokoaji Serikalini kwa kuandaa mafunzo maalumu ya uokoaji kwenye maji.

Ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kufungua mafunzo hayo yaliyohusisha vikosi vya Jeshi la Polisi Wanamaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vikundi mbalimbali vya uokoaji katika ngazi ya jamii iliyofanyika Sawasawa Bay Mikocheni, Dar es salaam.

Amesema boti iliyokabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaenda kwenye maziwa mito na maeneo mbalimbali ili ikakutane na taasisi za uokoaji na vikundi vya jamii ambavyo vitakuwa tayari kwa mafunzo.

Waziri Mhagama amesema, “maamuzi hayo ni ya kizalendo na tutaendelea kuheshimu uwepo wa taasisi hizo binafsi, ikiwa ni pamoja na utaratibu ambao zitakuwa zimejiwekea katika kuleta tija kubwa kwa taifa na ustawi wa Watanzania.”

Aliongezea kuwa matumizi ya uokoaji yanaenda sambamba na matumizi ya vifaa hivyo na kutoa wito juu ya utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa, kwa wakati sahihi na mahali sahihi pale ambapo vitahitajika ili viweze kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

"Boti iliyokabidhiwa ni boti ya kisasa na kwa sababu mambo ya uokoaji ni mambo mtambuka yataenda sambamba na uzuiaji wa uhalifu, na inaweza kutumika pia kuzuia uhalifu kwenye maeneo ya maji katika Taifa letu.”alisema Mhe. Mhagama

Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za kiraia ili kuweza kufika maeneo mbalimbali yenye uhitaji wa kupata mafunzo ya uokoaji.

Aidha alitoa rai kwa taasisi za uokoaji na vikundi vya uokoaji kuhakikisha wanatunza vifaa vilivyotolewa ili viweze kudumu kwa muda mrefu huku vikiendelea kutoa msaada wa uokoaji .

Watakaopokea mafunzo watumie vizuri maarifa hayo ili waweze kufunza wengine na kusaidia kundi kubwa  kunufaika na mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa muda wa wiki mbili, alisistiza

Waziri amesema, “ni vyema taasisi za uokoaji na vikundi vya uokoaji vikatumia elimu itakayotolewa kwa uzalendo mkubwa pindi tutakapokutana na majanga ya maafa.”

Waziri Mhagama alizikumbusha taasisi Sukos Kova Foundation kuendelea kufungua milango ili taasisi nyingine ambazo zinapenda kufanya ushirikiano na taasisi hiyo kwenye masuala ya uokoaji wawe tayari kushirikiana.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt, Koba Nguvila amesema Mkoa wa Dar es salaam unaguswa kwenye habari ya uokoaji na mafaa kwa sababu Mkoa huo unapata mafuriko na madhila ya kuchafuka kwa bahari.

Amesema kuwa hili ni jambo la faraja kwa taifa, pindi inapotokea jamii imezungukwa na maji unatumia vifaa vya kisasa vya uokoaji hivyo kusaidia kuimarisha usalama  wa kuokoa watu.

Naye Kamishna Mstaafu Suleiman Kova, amesema ya Sukos Kova Foundation kwa kushirikiana taasisi ya Peaceland Foundation wametoa boti Moja ili liweze kuogeza nguvu katika miundombinu iliyopo kazini.

"Tumeona tumpatie Jaketi la Uokoaji (Life JacketRais) Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa sababu amekuwa mstari wa mbele kutoa maelekezo makubwa wakati Maafa yanapotokea," alisema

Awali Mkuu wa Wajumbe kutoka Peaceland Foundation Bi. Jing Ping, amesema nchi ya China na Tanzania wamekuwa na ushirikiano na mshikamano wa karibu kwa zaidi ya miongo sita sasa.

"Nchi zetu zimekuwa zikisaidiana katika mambo mbalimbali na tukio la leo ni moja ya ushahidi wa ushirikiano wetu, na katika hili taasisi yangu kwa kushirikiana na Sukos Kova Foundation zimejikita katika kuimarisha juhudi za kukabiliana maafa kwa kutoa vifaa mbalimbali vya kusaidia uokoaji.

Monday, June 3, 2024

“MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI KUBADILI DHANA YA UTENDAJI SERIKALINI” WAZIRI MHAGAMA

 


Taasisi za Umma zimetakiwa kufanya tathmini za awali ya hali ya utekelezaji wa mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika taasisi zao na kuwasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu kabla ya tarehe 15 Julai, 2024.

Maagizo hayo yametolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya Uzinduzi wa nyaraka za msingi za Ufuatiliaji na Tathmini nchini na utiaji sahihi mikataba ya makubaliano katika kuimarisha shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini nchini.

Waziri Mhagama amesema kuzinduliwa kwa mwongozo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika Ufuatiliaji wa Tathmini na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tathmini hizo katika kufanya maamuzi na kuboresha utekelezaji na  utendaji katika ngazi zote.

“Katika kutekeleza mwongozo huu, ninaelekeza Taasisi za Umma kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Tathmini zote zilizofanyika kwa mwaka wa fedha 2023/24 na zinazotarajiwa kufanyika kwa mwaka wa fedha 2024/25 ili Ofisi yangu iweze kuandaa Mpango wa Tathmini wa mwaka 2024/25 na kufuatilia utekelezaji wake," amesema Mhe. Mhagama

Aidha katika kutekeleza mwongozo huo Mhagama ameelekeza yafuatayo:-Kufanya Tathmini ya Awali ya hali ya utekelezaji wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika Taasisi zao (M&E Readiness Assement), Kuandaa Mwongozo wa Matumizi (Operational Manual) ambao unaeleza utekelezaji wa Ufuatiliaji na Tathmini wa kila siku katika taasisi zao. Mwongozo huo uoneshe namna ambavyo vitengo, idara au sehemu za U&T zitakavyofanya kazi kwa kuzingatia Mwongozo huu.

Maelekezo mengine ni pamoja na Kuandaa Mpango wa Ufuatiliaji (Monitoring Plan) kwa kuonesha maeneo na kazi zote zitakazofuatiliwa kila siku kulingana na Mpango Kazi wa Taasisi (Action Plan) na mipango ya utekelezaji wa afua mbalimbali, Kuandaa Mpango wa Tathmini (Evaluation Plan) kwa kuonesha tathmini za afua za maendeleo zitakazofanyika katika kipindi husika.

Sambamaba na hayo ameelekeza Kuandaliwa kwa moduli za utendaji zinazojumuisha viashiria muhimu vya kupima utendaji wa Taasisi,Kuteua wataalamu (U&T Champions) kutoka Idara na Vitengo vyote vya taasisi husika. Wataalamu hao watashirikiana na Idara/Kitengo cha U&T katika utekelezaji wa Mwongozo huu.

 Pia amewasisitiza  Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakurugenzi wa Vitengo vya U$T katika Taasisi zote za Umma kuendelea kuimarisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vilivyoanzishwa kwa kutengewa bajeti ya kutosha kutekeleza shughuli zake na kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi waliopo katika vitengo hivyo na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya tathmini za mara kwa mara za utekelezaji wa Sera, Mipango, Miradi na Programu mbalimbali za Serikali na kuwasilisha taarifa hizo Ofisi ya Waziri Mkuu.

 Awali akitoa neno la utangulizi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amefafanua miongozo  iliyozinduliwa kuwa ni Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini unalenga kuziongoza taasisi za umma kuhusu namna ya kutekeleza majukumu ya Ufuatiliaji na Tathmini. Mwongozo huu umeainisha hatua za kufuata katika ufuatiliaji, ufanyaji wa Tathmini, maandalizi ya viashiria na kupima utendaji wa shughuli za Serikali.

Pia umezinduliwa Mwongozo wa Tathmini ya utayari wa Taasisi za Umma katika kutekeleza shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini umelenga kutathmini uwezo, udhaifu, fursa na changamoto zinazokabili taasisi za umma katika kutekeleza shughuli za ufuatiliaji na tathmini na hivyo kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha.

Aidha Mwongozo mwingine ni Mwongozo Kitaifa wa Tathmini (National Evaluation Guideline) unalenga kutoa namna bora ya kuratibu na kusimamia tathmini nchini. Kimsingi mwongozo huu unalenga kuhakikisha mipango ya tathmini inafuatwa, matokeo ya tathmini yanatumika na utamadumi wa kufanya tathmini unajengwa.

Dkt.Yonazi amesema utekelezaji wa miongozo hiyo kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini (Government wide integrated M&E System)

“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao, ipo katika mchakato wa maandalizi ya Mfumo huo.  Kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia katika ukusanyaji, uchakataji na utoaji wa taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini kwa wakati (real time data) na pia kuwezesha upimaji utendaji kazi utakaochangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alieleza Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uzinduzi huo huku akieleza kuwa hatua hii ni jambo zuri na kukumbusha kuwapa nafasi wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmnini ili kuyafikia matarajio ya Tanzania ya sasa na ya baadae.

Naye Bw. Kadari Singo Mkuu wa Taasisi ya Uongozi amesema upo umuhimu wa kuendelea kusimamia vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara na Taasisi zetu ili kusaidia kuleta matokeo yanayokusudiwa na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

“Ni vyema kukawa na desturi ya kufanya tathmini kuanzia mtu mmoja mmoja, nafasi ya familia, jamii na katika maeneo yetu ya kazi hii iwe ni sehemu ya maisha ya kila mmoja na kusadia kujua wapi unaenda sawa na wapi urekebishe na kuepuka kuenenda bila malengo,” alieleza Bw. Singo

Aliongezea kuwa, ili kuendelea kuwa na matokeo katika utendaji kazi wa kila siku, jamii haina budi kubadili mtazamo na kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya tathmini na ufuatiliaji kama nyenzo ya kujipa nafasi ya kufanya vizuri zaidi kuliko ambapo isingefanyika.

 

Saturday, June 1, 2024

“MAENDELEO YA SAYANSI NA TEKHNOLOJIA YAENDELEE KUTULETEA MABADILIKO CHANYA” WAZIRI MHAGAMA

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ameomba wanawake kuendelea kuliombea Taifa na kuombea kizazi kilichopo na kizazi kijacho ili kiendelee kuwa na hofu ya Mungu.

 Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Kongamano la Wanawake wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania ambalo limefanyika Sasaba Jijini Dar es salaam likiongozwa na kauli Mbiu, yake inayosema, Mwanamke ni Jeshi kubwa kwa Kanisa na Taifa.

 Ameeleza kwamba mabadiliko ya Sayansi na Tekhnolojia yanapaswa kuendelea kutusaidia kumjua Mungu kwa haraka na hayapaswi kutuingiza kwenye changamoto za kidunia. Licha ya kwamba nchi yetu haiegemei upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) lakini sehemu kubwa ya watu wake wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.

 “Tukifanya kazi hii vizuri tutakuwa tumelitendea haki Taifa, na naomba niendelee kutoa wito kwa wakinamama na watoto (CPCT) muendelee kubaki imara kwenye kanisa na Taifa letu,” alihimiza Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amezungumzia pia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo ametoa rai kwa wakinamama kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, ili chaguzi hizo zipite salama na tushawishi wanawake wenye uwezo wagombee.

 “Mwanamke akipata nafasi ya kuongoza Kijiji au Mtaa na akiwa ametoka kwenye Jeshi kubwa la kuliombea Taifa atafanya kazi weledi,” alitanabaisha

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Mhashamu Askofu Dkt. Barnabas Mtokambali Amesema umoja huo uliundwa na Hayati Ali Hassani Mwinyi aliyekuwa Raisi wa awamu ya pili ambaye aliridhia kuundwa kwa Umoja wa Baraza hilo mwaka 1993 na Makao yake Makuu yalikuwa Jijini Dar es Salaam.

 “Baraza hili linabaraka zote za madhebu ya kipentekoste na Baraka za Nchi na tumeunda Idara na Mabaraza kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya ikiwemo Idara hii ya wanawake ambayo inatimiza maono, na dhima iliyokusudiwa alisema,” Mhashamu Askofu Dkt. Barnabas Mtokambali

Ikumbukwe Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) limetimiza miaka 31 tangu kuundwa kwake, na lina idara 9 ikiwemo Idara ya Wanawake wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania lenye maono ya kuwa na wanawake wa Kipentekoste wanaotembea katika nguvu ya Roho Mtakatifu na kuubadilisha ulimwengu kwa Injili ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, na hili ni Kongamano la kwanza la Wanawake wa CPCT Taifa kufanyika.