Taasisi za Umma zimetakiwa
kufanya tathmini za awali ya hali ya utekelezaji wa mfumo wa Ufuatiliaji na
Tathmini katika taasisi zao na kuwasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera
Bunge na Uratibu kabla ya tarehe 15 Julai, 2024.
Maagizo hayo yametolewa Jijini
Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera,
Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya Uzinduzi wa nyaraka za
msingi za Ufuatiliaji na Tathmini nchini na utiaji sahihi mikataba ya makubaliano
katika kuimarisha shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini nchini.
Waziri Mhagama amesema
kuzinduliwa kwa mwongozo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika Ufuatiliaji wa
Tathmini na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tathmini hizo katika kufanya
maamuzi na kuboresha utekelezaji na
utendaji katika ngazi zote.
“Katika kutekeleza mwongozo
huu, ninaelekeza Taasisi za Umma kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Tathmini
zote zilizofanyika kwa mwaka wa fedha 2023/24 na zinazotarajiwa kufanyika kwa
mwaka wa fedha 2024/25 ili Ofisi yangu iweze kuandaa Mpango wa Tathmini wa
mwaka 2024/25 na kufuatilia utekelezaji wake," amesema Mhe. Mhagama
Aidha katika kutekeleza
mwongozo huo Mhagama ameelekeza yafuatayo:-Kufanya Tathmini ya Awali ya hali ya
utekelezaji wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika Taasisi zao (M&E
Readiness Assement), Kuandaa Mwongozo wa Matumizi (Operational Manual) ambao
unaeleza utekelezaji wa Ufuatiliaji na Tathmini wa kila siku katika taasisi
zao. Mwongozo huo uoneshe namna ambavyo vitengo, idara au sehemu za U&T
zitakavyofanya kazi kwa kuzingatia Mwongozo huu.
Maelekezo mengine ni pamoja na Kuandaa Mpango wa Ufuatiliaji (Monitoring Plan) kwa kuonesha maeneo na kazi zote zitakazofuatiliwa kila siku kulingana na Mpango Kazi wa Taasisi (Action Plan) na mipango ya utekelezaji wa afua mbalimbali, Kuandaa Mpango wa Tathmini (Evaluation Plan) kwa kuonesha tathmini za afua za maendeleo zitakazofanyika katika kipindi husika.
Sambamaba na hayo ameelekeza
Kuandaliwa kwa moduli za utendaji zinazojumuisha viashiria muhimu vya kupima
utendaji wa Taasisi,Kuteua wataalamu (U&T Champions) kutoka Idara na
Vitengo vyote vya taasisi husika. Wataalamu hao watashirikiana na Idara/Kitengo
cha U&T katika utekelezaji wa Mwongozo huu.
Pia amewasisitiza Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakurugenzi wa Vitengo vya U$T katika Taasisi zote za Umma kuendelea kuimarisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vilivyoanzishwa kwa kutengewa bajeti ya kutosha kutekeleza shughuli zake na kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi waliopo katika vitengo hivyo na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya tathmini za mara kwa mara za utekelezaji wa Sera, Mipango, Miradi na Programu mbalimbali za Serikali na kuwasilisha taarifa hizo Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia umezinduliwa Mwongozo wa
Tathmini ya utayari wa Taasisi za Umma katika kutekeleza shughuli za
Ufuatiliaji na Tathmini umelenga kutathmini uwezo, udhaifu, fursa na changamoto
zinazokabili taasisi za umma katika kutekeleza shughuli za ufuatiliaji na
tathmini na hivyo kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha.
Aidha Mwongozo mwingine ni
Mwongozo Kitaifa wa Tathmini (National Evaluation Guideline) unalenga kutoa
namna bora ya kuratibu na kusimamia tathmini nchini. Kimsingi mwongozo huu
unalenga kuhakikisha mipango ya tathmini inafuatwa, matokeo ya tathmini
yanatumika na utamadumi wa kufanya tathmini unajengwa.
Dkt.Yonazi amesema utekelezaji
wa miongozo hiyo kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo wa Mfumo Jumuishi wa
Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini (Government wide integrated M&E
System)
“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao, ipo
katika mchakato wa maandalizi ya Mfumo huo.
Kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia katika ukusanyaji, uchakataji na
utoaji wa taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini kwa wakati (real time data) na pia
kuwezesha upimaji utendaji kazi utakaochangia katika utoaji wa huduma bora kwa
wananchi,” alieleza Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel ameipongeza Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa uzinduzi huo huku akieleza kuwa hatua hii ni jambo zuri na
kukumbusha kuwapa nafasi wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmnini ili
kuyafikia matarajio ya Tanzania ya sasa na ya baadae.
Naye Bw. Kadari Singo Mkuu wa
Taasisi ya Uongozi amesema upo umuhimu wa kuendelea kusimamia vitengo vya
Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara na Taasisi zetu ili kusaidia kuleta
matokeo yanayokusudiwa na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila
siku.
“Ni vyema kukawa na desturi ya
kufanya tathmini kuanzia mtu mmoja mmoja, nafasi ya familia, jamii na katika
maeneo yetu ya kazi hii iwe ni sehemu ya maisha ya kila mmoja na kusadia kujua
wapi unaenda sawa na wapi urekebishe na kuepuka kuenenda bila malengo,”
alieleza Bw. Singo
Aliongezea kuwa, ili kuendelea
kuwa na matokeo katika utendaji kazi wa kila siku, jamii haina budi kubadili
mtazamo na kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya tathmini na ufuatiliaji kama nyenzo
ya kujipa nafasi ya kufanya vizuri zaidi kuliko ambapo isingefanyika.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.