Friday, September 20, 2024

WAZIRI MKUU AAGIZA KUIMARISHWA UFUATILIAJI NA TATHMINI KULETA MAENDELEO

 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yameelezwa leo Zanzibar na Dkt. Biteko wakati akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika  Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza.

Amesema wataalam wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo na kuwashawishi kwa hoja wakuu wa taasisi husika kupenda kazi zinazotokana na taaluma hiyo badala ya kujisikia wanyonge kitaaluma.

Aidha, Dkt. Biteko amewataka washiriki muda wote kusisitiza misingi ya taaluma hiyo na baadaye kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa na watu wake. “Inawezekana katika maeneo yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukubaliana na hilo ni kujiua wenyewe. Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika.” Amesema Dkt. Biteko.

Aidha, amewataka wataalamu hao kusema ukweli na kusimamia taaluma yao. “ Nataka niwaombe mkajiamini Rais Samia ameahiza na kuelekeza uwepo wa vitengo vya tathmini  ndani ya Serikali, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wafanyekazi na kitengo cha ufuatiliaji kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu mfuatilie fedha zinazopelekwa kwenye miradi na matokeo yake kwenye kubadilisha hali za maisha ya watu.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Kupitia kikao hicho, ametoa maagizo matano yakilenga kuboresha ufuatiliaji, tathmini na kujifunza.

“ Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu ikamilishe mapema Mfumo Ufuatiliaji na Tathmini na kuwezesha taarifa za utendaji wa Serikali kupatikana kwa urahisi.Tume zetu za Mipango zikamilishe uchambuzi wa miradi yote inayotekelezwa ndani ya Serikali na kila mwaka kutoa taarifa ya utekelezaji. Namna hii itawezesha Serikali kuona tija ya miradi inayoidhinishwa na kutekelezwa hapa nchini.” Amesema Dkt. Biteko.

Aidha ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini. Sambamba na TanEA na ZaMEA kuweka mikakati ya kujiimarisha kiuchumi ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa uanzishwaji wake.

Aidha, Dkt. Biteko aziagiza TanEA na ZaMEA kuwa Sera pamoja na mikakati yake ziwe zinafanyiwa Tathimini kila baada ya miaka mitatu baada ya kuandaliwa. Hii itasaidia kujua kila hatua inayofikiwa kwa utelezaji wake pamoja na utatuzi wa changamoto za utelezaji na maboresho wakati wa uhuishaji wa Sera.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi amesema kuwa Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lenye kauli mbiu isemayo  ‘Kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika  ufuatiliaji na tathmini na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya maamuzi’ limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.

Ametaja lengo la Kongamano hilo kuwa ni kuweka  msisitizo kwenye lengo kuu la Serikali la kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi na kuwa katika kutimiza azma hiyo, washiriki wamehamasishwa kutumia vizuri taaluma na mafunzo mbalimbali wanayoyapata kuhakikisha wanakuwa jicho la Serikali katika mipango yake, utendaji wake na utekelezaji wa miradi ili iweze kupata maendeleo.

Aidha Mhe. Lukuvi amesema  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali kwa ujumla wake, utekelezaji wa miradi yote nchini na utoaji wa huduma bora kwa wakati kwa wananchi wote.

Amesema kuwa marais hao wanafanya hayo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambapo kwa sekta zote umewekwa mkazo wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji, utekelezaji wa miradi na utoaji huduma.

“ Katika kuimarisha Sekta ya Fedha, ibara ya 20 (f) ya Ilani ya CCM inaitaka Serikali kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya mashirika na taasisi zilizobinafsishwa ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa ipasavyo na Sekta ya Ujenzi, ibara ya 51(a)(ii) ya Ilani  inaitaka Serikali kuboresha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za barabara kwa kuhakikisha thamani ya ubora wa kazi inaendana na fedha zilizotumika.” Amesema Mhe. Lukuvi.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa kupitia Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa  na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa wataalamu. Sambamba na washiriki kujifunza mbinu mpya za kuboresha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini, hasa kwa kutumia teknolojia na takwimu sahihi ili kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.

“ Kongamano hili limesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha Serikali na wahisani wanatoa huduma zenye tija. Pia, ushirikishwaji wa waananchi utasaidia kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inawafaidisha moja kwa moja.” Amesema Dkt. Yonazi.

Vilevile ameongeza kuwa, kongamano hilo limelenga kukuza uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa sera na miradi ya maendeleo, kwa kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo watendaji wa serikali, wabunge, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi, aidha, limetoa jukwaa la kujadili jinsi ufuatiliaji na tathimini unavyoweza kutumika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na uwajibika.

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Dkt. Ameir Haji Sheha amesema kuwa ushiriki wa Kongamano hili limeibuwa haja na mahitaji mbalimbali na kuwa Kongamano hilo limejumuisha washiriki 738 na ameishukuru Ofisi ya Waziri, Sera, Bunge na Uratibu kwa ushirikiano wakati wote wa maandalizi wa Kongamano hilo.

Wednesday, September 18, 2024

“SERIKALI INATEKELEZA ILANI KWA VITENDO,” WAZIRI LUKUVI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Williamu Lukuvi amesema ujenzi na uimarishaji wa wa miundo mbinu ya Maji Kata ya Mbezi ni kielelezo tosha kinachoonesha kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza Ilani ya Chama kwa vitendo.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Miradi ya Maendeleo ambapo ametembelea na kujionea Mradi wa Maji Mshikamano ulipo Kata ya Mbezi Katika Wilaya ya Ubungo Jijini Dar e salaam na baadae kufanya Mkutano wa hadhara Mburahati.

Shida ya maji Kata ya Mbezi ilikuwa tatizo kubwa hivyo kukamilika kwa Mradi wa Maji niliotembelea   kwa 100% utahudumia watu zaidi ya laki mbili.

“Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan ametegua kitendawili hicho kwa Wananchi wa Ubungo kupata Maji safi na salama ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake hivyo niwape shime Wananchi muendelee kutangaza kazi njema zinazofanywa na Serikali,” alisema Waziri Lukuvi.

Kazi hizi zinazofanywa na Serikali zinapaswa kuonekana na kutangazwa ili Watanzania wengine waone kazi mbalimbali kwa mifano na Falsafa ya Mhe. Rais ya Kazi iendelee  inaendelea kutekelezwa kwenye miradi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) Ubungo amesema kupitia mradi wa Metroplitan Development Project (DMDP) Awamu ya Pili utajenga kingo za Mto Gide na Mto China huko Makurumula,

Aidha kwa kupitia Mradi wa (DMDP) kwa upande wa Ubungo kuna barabara 21 zitakazojengwa ikiwemo barabara nne kubwa katika Kata ya Kimara ambazo ni barabara ya lami Suka, Barabara ya Mlingo, barabara ya Milenia ya tatu, alisema Waziri Kitila.

Naye Mhe. Issa Mtemvu (Mb) Kibamba amesema Wilaya ya Ubungo ilikuwa na wastani mdogo wa upatikanaji wa maji, lakini Mhe. Rais amechukua kilio cha wakazi wa Ubungo na leo miradi imekamilika.

“Serikali haikuwaacha Wananchi wa Goba na viunga vya Salasala katika ujenzi wa tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita zaidi ya milllioni sita eneoTegeta A hivyo tunamshukuru sana Mhe. Rais, Dkt Samia,” alisema Mhe Mtemvu

Wabunge tumepata bahati tunaomba fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo Serikalini na tunazipata, ahadi yetu ni kuendelea kumunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani.

Awali Mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe Hassan Bomboko amesema kwa kipindi cha miaka mitatu ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa na zuri kwa kuleta miradi ya maendeleo ambayo imechagiza mabadiliko makubwa kwa sekta mbalimbali.

Wananchi wa wilaya ya Ubungo wana deni kwa Mhe, Rais kutokana na kazi kubwa ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo iliyofanya na Serikali ya Awamu ya Sita, kwa dhamira ya kweli na ya dhati.

“Hakuna Kata ambayo haijaguswa kabisa kwa upande wa mradi iwe ni upande wa Elimu, Maji, Barabara Afya au Miradi mengine ya Maendeleo” alisema, Mkuu wa wilaya Bomboko.

Tuesday, September 17, 2024

SERIKALI YA SMT NA SMZ ZITAENDELEA NA JUHUDI ZA KUIMARISHA DHANA YA UFUATILIAJI NA TATHMINI KWA PANDE ZOTE MBILI ZA MUUNGANO

 


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zitaendelea na juhudi za kuimarisha dhana ya Ufuatiliaji na Tathmini kwa pande zote mbili za Muungano hasa katika shughuli za Mipango ya Kitaifa na Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Kongamano la Tatu (3) la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi liliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Amesema Tanzania inaendelea kupiga hatua katika uimarishaji wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini ikiwemo kuweka mifumo na miundombinu yenye kuwezesha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa Taasisi za Kitaifa zinazoratibu masuala hayo kwa maslahi mapana ya nchi.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed amesema matumizi ya Teknoloji katika kufanya ufuatiliaji na Tathmini kutaiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kuimarisha uwajibikaji  na kuongeza kasi na uwazi katika kuleta ustawi wa wananchi kwa kutoa huduma sahihi za kijamii na kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa anatambua kuwa mafanikio makubwa yamepatika katika shuhuli za ufuatiliaji na tathmini nchini hivyo amezitaka Mamlaka husika kufanya jitihada za kukamilisha maandalizi ya Sera za Ufuatiliaji kwa Serikali zote mbili pamoja na kutenga rasilimali za kutosha kuwezesha utekelezaji wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini.

Aidha amezitaka  Taasisi  hizo kuhakikisha taarifa zinazozalishwa kutokana na kazi za ufuatiliaji na tathmini zinatumika katika kufanya maamuzi na kuweka mikakati imara ya kuhabarisha Umma juu ya matokeo ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa kushirikiana na waandishi wa habari ili kufikia malengo ya taasisi na Taifa kwa ujumla .

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ametoa wito kwa chama cha Wataalamu Afrika(AFrEA) kuendelea kuvilea vyama vidogo vidogo vilivyomo nchi wanachama pamoja na kuapta fursa za kujifunza na kujiimarisha ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Mhe. William Lukuvi amesema katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kunahitaji uwepo wa taasisi zenye kufanya Ufuatiliaji na Tathmini ili kusaidia kulinda matumizi ya rasilimali fedha zinazotumika katika miradi hiyo.

Mhe. Lukuvi amesema kuwepo kwa Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza vinaakithi dhamira ya Serikali zote mbili ya kuhakikisha mabadiliko na marekebisho makubwa yanafanyika katika kuimarisha Teknolojia na mifumo ambayo itasaidia kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali hizo kwa maslahi mapana ya wananchi wa pande zote mbili za muungano.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji (SMZ) Mhe. Sharif Ali Sharif amesema kufanyika kwa Kongamano la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza hapa Zanzibar litaibua na kupendekeza njia nzuri zaidi za kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini hasa katika masuala ya Utalii na Uwekezaji nchini.

Mhe. Sharif amesema kufanyika kwa Ufuatiliaji na Tathmini kunasaidia katika kupima shuhuli za mipango ya maendeleo ya Kimataifa, kitaifa na Kikanda kwa kutathmini ufanisi na uwajibikaji wa Taasisi husika hasa katika kupata taarifa na Takwimu sahihi zenye  matokeo chanya ya mipango hiyo.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akieleza kuhusu kongamano hilo amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu makongamano hayo ikiwa hilo ni la Tatu kufanyika na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 650 na kusema ni ongezeko kubwa linaloonesha muamko kwa washiriki kwa kulinganisha awamu zilizopita ambapo Awamu ya kwanza walijitokeza washiriki 302, awamu ya pili washiriki 624.

“Lengo ni kuendeleza jitihada za Serikali za kujenga uelewa na utamaduni wa ufuatiliaji na tathmini kwa watendaji wa Serikali, Wadau na Jamii kwa ujumla. Hivyo, Kongamano hili linawakutanisha wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, na wadau wa Serikali na sekta binafsi wakiwemo watunga sera, watekelezaji sera na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Aliongezea kuwa Kongamano hilo linatoa fursa ya kukumbushana juu ya umuhimu na faida za ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali.

“Ni matarajio yetu kongamano litaleta matokeo mengi ikiwemo kuongeza ubunifu katika utendaji wetu, matumizi ya TEHAMA pamoja na kuongeza weledi katika dhana hii ya ufuatiliaji na tathmin,”alisema Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Mwakilishi wa USAID Tanzania Bw. Craig Hart ameeleza kuwa uwepo wa kongamano hilo unatarajiwa kuleta matokezo zaidi katika shughuli za kila siku kwa kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya kisasa.

“Hakika wiki hii ni matarajio yetu ilete matokeo yanayotarajiwa hivyo litumike kwa usahihi hasa kujifunza na kuona namna ya kujitathim namna tunavyofanya kazi na ujuzi huu utumike kwa kuimarisha utendaji kazi, tunaahidi kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada wakati wa Kongamano hilo amesema kuwa,tathimin na ufuatiliaji ni jambo la msingi hivyo linapaswa kuendelea kupewa kipaumbele kwa lengo la kusaidia namna ya kuendelea kuzitumia malighafi tulizonazo, hivyo ni eneo muhimu sana katika shughuli zetu za kila siku.

“Ufuatiliaji na tathmini ndiyo njia pekee inayotusaidia kujua nini kiboreshwe na wapi penye kuhitaji mkazo kwa kuzingatia umuhimu wake, hivyo hii ndiyo engeene muhimu yenye kutupa uwezo wa kujitathmin,” alisema Profesa Elisante

 

Thursday, September 12, 2024

DKT. YONAZI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UJUMBE KUTOKA IFAD


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo - IFAD wanaosimamia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Uvuvi (AFDP) katika ukumbi wa Ofisi hiyo leo 12 Septemba, 2024 Jijini Dodoma.

Tuesday, September 10, 2024

MAONESHO YA MIFUKO YA UWEZESHAJI FURSA KWA WANANCHI SINGIDA

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi amefungua rasmi Maonesho ya Saba ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mkoani Singida ambayo yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)

 

Wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Mheshimiwa Lukuvi amesema kuwa maonesho hayo yatafungua fursa za Kiuchimi kwa wafanyabiashara, wakulima na wafanyabiashara wa Singida na Mikoa ya Jirani.

Waziri Lukuvi Aliongeza kuwa, Maonesho hayo yatawezesha wananchi kupata huduma za uwezeshaji ikiwemo mitaji, mikopo nafuu, dhamana za mikopo, vifaa, mashine au mitambo, urasimishaji ardhi,urasimishaji biashara, huduma za msimbomilia, ujuzi, ithibati ya bidhaa, huduma za sheria, huduma za ushirika, huduma za ushauri wa kitalaam, elimu rasmi na elimu ya ufundi stadi, kuunganisha wananchi na fursa,na ukaguzi wa bidhaa.

Mhe. Lukuvi alibainisha kuwa, Maonesho hayo ni muhimu kwa kuwa yanakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji wakiwemo, Wizara, Mikoa, Halmashauri; Taasisi zinazosimamia Mifuko na Programu za Uwezeshaji, Taasisi za Fedha, Wafanyabiashara, Kampuni, Taasisi za Elimu na Tafiti, Wakulima, Wafugaji,na Wajasiriamali.

Aliongeza kuwa, Maonesho hayo yana lengo la kuhakikisha kuwa washiriki wanabadilishana ujuzi, maarifa, uzoefu na teknolojia mbalimbali ambazo zinatumika katika kukuza ushiriki wa wananchi katika shughulli za kiuchumi.

“Nina imani kuwa, Maonesho haya yatatoa fursa nyingi kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na Mikoa mingine.” Alisisitiza

Akiongea kwa Niaba  ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge naa Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Bw. Condradi Milinga amesema kuwa pamoja na  maonesho hayo kutoa fursa mbalimbali kwa wajasailiamali, wananchi pia watapata mafunzo na ujuzi kuhusu masuala mbalimbali kutoka kwa Washiriki wa Maonesho na kutoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho hayo.

Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (NEEC), Bi Beng’ Issa amesema kuwa kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa lengo la kujenga uchumi na kuwaondoa wananchi katika umaskini.

“Juhudi hizo ni pamoja na kuanzisha mifuko na program za uwezeshaji mbalimbali kwa lengo la kutoa mikopo au dhamana ya mikopo kwa wananchi kwa masharti nafuu, kutoa ruzuku pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi ili waweze kukopesheka au kuhudumiwa na wadau wengine.” Alibainisha

Aliendelea kufafanua kuwa, mpaka sasa Baraza linaratibu Jumla ya Mifuko ya Uwezeshaji na Programu 72 ambayo 62 ipo Serikalini na 10 ipo Sekta binafsi, hivyo Lengo kuu la Maonesho haya ni kutoa uelewa wa fursa za Mifuko kwa Wananchi ambapo ilionekana mifuko mingi haifahamiki kwa wananchi hivyo kuchelewesha kufikisha huduma za uwezeshaji kwa wananchi.

Maonesho hayo ya siku Saba yaliyofunguliwa leo Mkoani Singida yana Kaulimbiu inayosema Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Unufaike na Fursa za Uwezeshaji

 


Monday, September 2, 2024

INEC, VYAMA VYA SIASA KUANDAA KANUNI ZA MAADILI YA UCHAGUZI

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushauriana na vyama vyote vya siasa itaandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

Mhe. Nderiananga ameyasema hayo leo katika Mkutano wa 16 Kikao cha Tano, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Neema Lugangira ambapo alitaka kufahamu ni lini kanuni za maadili ya uchaguzi zitakuwa tayari baada ya makosa ya ukatili wa Kijinsia kuongezwa kwenye Sheria za Uchaguzi mwezi Februari, 2024.

 “Kwa mujibu wa Kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 kinaeleza kuwa, Tume baada ya kushauriana na vyama vyote vya Siasa itaandaa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi; aidha, kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 1.2 ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi za mwaka 2020, maadili ya Uchaguzi yatatumika katika Uchaguzi Mkuu na katika chaguzi ndogo,” alifafanua Mhe. Nderiananga.

 Aidha, Naibu Waziri huyo alieleza kwamba, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushauriana na vyama vyote vya siasa itaandaa Kanuni hizo kwa kuwa maadili mpya ya uchaguzi huandaliwa katika kila mwaka wa uchaguzi Mkuu.