Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu) Mhe. William Lukuvi ameishukuru Umoja wa Afrika
kwa kutoa kibali cha kuichangia nchi ya Tanzania Dola za Kimarekani 200,000
kama ishara ya mshikamano kutokana na maafa makubwa yaliyotokea Wilaya ya
Hanang’ mkoani Manyara.
Waziri Lukuvi ametoa shukrani
hizo leo katika Ofisi za Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu zilizopo Jijini
Dodoma na kubainisha kuwa mchango huo ni muhimu kwa kuwa utasaidia juhudi
zinazofanywa na Serikali za kurejesha hali ikiwemo ujenzi wa shule, kituo cha
afya na soko katika eneo lililoathirika.
Akipokea mchango wa fedha hizo kutoka kwa
Mheshimiwa Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa
Botswana nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent
Representative Sub Committee on refugees, Returnees and IDPs), Mhe. Lukuvi
amemweleza kuwa, mwaka 2023/2024 Tanzania ilikumbwa na El-Niño ambayo
ilisababisha kuwepo kwa mvua kubwa zilizofululiza kwa kipindi kirefu na kusababisha
mafuriko, upepo mkali, maporomoko ya tope na udongo.
Ameeleza, pamoja na juhudi
zilizofanywa na Serikali katika kuzuia na kupunguza madhara, bado El-Niño
ilileta madhara makubwa ikiwemo maafa ambayo yaliyosababisha vifo, kuharibu
makazi ya watu na miundombinu muhimu.
“Maporomoko ya tope wilayani Hanang’
yaliathiri maisha ya watu, miundombinu, shughuli za kiuchumi na kijamii,
takwimu zinaonesha kuwa watu wapatao 89 walipoteza maisha na watu wapatao 139
waliumia kutokana na maporomoko hayo. Aidha, tathmini iliyofanyika inaonesha
jumla ya nyumba 261 ziliathirika kwa namna moja au nyingine ambapo nyumba 95
zilibomoka kabisa na zingine kuzungukwa na tope, Watu wapatao 1576 kutoka 526
waliachwa bila makazi katika kipindi cha tukio” ameeleza Mhe. Lukuvi.
Aidha, ameongeza kuwa, katika kukabiliana na
maafa, Serikali ilifanya juhudi za kurudisha hali ambapo mpaka sasa imewezesha
kujengwa nyumba 108 za makazi ya watu, kati ya nyumba hizo 73 zimejengwa kwa
fedha za Serikali na nyumba 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu,
ujenzi wa nyumba hizo 108 umekamilika.
“Ninaelewa kuwa ujumbe wako utatembelea Wilaya
ya Hanang’ tarehe 14 Novemba, 2024, katika safari yenu mtashuhudia juhudi kubwa
za Serikali kwa kushirikiana na wadau zinazoendelea za kurejesha hali ikiwemo
miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme, maji na ujenzi wa nyumba 108 za
makazi, ameeleza Mhe. Lukuvi.
Kwa upande wake Mheshimiwa
Balozi Tabelelo Alfred Boang, Balozi wa Jamhuri wa Muungano wa Botswana nchini
Ethiopia na Mwakilishi wa kamati ya Mabalozi (Permanent Representative Sub
Committee on refugees, Returnees and IDPs), ameeleza kuwa, ujumbe huo umeagizwa
na Kamati ya Mabalozi kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea katika maeneo
yaliyoathiriwa ikiwa dhamira kubwa ni Mkoa wa Manyara, aidha muhimu zaidi ni
kusikia kutoka kwenye mamlaka na ndio maana wamekutana na Mheshimiwa Waziri na
timu yake.
“Muhimu zaidi kama Umoja wa Afrika kwa hakika
kila kidogo tulicho nacho huwa tunainuka tunajivunia kuwa tumejitolea na kusema
tunaenda kutafuta suluhu ya Afrika, matatizo au changamoto za Afrika”
amebainisha Balozi Tabelelo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.