Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt.
James Kilabuko amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Halmashauri ya
Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa huku akisisistiza nyaraka hizo kutekelezwa kwa
vitendo.
Dkt.
Kilabuko amesema hayo wakati wa uzinduzi huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni
mwanzo wa kuanza kazi rasmi endapo kutatokea janga lolote, na kutoa wito kwa
idara, vitengo na taasisi ngazi ya wilaya kuzingatia nyaraka hizo kwa
kuhakikisha zinakuwa chachu ya kuongeza ushirikishwaji wa jamii na wadau katika
masuala ya menejimenti ya maafa.
Ameongeza
kuwa, hatua hiyo itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu masuala ya usimamizi
wa maafa, kuimarisha mfumo wa utoaji wa tahadhari awali, kujenga uwezo wa
kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa na kurejesha hali pindi maafa
yanapotokea.
Dkt.
Kilabuko alifafanua kuwa, nyaraka hizo zimekuja wakati sahihi kwa
kuzingatia kuwa, Wilaya imekuwa ikikabiliwa na maafa yanayosababishwa na
majanga hasa ya upepo mkali, magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama,
mafuriko pamoja na mgongano wa wanyamapori na binadamu ambayo yamekuwa
yakijirudia mara kwa mara.
“Nimeelezwa
kuwa matokeo ya tathmini ya maafa iliyofanyika katika Halmashauri ya Nkasi
mwezi Januari, 2026 yalionesha kuwa yapo majanga mengine ambayo yamekuwa
yakijitokeza japo hayajaleta athari kubwa ikiwemo wadudu waharibifu wa mazao,
ajali za barabarani, moto, ajali za majini, tetemeko la ardhi, radi pamoja na
maporomoko ya ardhi.Natambua kuwa Wilaya imekuwa ikikabiliwa na mlipuko wa
ugonjwa wa kipindupindu,nitumie fursa hii kuwapongeza kwa jitihada mnazoendelea
nazo katika kukabiliana na ugonjwa huo,”Alisema Dkt. Kilabuko
Kwa
hatua nyingine, Ameshukuru Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa
(UNICEF) kwa ufadhili ambao umewezesha kuchangia jitihada za Serikali katika
kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa pamoja na Mkakati wa
Kupunguza Vihatarishi vya Maafa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Naye
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Uratibu na Wenye Ulemavu Brigedia Generali Hosea Ndagala amesema Idara hiyo
imekuwa ikichukua hatua za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa na
kurejesha hali pindi maafa yanapotokea kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
zilizopo.
Aliongezea
kuwa,Serikali kwa kutambua hilo na katika kuhakikisha nchi inakuwa stahimilivu
dhidi ya maafa, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali. Jitihada hizo ni pamoja
na kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya maafa kwa kutunga Sera ya
Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004, Toleo la Mwaka 2025 na Sheria ya
Usimamizi wa Maafa Sura ya 242 ambayo imeweka mfumo mzuri wa usimamizi wa maafa
kutoka ngazi ya Taifa hadi Kijiji/Mtaa.
“Ni
muhimu kwa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti juu ya utekelezaji
wa Mpango huu uliozinduliwa leo na kuendelea kutoa elimu kuhusu namna bora ya
wananchi kuendelea kuchua hatua za awali kwa kuzingatia maafa ni suala mtambuka
na linaanza na mtu mmoja,” alisisitiza
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mheshimiwa Peter Lijualikali ameishukuru
Ofisi ya Waziri Mkuu na UNICEF kwa kazi nzuri ya uandaaji wa nyaraka za
usimamizi wa maafa na kutoa elimu juu ya masuala ya menejimenti ya maafa kwa
Wilaya ya Nkasi na kuahidi kuzifanyia kazi nyaraka hizo.
“Wilaya
imepata kitu chema kitakachotufaa, nasi tunaahidi kuzitumia kama miongozo
sahihi ya kuleta matokeo kwa kuzingatia Serikali imeweka fedha katika
kuhakikisha mipango inaleta matokeo yaliyokusudiwa, hivyo tusiwe nyuma,
tufanyie kazi kwa tija ya Halmashauri nzima,” alisema Lijualikali
Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi Mheshimiwa Richard Leonard Masai
akitoa Salam ameshukuru uratibu mzuri wa uandaaji wa nyaraka hizo na kutoa
rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhali za awali na kuzingatia taarifa za
tahadhali zinazotolewa na wataalamu ili kuendeala kuwa na jamii iliyo salama na
yenye kujiletea maendeleo yake.

No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.