Mkuu
wa Wilaya ya Nkasi, Mheshimiwa Peter Lijualikali amepongeza Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu kwa namna ilivyoratibu zoezi la
uandaaji wa Rasimu za Nyaraka za Usimamizi wa Maafa kwa Wilaya yake huku
akiwasihi wajumbe wa kamati kuzitumia kama ilivyokusudiwa mara baada ya
uzinduzi utakaofanyika hivi karibuni.
Ameyasema
hayo leo wakati wa kikao cha Kamati Elekezi ya Wilaya ya Usimamizi wa Maafa
ikihudhuriwa na timu ya wajumbe hao wakiongozwa na mkuu wa Wilaya huyo ambaye
ndiye Mwenyekiti wa Kamati.
“Kipekee
nawapongea Ofisi ya Waziri Mkuu na UNICEF kwa kuona umuhimu wa kuja katika
Wilaya yetu ya Nkasi, na tutahakikisha kile mlichokifanya hapa Nkasi kinaleta
matokeo chanya hasa kwa elimu tuliyoipata ya masuala ya usimamizi wa maafa
hususani katika kuzuia na kujiandaa ili kusiwe na athari kubwa endapo majanga
yatatokea,” alieleza Mhe. Lijualikali.
Naye
Mratibu wa Maafa Mkoa wa Rukwa Bi. Aziza Kalyatila amesema ipo haja ya
kuendelea kupewa elimu zaidi ya masuala ya usimamizi wa maafa kwani itasaidia
katika kuwajengea uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili, na kurejesha hali pindi
maafa yanapotokea.
Kikao
hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye
Ulemavu kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto
(UNICEF) pamoja na timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya
Nkasi kikilenga kuwapitisha katika nyaraka zilizoandaliwa kwa ajili ya matumizi
ya Halmashauri ambazo ni Tathmini ya Vihatarishi vya Majanga, Uwezekano wa
Kuathirika na Uwezo wa Kukabiliana na Majanga, rasimu ya Mpango wa Kujiandaa na
Kukabiliana na Maafa pamoja na rasimu ya Mkakati wa kupunguza vihatarishi vya
maafa.

No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.