Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,
Uratibu na Wenye Ulemavu, kupitia Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji
wa Serikali, imesaini Hati za Mashirikiano (MoU) na Vyuo Vikuu vinne ambavyo ni
Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha
na Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na
tathmini unaotumia ushahidi katika kupanga na kutekeleza sera, mipango,
programu na miradi ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo
iliyofanyika leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu (SBUU) Dkt. Jim Yonazi amesema kupitia mashirikiano hayo, Serikali na Vyuo
Vikuu vitashirikiana katika kuimarisha uwezo wa wataalamu wa ufuatiliaji na
tathmini, kufanya tathmini za pamoja za miradi ya maendeleo, kuendeleza tafiti
bunifu na kuhakikisha maarifa yanayozalishwa vyuoni yanatumika kuboresha
utendaji wa Serikali.
"Mafanikio ya MoU hizo yatapimwa
kwa utekelezaji wake, kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye msisitizo wa matokeo
yanayopimika na manufaa halisi kwa wananchi" ameongeza Dkt. Yonazi.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Makamu
Wakuu wa Vyuo Vikuu vilivyoshiriki katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amesema kuwa, Ufuatiliaji na Tathmini ni eneo
muhimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa na Vyuo Vikuu vinaahidi kushirikiana na
serikali katika kuhakikisha tunafanya vizuri katika eneo hilo ili nchi
zinazotuzunguka wajifunze kutoka Tanzania.
Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya
Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali Bi. Sakina Mwinyimkuu amesema
kuwa ushirikiano huo wenye nia ya pamoja una malengo ya kuongeza nguvu ya
kusaidia taifa na kujenga tamaduni ya uwajibikaji.

No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.