Tuesday, February 19, 2019

MAJALIWA AKAGUA MRADI WA MAJI WA MUHANGE WILAYANI KAKONKO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili kwenye eneo la Mradi wa Maji wa  Muhange wilayani Kakonko kukagua mradi huo, Februari 19, 2019. Kulia ni mkewe Mary na kushoto ni Mbunge wa Buyungu, Mhandishi Christopher Chiza.
Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akiwasalimia wananchi wa kijiji cha  Muhange wilayani Kakonko wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokagua Mradi wa Maji kijijini hapo, Februari 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim  Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kakagua Mradi wa Maji wa Muhange wilayani Kakonko, Februari 19, 2019.  Wengine kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, Mbunge wa Buyungu Mhandisi Christopher Chiza, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na kulia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Diwani wa Kata ya Muhange wilayani Kakonko, Ibrahim Katunzi jumla ya shilingi milioni moja kwa ajili ya Mradi wa Maji na Zahanati katika Kata hiyo, Februari  19, 2019.

Read More

SERIKALI YAKERWA NA MAUAJI, UNYANG’ANYI MIPAKANI

*Yaviagiza vyombo vya ulinzi viongeze ulinzi na doria 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na ongezeko la vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitisho kwa wananchi.

Pia, Waziri Mkuu ameagiza wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kwenye makambi wanayohifadhiwa na kuingia uraiani wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kwani wanachokifanya ni ukiukwaji wa sheria.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Februari 19, 2019) alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kigoma.

Alisema maeneo yaliyo katika hali mbaya ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini, ambako wananchi hususani wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na vitendo hivyo.

Waziri Mkuu alisema pamoja na undugu waliokuwanao na nchi jirani, lakini kila nchi ina sheria na taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe na ni marufuku kuingia katika nchi yoyote bila ya kufuata sheria na taratibu za nchi husika.

“Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki. Kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali.”

Alisema watu wote wanaoingia bila ya kufuata sheria na taratibu ndio hao wanashiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za kivita pamoja na utekaji wa watoto.

Waziri Mkuu alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kulinda mipaka yetu na watu wote watakaobainika wameingia nchini bila vibali wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aliongeza kuwa wakimbizi wanaohifadhiwa katika maeneo mbalimbali nchini hawaruhusiwi kutoka nje ya kambi hizo kwa sababu huduma zote wanazostahili zikiwemo za afya, elimu  na chakula zinapatikana kambini.

Pia, Waziri Mkuu aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iwasimamie vizuri watumishi wake wanaofanya kazi kwenye kambi hizo na kuchukua hatua kwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Mbali na agizo hilo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pia Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa wizara hiyo ufanye mazungumzo na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) ili litekeleze majukumu yake bila kukiuka sheria za nchi.

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi kuacha tabia ya kuwachukua raia wa nchi jirani na kuwaleta nchini kwa ajili ya kuja kufanya kazi za vibarua katika mashamba yao bila ya kuwa na vibali.

“Tabia ya kuwachukua watu kutoka nchi jirani kwa ajili ya kulima mashamba bila ya kuwaandikisha ni makosa kisheria. Anayetaka kupata vibarua kutoka huko aende kuomba vibali huku akieleza idadi ya anaowataka na siku watakazokaa.”

Waziri Mkuu alisema lengo la kufanya hivyo ni kulinda usalama kwa sababu wengine wanawafanyisha kazi na wakimaliza hawawalipi wanawatishia kuwashitaki kwa kuingia nchi bila ya kibali jambo linalochangia kuwepo kwa migogoro na visasi.

Pia, Waziri Mkuu alisema hata kama wakiwalipa hakuna anayefuatilia kama kweli baada ya kumaliza vibarua hivyo wanarudi makwao kwani wengi wao wanaendelea kubaki nchini huku baadhi wakijihusisha na vitendo vya kihalifu.

(mwisho)

Read More

MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA OFISI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA KAKONKO

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua ujenzi wa Ofisi  ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Februari 19, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akifurahia baada ya kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Februari 19, 2019. Kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako na wapili kushoto ni Mbunge wa Buyungu, Christopher Chiza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua ujenzi wa Ofisi  ya Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo, Februari 19, 2019.  Wapili kulia ni mkewe Mary.

Read More

WAZIRI MKUU AMSIMAMISHA KAZI MWEKA HAZINA KIBONDO

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Thomas Chogolo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma  zinazomkabili za ubadhilifu wa makusanyo ya mapato ya halmashauri hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa halmashauri huyo kumaliza haraka migogoro yao ya kiutendaji kabla ya Serikali haijawachukulia hatua kwani wanachokifanya ni kinyume na maelekezo yake.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma.

“Katika Serikali hii suala la ukusanyaji wa mapato ni jambo nyeti na limepewa kipaumbele, hivyo ni lazima fedha inayokusanywa itumike kama ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi.”

Waziri Mkuu amesema wananchi wa halmashauri hiyo wanalipa kodi kupitia kwa watendaji wa kata katika maeneo yao lakini  Mweka Hazina haingizi kwenye mfumo wa Serikali. “Jambo hili halivumiliki.”

Amesema mbali na fedha za makusanyo ya kodi pia matumizi ya fedha mbalimbali zinazopelekwa na Serikali katika halmashauri hiyo nayo hayaridhizishi. Ametoa mfano wa fedha za sekta ya Afya ambapo zaidi ya bilioni mbili zimepelekwa na dawa hakuna.

Waziri Mkuu amesema uaminifu na uadilifu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na watumishi wa umma, hivyo amewataka watumishi hao wasijiingize kwenye mambo ambayo hayana tija katika utumishi wao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imewapa dhamana watumishi hao kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kutanguliza maslahi yao binafsi, amewataka wajirekebishe kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Serikali haitawapa nafasi ya kuendeleza migogoro yenu kila mmoja lazima atambue majukumu yake na kuyatekeleza. Serikali haiitaji mtumishi mvivu, masiyekuwa muadilifu na wala anayejihusisha na vitendo vya rushwa.”

Amesema ni lazima wakamaliza migogoro ya kiutendaji ambayo imesababisha watendaji wa halmashauri kutoelewana na kugawanyika katika makundi na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

 (mwisho)
Read More

Monday, February 18, 2019

VIJANA ANZISHENI MASHAMBA YA MICHIKICHI-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka vijana mkoani Kigoma waanzishe mashamba ya michikichi kwa kuwa zao hilo litawapatia kipato cha uhakika.

Amesema Serikari imedhamiria kufufua zao la michikichi ili kuliwezesha Taifa kujitosheleza kwenye mafuta ya kula na kuokoa fedha za kigeni.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Februari 18, 2019) alipowasalimia wananchi wa kijiji cha Nyakitondo wilayani Kasulu akiwa njiani kwenda Kibondo.

Waziri Mkuu ambaye yupo mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufufua kilimo cha michikichi amesema ni vema wananchi wakachangamkia fursa hiyo.

“Vijana limeni michikichi kwani ukipanda ukiwa darasa la tano baada ya miaka mitatu utaanza kuvuna na kujipatia kipato ambacho kitakuwezesha kujikimu.”

Amesema kilimo cha zao la michikichi kitawawezesha wananchi hususani vijana kupata mitaji ya uhakika kwa ajili ya shughuli zingine za kiuchumi

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inaongoza kwa kilimo cha zao la michikichi katika nchi za Afrika Mashariki.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi hao wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa matibabu kwa yao na familia zao.

Wakati huohuo Waziri Mkuu ametembelea kambi ya Wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo na kukagua shule ya msingi Kassim Majaliwa na baadae wodi ya wazazi katika Hospitali Nduta.

 (mwisho)
Read More

Sunday, February 17, 2019

MAJALIWA ATEMBELEA KAMBI YA JKT YA BULOMBORA MKOANI KIGOMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja  Jenerali , Martin Busungu wakati alipowasili kwenye Kambi ya JKT ya Bulombora wilayani Uvinza, kuhamasisha ufufuaji wa zao la michikichi, Februari 17, 2019. Wapili kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary (kushoto) wakitazama sabuni zinazotengenezwa na Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi ya Bulombora wilayani Uvinza wakati alipotembelea  kambi hiyo kuhamasisha ufufuaji wa zao la michikichi, Februari 17, 2019.
Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akiwasha trekta ikiwa ni ishara ya kuzindua trekta hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora wilayani Uvinza, Februri 17, 2019. Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Kigoma kwa ziara yenye lengo la kuhamasisha ufufuaji wa zao la michikichi.
Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akipanda mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua upanuzi wa shamba la zao hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora  wilayani Uvinza, Februari 17, 2019. Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Kigoma kwa ziara yenye lengo la kuhamasisha  ufufuaji wa zao la michikichi.
Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akipanda mchikichi ikiwa ni ishara ya kuzindua upanuzi wa shamba la zao hilo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Bulombora  wilayani Uvinza, Februari 17, 2019. Mheshimiwa Majaliwa yuko mkoani Kigoma kwa ziara yenye lengo la kuhamasisha  ufufuaji wa zao la michikichi.

Read More

HATUTAMVUMILIA ATAKAYEHUJUMU MKAKATI WA KUFUFUA ZAO LA MICHIKICHI -MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitomvumia mtu yeyote 
atakayebainika kuhujumu mkakati wake wa kulifufua zao la michikichi nchini.

Amesema wanataka kuona wakulima zao hilo wakinufaika kama wengine wa mazao makuu ya biashara, hivyo haitomfumbia macho mtu atakayezembea.

Aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Februari 17) mara baada ya kukagua shamba la michikichi la kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bulombora.

Alisema Serikali inataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama ilivyokuwa kwa wakulima wa korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku.

Alisema Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula kwani inatumia fedha nyingi kuagiza nje ya nchi.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi mkoani Kigoma kwamba suala la kilimo cha michikichi liwe ajenda ya kudumu kwenye vikao vyao.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe shamba darasa la zao la michikichi ili wananchi waweze kujifunza mbinu bora za kulima zao hilo.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha zao la michikicho.

Waziri huyo alisema kiasi hicho cha fedha kimetengwa katika bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha michikichi nchini.

Alisema iwapo kilimo cha zao hilo kitaboreshwa kitasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

Pia, Waziri Mgumba alisema tayari wizara hiyo imeshaongeza watafiti zaidi ya 10 wa zao la michikichi katika kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga. 

Waziri Mgumba alipongeza Jeshi la Magereza  na JKT kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wizara katika kipindi hiki cha ufufuaji wa zao la michikichi.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa maelekezo yote aliyoyatoa kuhusu kilimo cha michikichi watayatekeleza.
Read More

GEREZA LA KWITANGA LIPATIWE KIWANDA CHA KISASA-MAJALIWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe gereza la Kwitanga mkoani Kigoma linapata kiwanda bora na cha kisasa cha kukamulia mafuta ya mawese kitakachoonesha dhamira ya Serikali ya kufufua zao la michikichi nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza katika kuboresha shamba lake la michikichi pamoja na mabadiliko waliyoyafanya kwenye kiwanda chao cha kuzalisha mafuta.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 17) wakati alipotembelea Gereza la Kwitanga kwa ajili ya kukagua shamba la michikichi na kuzindua trekta na kufungua sero moja iliyojengwa gerezani hapo.

Amesema amefurahishwa baada ya kukuta mashine mpya ya kukamulia mafuta ya mawese inafungwa kwenye kiwanda cha gereza hilo ambayo itakuwa inatumia mota tofauti za zamani wapolikuwa wanatumia mashine ya kusukumwa na mikono.

Kadhalika Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) waimarishe teknolojia ya kukamua mafuta kwenye kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha kwa tija.

Katika kuhakikisha gereza hilo linakuwa la mfano kwenye kilimo cha zao la michikichi, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inunue gari lenye winchi litakalorahisisha uvunaji wa chikichi.

Waziri Mkuu amesema njia inayotumiwa kwa sasa ya kupanda juu ya mchikichi wakati wa mavuno si salama kwa mvunaji, hivyo ni vema wakatumia magari hayo yenye winchi kwa ajili ya kurahisisha shughuli ya uvunaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Leonard Burushi amesema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mafuta kutoka pipa 63.4 kwa mwaka 2016/2017 na kufikia pipa 97 kwa mwaka 2018/2019 na zoezi la uvunaji bado linaendelea.

Amesema mafanikio hayo yametokana na maagizo yalitolewa na Waziri Mkuu alipotembelea gereza hilo Julai, 2018, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza waboreshe eneo la kukamulia mafuta ili waongeze uzalishaji.

Kiongozi huyo wa Magereza mkoa wa Kigoma amesema eneo la ekari 20 limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kukamua mafuta ya mawese, maghala ya kutunzia mafuta machafu na upanuzi wa kiwanda baadae.

Amesema maelekezo mengine yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na Magereza ya Kwitanga na Ilagala yaongeze eneo la mashamba yake kwa ajili ya kupanda michikichi mipya ambalo limetekelezwa. 

Amesema tayari gereza la Ilagala limeandaa jumla ya ekari 150 zenye uwezo wa kupandwa michikichi aina ya tanera 8,550 na Kwitanga ekari 400 ambazo zitapandwa miche 22,800 ya michikichi aina ya tanera.

(mwisho)
Read More