*Ni ya uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya
uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel
Manyele ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu, Machi
27, 2017) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar
es Salaam.
Akisoma taarifa hiyo mbele
ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya
uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali
vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama
mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.
Prof.
Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika
hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo
Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu
kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali. Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa
karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu
zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na
taasisi zake,” amesema.
Prof.
Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha
Faru John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa
Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama
pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi
kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi
binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya
uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na kwamba mawasiliano
yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka
kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA
kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia
kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za
wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele
amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi
vizuri na kwamba tume inashauri TAWIRI
na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.
Amesema
kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za
vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa mengine. “TUME inashauri
maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi
wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake
iweze kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa
kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini
ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu
uliokuwemo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.
“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa
kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili
kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”
Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana
na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo
yaliyoainishwa na tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili
za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha
faru huyo. Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani
mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru
John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Alitoa agizo
hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro,
mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza
la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.