Wednesday, February 27, 2019

UAMUZI WA SERIKALI WA KUWABANA WATUMISHI WA UMMA WAZAA MATUNDA


*Wananchi waipongeza kwa kuwa umeimarisha utoaji wa huduma za afya
WANANCHI wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwabana watumishi wa umma, kwa sababu uamuzi huo umezaa matunda na sasa hali ya utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya hospitali yameimarika.

Kauli hiyo imetolewa leo (Jumatano, Februari 27, 2019) na wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hospitali hapo.

“Huduma zimeimarishwa dawa tunapata, hakuna lugha chafu wala kuombwa rushwa. Tunahudumiwa vizuri na kuna wakati hadi tunabembelezwa kunywa dawa mambo ambayo hapo nyuma hayakuwepo, hivyo tunaishikuru Serikali.”

Mmoja wa wagonjwa hao ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi hospitalini hapo baada ya kujifungua, Mwajuma Mohammed amesema baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani na kuwabana watumishi wa umma sasa kuna mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji.

Amesema zamani baadhi ya wauguzi hususani wanaofanyakazi kwenye wodi ya wazazi hawakuwa na lugha nzuri walikuwa wakiwatukana na kuwakashifu jambo ambalo kwa sasa halipo, kwani wakifika wapokelewa vizuri.

Mama mwingine aliyelazwa kwenye wodi hiyo, Crista Moyo amemuomba Waziri Mkuu kuisadia hospitali hiyo kwa kuiongezea watumishi kwa kuwa walipo ni wachache ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kila siku.

Crista ameishauri Serikali ikiwezekana iajiri hata watu wasiokuwa na taaluma ya udaktari au uuguzi ili wakafanyekazi ambazo hazihitaji ujuzi kama za  kuwasaidia wagojwa kutoka eneo moja kwenda lingine.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amezishauri Halmashauri jijini Dar es Salaam zihakikishe zinaendelea kuimarisha vituo vya afya na kuongeza vingine ili utoaji kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.

Pia ameshauri ianzishwe miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika hospitali hizo kwa lengo ya kuwezesha utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za dharura kwa wakati. 

“Rais Dkt. Magufuli anataka wananchi wapate huduma za afya karibu na  makazi yao ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo. Ndio maana tunajenga vituo vya afya vilivyokamilika vinavyotoa huduma zote muhimu kama maabara, upasuaji na mama na mtoto.”

Waziri Mkuu amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua utoaji wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hizo na kubaini kama kuna changamoto ili Serikali iweze kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi.

“Tumesikia changamoto zinazowakabili madaktari, tumezichukua na tutazifanyia kazi ikiwepo ya upungufu wa watumishi mbalimbali kama madaktari na wauguzi ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.”

Waziri Mkuu amesema dhamira ya dhati ya Serikali kwao ni ya kuwatumikia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo waendelee kuwa wazalendo na washirikiane na Serikali yao. Wafanye kazi kwa bidii.

Naye,Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Amaani Malima amesema hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wa nje 1,800 hadi 2,000 kwa siku na wagonjwa wa ndani 250 hadi 300. Wagonjwa hao watoka wilaya mbalimbali.

Dkt. Malima amesema hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 439 kati yao madaktari bingwa ni 16, madaktari 76 na wauguzi 209 na watumishi wengine 138. “Idadi hii ni ndogo kulingana na mahitaji ya hospitali kwani tuna upungufu wa watumishi 278 sawa na asilimia 39.”

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa  dawa muhimu kwenye hospitali hiyo, Dkt. Malima amesema kwa kipindi cha Januari upatikanaji ulikuwa wa kuridhisha kwa asilimia 85 ya kiasi cha dawa na vifaa tiba vilivyohitajika.

Awali, Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala ambapo alikagua mradi wa ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa mashuhuri ambalo lilianza tangu mwaka 2014 na bado halijakamilika.

Hivyo, ameishauri Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuangalia namna ya kuweza kusaidia ujenzi wa jengo hilo ili mradi huo uweze kukamilika na hatimaye huduma zilizokusudiwa kutolewa katika jengo ziweze kufanyika.

Pia, Waziri Mkuu amewataka Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Daniel Nkungu na Kiongozi wa Wauguzi, Wambura wahakikishe wanaimarisha ushirikiano wao na hata wanapotoa maagizo kwa wasaidizi wao wawe wanataarifiana.

Kwa upande wa watumishi wanaofanya kazi katika idara za maabara amewataka wawe wanawahi kutoa huduma kwa sababu kuna malalamiko ya ucheleweshwaji wa huduma katika eneo hilo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watumishi wanaofanya kazi katika kitengo cha radiolojia kwenye hospitali za Rufaa za Mkoa za Mwananyamala na Temeke jijini Dar es Salaam waache urasimu na wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao.


(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.