*Wananchi waipongeza kwa kuwa umeimarisha utoaji wa huduma za afya
WANANCHI
wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John
Magufuli kwa kuwabana watumishi wa umma, kwa sababu uamuzi huo umezaa
matunda na sasa hali ya utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini
yakiwemo ya hospitali yameimarika.
Kauli
hiyo imetolewa leo (Jumatano, Februari 27, 2019) na wagonjwa waliolazwa
katika wodi ya wazazi kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke
jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
hospitali hapo.
“Huduma
zimeimarishwa dawa tunapata, hakuna lugha chafu wala kuombwa rushwa.
Tunahudumiwa vizuri na kuna wakati hadi tunabembelezwa kunywa dawa mambo
ambayo hapo nyuma hayakuwepo, hivyo tunaishikuru Serikali.”
Mmoja
wa wagonjwa hao ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi hospitalini hapo
baada ya kujifungua, Mwajuma Mohammed amesema baada ya Serikali ya Awamu
ya Tano kuingia madarakani na kuwabana watumishi wa umma sasa kuna
mabadiliko makubwa sana ya kiutendaji.
Amesema
zamani baadhi ya wauguzi hususani wanaofanyakazi kwenye wodi ya wazazi
hawakuwa na lugha nzuri walikuwa wakiwatukana na kuwakashifu jambo
ambalo kwa sasa halipo, kwani wakifika wapokelewa vizuri.
Mama
mwingine aliyelazwa kwenye wodi hiyo, Crista Moyo amemuomba Waziri Mkuu
kuisadia hospitali hiyo kwa kuiongezea watumishi kwa kuwa walipo ni
wachache ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo
kila siku.
Crista
ameishauri Serikali ikiwezekana iajiri hata watu wasiokuwa na taaluma
ya udaktari au uuguzi ili wakafanyekazi ambazo hazihitaji ujuzi kama
za kuwasaidia wagojwa kutoka eneo moja kwenda lingine.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu amezishauri Halmashauri jijini Dar es Salaam zihakikishe
zinaendelea kuimarisha vituo vya afya na kuongeza vingine ili utoaji
kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za rufaa.
Pia
ameshauri ianzishwe miradi ya ujenzi wa nyumba za watumishi katika
hospitali hizo kwa lengo ya kuwezesha utoaji wa huduma mbalimbali
zikiwemo za dharura kwa wakati.
“Rais
Dkt. Magufuli anataka wananchi wapate huduma za afya karibu na makazi
yao ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Ndio maana tunajenga vituo vya afya vilivyokamilika vinavyotoa huduma
zote muhimu kama maabara, upasuaji na mama na mtoto.”
Waziri
Mkuu amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua utoaji wa huduma za afya
zinazotolewa katika hospitali hizo na kubaini kama kuna changamoto ili
Serikali iweze kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi.
“Tumesikia
changamoto zinazowakabili madaktari, tumezichukua na tutazifanyia kazi
ikiwepo ya upungufu wa watumishi mbalimbali kama madaktari na wauguzi
ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi.”
Waziri
Mkuu amesema dhamira ya dhati ya Serikali kwao ni ya kuwatumikia
wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo waendelee kuwa
wazalendo na washirikiane na Serikali yao. Wafanye kazi kwa bidii.
Naye,Mganga
Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Amaani Malima amesema hospitali hiyo
inahudumia wagonjwa wa nje 1,800 hadi 2,000 kwa siku na wagonjwa wa
ndani 250 hadi 300. Wagonjwa hao watoka wilaya mbalimbali.
Dkt.
Malima amesema hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 439 kati yao
madaktari bingwa ni 16, madaktari 76 na wauguzi 209 na watumishi wengine
138. “Idadi hii ni ndogo kulingana na mahitaji ya hospitali kwani tuna
upungufu wa watumishi 278 sawa na asilimia 39.”
Akizungumzia
hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwenye hospitali hiyo, Dkt. Malima
amesema kwa kipindi cha Januari upatikanaji ulikuwa wa kuridhisha kwa
asilimia 85 ya kiasi cha dawa na vifaa tiba vilivyohitajika.
Awali,
Waziri Mkuu alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala
ambapo alikagua mradi wa ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa mashuhuri
ambalo lilianza tangu mwaka 2014 na bado halijakamilika.
Hivyo,
ameishauri Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuangalia namna ya
kuweza kusaidia ujenzi wa jengo hilo ili mradi huo uweze kukamilika na
hatimaye huduma zilizokusudiwa kutolewa katika jengo ziweze kufanyika.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Daniel Nkungu
na Kiongozi wa Wauguzi, Wambura wahakikishe wanaimarisha ushirikiano wao
na hata wanapotoa maagizo kwa wasaidizi wao wawe wanataarifiana.
Kwa
upande wa watumishi wanaofanya kazi katika idara za maabara amewataka
wawe wanawahi kutoa huduma kwa sababu kuna malalamiko ya ucheleweshwaji
wa huduma katika eneo hilo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewataka watumishi wanaofanya kazi katika kitengo cha
radiolojia kwenye hospitali za Rufaa za Mkoa za Mwananyamala na Temeke
jijini Dar es Salaam waache urasimu na wafanye kazi kwa kuzingatia
maadili ya taaluma zao.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.