WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 21 kwa viwanda vyote vinavyozalisha vileo nchini viwe vimefunga mfumo ukusanyaji kodi kwa kutumia stempu za kielektroniki.
Pia ameziagiza Wizara
na Taasisi zote za Umma ziwe zimejiunga na Mfumo wa Serikali wa
Kielektroniki wa ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli (GePG) kabla ya
Juni mwaka huu.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Februari 9, 2019) , wakati akiahirisha mkutano wa kumi na nne wa Bunge la kumi na moja, Bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isimamie uwekaji wa mifumo hiyo na ifikapo februari 28, 2019 kila kiwanda kiwe kimefunga mfumo huo.
“Naielekeza
TRA kusimamia uwekaji wa mifumo ya kukusanya kodi za vileo kwa kutumia
stempu za kielektroniki kwa viwanda vyote vinavyozalisha vinywaji
hivyo.”
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali
inaendelea kuchukua hatua za kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa
matumizi ya fedha na rasilimali za umma ili kufikia malengo.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutumia
mfumo wa kielektroniki wa stempu za kodi kwenye viwanda vinavyozalisha
bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na zile zinazoingizwa nchini.
Waziri
Mkuu amesema mfumo huo utasaidia Serikali katika kupata taarifa sahihi
za uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato ya Serikali.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza maelekezo
ya Rais Dkt. John Magufuli aliyoyatoa Januari 22, 2019, alipokutana na
wadau wa sekta ya madini.
AmesemaSerikali imefutaKodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Zuio ya asilimia tano ya
mwisho inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote kwa
wachimbaji hao.
Waziri
Mkuu amesema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza utoroshwaji wa madini;
kuwatambua wachimbaji wadogo kupitia masoko ya madini yatakayoanzishwa.
Pia
itasaidia kuwapunguzia gharama wachimbaji wadogo na hivyo kuendesha
shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuongeza wigo wa mapato kwa kuwa
madini yatauzwa ndani ya nchi.
“Nitoe
rai kwa wachimbaji wote wadogo kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za
Serikali kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika kikao na Mheshimiwa
Rais.”
Amesema
siku zote Watanzania wanamuenzi Rais Dkt. John Magufuli, kwa hatua za
makusudi anazochukua katika kuhakikisha anaimarisha mifumo ya ukusanyaji
wa mapato.
Waziri
Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anafanya hayo yote kwa lengo la kuona
Tanzania inapunguza utegemezi wa misaada kutoka katika mataifa mengine.
“Mifano
maelekezo aliyoyatoa kwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa wawasilishe
mapendekezo kuhusu namna bora ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani
katika maeneo yao.”
Waziri
Mkuu amesema tayari Serikali imeshapokea mapendekezo hayo na imetoa
maagizo mahsusi kwa TRA na TAMISEMI zishirikiane katika ukusanyaji wa
kodi za majengo.
Akizungumzia kuhusu hali ya uchumi, Waziri Mkuu amesema imeendelea
kuimarika, ambapo kati ya Januari hadi Septemba 2018, pato la Taifa
lilikua kwa wastani wa asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 6.2
katika kipindi kama hicho mwaka 2017.
AmesemaOngezeko
hilo la ukuaji wa uchumi limechochewa zaidi na uwekezaji mkubwa kwenye
miundombinu hususan ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.
Waziri Mkuu amesema masuala mengine yaliyochangia ukuaji mzuri wa uchumi ni kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati na hali nzuri ya hewa kwa upande wa kilimo.
“Shughuli
za kiuchumi zilizoendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa
kipindi hicho ni kilimo (asilimia 33.4), ujenzi (asilimia 15.7) na
biashara (asilimia 10.2).”
Amesema
kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo, Serikali itaendelea kuboresha
miundombinu ya umwagiliaji, kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana
kwa wakati.
Pia
kuhakikisha huduma za ugani zinaimarishwa katika maeneo yote nchini
pamoja na kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko.
Lengo
la Serikali ni kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo na
hivyo kumwongezea kipato mkulima kitakachomwezesha kujikimu na
kujikwamua na umaskini.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.