Sunday, May 24, 2020

RAIS DKT MAGUFULI AWASHUKURU WATANZANIA KWA KULIOMBEA TAIFA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Viongozi wa Dini ya Kiislam, Mkoa wa Dodoma, wakati akiwasili katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, kuhudhuria Sala ya Eid el Fitri, May 24, 2020.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiitikia dua, baada ya sala ya Eid el Fitri, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020.
Waumini wa Dini ya Kiislamu, waliyohudhuria katika ibada ya sala ya Eid el Fitri, akiitikia dua, baada ya sala, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia Waumini wa Dini ya Kiislam, baada ya sala ya Eid el Fitri, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwahutubia Waumini wa Dini ya Kiislam, baada ya sala ya Eid el Fitri, katika Msikiti wa Gaddafi, Jijini Dodoma, May 24, 2020.


WAZIRI KAIRUKI AWATOA HOFU WAWEKEZAJI NCHINI

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri ya Mkuu anayeshughulikia  Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki amewatoa hofu wawekezaji na wafanyabiashara juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akingumza  mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma, wakati wa ziara yake  ya kukagua shughuli za uzalishaji katika viwanda vinavyozalisha mvivyo kikiwemo DOMIYA ESTATE kinachozalisha  vinywaji vikali na baridi kama  soda, maji na chai baridi aina ya ASANTE na kiwanda  cha Alko Vintages Co. Ltd amesema kuwa Serikali ina mipango na mikakati ya kuhakikisha kuwa kuna  mazingira bora ya uwekezaji.
“Serikali inatambua changamoto mnazopitia na imeweka mikakati ya kuhakikisha inazitatua ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji nchini inayolenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji,”alisema Waziri Kairuki
Amesema, changamoto ambazo wawekezaji wamekuwa wakikabiliana nazo zinaendelea kutatuliwa ikiwa ni pamoja na; utitiri wa kodi, ukosefu wa maji ya uhakika, ubovu wa miundombinu ya barabara, gharamza kubwa za uzalishaji, uzalishaji duni kwa ubora na wingi wa zabibu, ukosefu wa aina mabalimbali za zabibu.
Changamoto nyingine walizobainisha ni; ugumu wa kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika zabibu, ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha zabibu, pamoja na uwepo wa bidhaa zisizo na ubora sokoni.
Akijibu changamoto hizo, Waziri Kairuki aliwatoa hofu kwa kuainisha maeneo muhimu yaliyofanyiwa maboresho ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa tozo na kodi zaidi ya 168 nchini, kuendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwemo barabara zinazosimamiwa na TARURA,  kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme na maji ili kila mwekezaji na mfanyabiashara anufaike na kuwekezaji kwake.
Aidha Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo  cha Uwekezaji nchini  inaendelea kuandaa mpango wa kuteua mabalozi kwa lengo la kuvutia wawekezaji kama ilivyo  katika sekta nyingine ikiwemo utalii.
“Tumeendelea na hatua za awali za kuanzishwa kwa mpango wa kuwa na mabalozi watakao tangaza masuala ya uwekezaji nchini, hii ni pamoja na kushirikisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuona namna ya kupata mabalozi hao watakaofikia taifa na nje ya Nchi,”alisisitiza Waziri Kairuki
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashauri wawekezaji kuvitumia vyema vyombo vya habari katika kutoa elimu na kujitangaza ili kuendelea kuwa na soko la uhakika kwa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha.
Naye Mchumi Mkuu kutoka idara ya Uwekezaji Bw. Francis Mollay, alibainisha baadhi ya jitihada za kuhakikisha wawekezaji wananufaika na uwekezaji wao pamoja na uwepo wa sheria na kanuni zinazobainisha namna bora ya kuboresha mazingira yao ili kuwa na maendeleo katika sekta zote.
“Tunaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupitia sheria na sera zinazohusiana na kodi mbalimbali ili kutatua changamoto za kikodi zilizopo,”alieleza Mollay.
Kwa upande wake Mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Alko Vintages Bw. Archard Kato alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na kutoa rai kwa vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo hasa cha zabibu kwa kuonesha nia na uthubuti ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Vijana lazima mjiamini na kuwa na uthubutu katika kuanzisha biashara ili kuingia kwenye sekta ya uwekezaji, hakikisha una maono au jambo linalokuvutia na weka mikakati ya kulifikia.Hakikisha unajaribu wazo ulilonalo na kuwatumia walioweza katika hilo, utayaona manufaa kama kijana,”alisema Kato.
Kiwanda kingine alichotembelea ni Alko Vintages Co. Ltd kinachozalisha mvinyo wa aina mbalimbali ikiwemo Dompo, Altar, St. Mary’s, Image, Rose na Klymax viliyopo katika Wilaya ya Dodoma Mjini mkoani Dodoma.

=MWISHO=

Friday, May 22, 2020

BUNGENI LEO 22.05.2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Angelah Kairuki, Bungeni jijini Dodoma, May 22, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Bungeni jijini Dodoma, May 22, 2020.

WAHITIMU WA VYUO VYA ELIMU YA JUU 3,200 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA VITENDO SEHEMU ZA KAZI

Sehemu ya Vijana wanufaika wa Mafunzo ya Vitendo sehemu za Kazi “Internship Training” wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani).
Baadhi ya washiriki wakisikiliza kwa makini maelezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani). Kushoto ni Afisa Kazi kutoka Kitengo cha Huduma za Ajira Bw. Hussein Hassan na Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa GIBRL Business Solutions Ltd, Bi. Hadija Jabir.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela akitoa taarifa kuhusu Mafunzo ya Vitendo sehemu za Kazi “Internship Training” kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mafunzo wanayopatiwa vijana hao na waajiri katika mkoa huo. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela mara baada ya kuwasili mkoani Iringa wakati wa ziara ya kuwatembelea waajiri wenye vijana wanaopatiwa mafunzo sehemu za kazi “Intenship” Mei 21, 2020.

WAHITIMU WA VYUO VYA ELIMU YA JUU 3,200 WANUFAIKA NA MAFUNZO YA VITENDO SEHEMU ZA KAZI

 Na; Mwandishi Wetu - Iringa
Vijana wahitimu wa Vyuo vya elimu ya juu zaidi ya 3,200 nchini wamenufaika na Mafunzo ya vitendo mahala pa kazi “Internship Training” yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira ambapo zamani ilikuwa ni Wakala wa Huduma za Ajira (TAESA).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa katika ziara Mkoani Iringa kutembelea waajiri wenye vijana wanaowapatia mafunzo katika sehemu zao za kazi yaani “Interns”.

Waziri Mhagama alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa yakihusisha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu ambapo wanapatiwa fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya kazi kwa lengo la kuwapatia uzoefu wa kazi utakaowasaidia kuajiriwa au kujiajiri.

“Kuanzishwa kwa mafunzo hayo ilikuwa ni moja kati ya maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba vijana hususani kwenye masuala ya ajira nchini, hivyo vijana waliomaliza kozi mbalimbali kupatiwa ujuzi katika maeneo ya kazi ili waweze kuwa na uzoefu pale wanapojiajiri ama kuajiriwa,” alisema Mhagama

Aliongeza kuwa Mpango huu wa mafunzo ya vitendo mahala pa kazi umekuwa na mchango mkubwa na ni chachu katika kuwezesha nguvukazi ya taifa hususan vijana waliohitimu kwa kuwajengea uzoefu, weledi na maadili ya kazi yanayohitajika pindi wanapoajiriwa.

“Tunataka kuona vijana wanapomaliza mafunzo haya wanakuwa na dhana ya kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu hii ya tano kwa kuwa tayari mnauzoefu,” alisema Mhagama

“Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufanya tathmini ya mafunzo haya na mafunzo mengine yanayotolewa chini ya Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuona namna ujuzi wanaopatiwa vijana nchini unakuwa wa manufaa katika kuwezesha vijana wanakuwa sehemu ya kufikisha taifa lao katika uchumi wa kati,” alieleza Mhagama

Aidha Waziri Mhagama alitoa wito kwa vijana ambao wamenufaika na mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidi, weledi na maarifa kwa kuonyesha umahiri wa kujenga uchumi wa taifa.

Sambamba na hayo, alitoa pongezi kwa waajiri wote nchi katika sekta ya Umma na Binafsi kwa namna walivyoshirikiana na Serikali katika kuwapatia vijana mafunzo hayo kwa muda wa miezi sita hadi mwaka mmoja na wamekuwa sehemu ya mafanikio katika kuziwezesha taasisi kufikia malengo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela alieleza kuwa Programu hiyo ya mafunzo kwa Vitendo sehemu za Kazi imekuwa na manufaa makubwa kwa vijana na ameiomba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha ujao kutenga bajeti zaidi kwa ajili ya kuwezesha vijana wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini ili waweze kunufaika na mafunzo hayo.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa GIBRL Business Solutions Ltd, Bi. Hadija Jabir alisema kuwa uwepo wa vijana wanaopatiwa mafunzo hayo katika kampuni yake umekuwa na tija.

“Kama mwajiri nimeona ufanisi wa vijana hao, naiomba serikali iwapatie nafasi zaidi ya vijana hao wanaohitimu kufanya mafunzo katika sehemu za kazi ili yale waliyojifunza kwa nadharia waweze kuyatekeleza kwa Vitendo,” alisema Jabir

Naye, Mmoja wa Wanufaika wa Mafunzo hayo, Bi. Felister Gerald ameishukuru serikali kwa kutambua mchango wa vijana na kuwapatia mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kuwajengea uzoefu na ujasiri wa kufanya kazi.

Tuesday, May 19, 2020

WAZIRI MKUU AWASIMAMISHA KAZI WATUMISHI WATATU TEMESA

* Atoa onyo kwa Mtendaji Mkuu wa TEMESA
* Taasisi za Serikali zapewa miezi miwili kulipa deni la sh. bil 25

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa sh. milioni 780 zinazotokana na zabuni.

Vile vile, Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi miwili kwa taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na TEMESA kiasi cha sh. bilioni 25.88 ziwe zimeshalipa na iwapo kuna taasisi itashindwa kulipa deni lake hadi Julai 30, 2020 apewe taarifa.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Mei 19, 2020) alipotembelea karakana ya mitambo ya TEMESA jijini Dodoma na amewasisitiza watumishi hao wafanye kazi kwa uadilifu na Serikali haihitaji wala haitowavumilia watumishi wazembe.

Watumishi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Hans Lyimo, Kaimu Mhasibu Mkuu, Jonas Bakuza na Lecian Mgeta aliyekuwa Mhasibu wa Wakala huo ambaye aliandika barua ya kuacha kazi Aprili 6, 2020. Waziri Mkuu ameagiza mtumishi huo arudishwe kazini ili akajibu tuhuma zinazomkabili.

“Kazi hii imefanywa kwa ushirikiano na Afisa wa benki ya CRDB asiyekuwa muaminifu ambaye naye tutamtafuta hadi tumpate. Fedha hizo zilikuwa kwenye mfumo wa hundi wao wakazibadilisha na kuziweka katika mfumo wa fedha taslimu. Umakini usipokuwepo fedha zote zitakuwa zinaliwa tu.”

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemuonya Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Japhet Maselle kutokana na usimamizi wake usioridhisha, ambapo amesema Mtendaji huyo alikuwa anajua kuhusu upotevu wa fedha katika wakala huo na hakuchukua hatua kwa wahusika.

 “…si mzuri kwenye usimamizi unapenda kuacha watu wanaofanya maovu wakiwemo na watumishi hawa watatu. Mtendaji ulikuwa unajua, ulikuwa hauchukui hatua hadi uliposikia nakuja, hii si sahihi sheria zipo na maelekezo ya Serikali yapo. Upotevu wa sh. milioni 780 katika taasisi ni doa.”

Waziri Mkuu amesema kufuatia na matumizi mabaya ya fedha yanayofanywa TEMESA, amemuagiza Mdhibiti na Makaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akafanye ukaguzi katika wakala huo kutokana na upotevu wa sh. milioni 780 zilizotakiwa zipelekwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na wakala huo ziwe zimelipa madeni yote katika kipindi cha miezi miwili ili kuiwezsha TEMESA kuweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Tukishapata bilioni 25 TEMESA hii tukapeleka walau bilioni moja moja kila mkoa watanunua mitambo, watanunua vipuri na magari yatatengenezwa kwa haraka. Magari yote ya Serikali lazima yatengenezwe TEMESA kwa sababu ya uhakika wa usalama wake.”

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wakala huo ufanye maboresho makubwa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sehemu ya magari kwa kuwa inalalamikiwa zaidi hususani suala la utengenezaji wa magari yanayopelekwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa wanalalamikia gharama kubwa wanazotozwa kwa ajili ya utengenezaji wa magari, hivyo lazima ziangaliwe kama ni halisi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wakala huo ujiridhishe kila kivuko kama ni kizima ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea na wavifanyie ukaguzi wa mara kwa mara.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TEMESA alisema wakala huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo madeni makubwa yanayotokana na huduma zao kutolipwa kwa wakati au kutolipwa kabisa.

“…kwa mfano hadi mwezi Machi 2020 tunazidai taasisi za Serikali kiasi cha shilingi 25,882,593,038 na wakati huo huo tukidaiwa na wazabuni mbalimbali kiasi cha shilingi 18,959,630,408.”

Changamoto nyingine aliyoitaja ni uchakavu wa karakara nyingi zinazomilikiwa na wakala huo katika makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini, hivyo kuathiri ufanisi katika matengenezo ya magari ya Serikali.


(mwisho)

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KARAKANA YA MITAMBO YA WAKALA WA UFUNDI NA UMEME (TEMESA)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia ghala la spea za magari, katika yadi ya TEMESA, jijini Dodoma, May 19, 2020, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala hao wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia magari, katika yadi ya TEMESA, jijini Dodoma, May 19, 2020, yaliyofika kwa ajili ya matengenezo, wakati alipotembelea karakana hiyo ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia mashine ya kukandamizia vipuri, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020, 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020, alipotembelea karakana hiyo.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiangalia mashine ya kupimia matairi, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020, 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimsikiliza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimsikiliza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na watumishi wa TEMESA, baada ya kukagua karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimpa onyo, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, baada ya kutoridhishwa na utendaji wake, wakati alipotembelea karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020, katikati ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, baada ya kukagua karakana ya mitambo ya wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), jijini Dodoma, May 19, 2020,


WAZIRI KAIRUKI AHIMIZA WAWEKEZAJI KUONGEZA UZALISHAJI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amehimiza wawekezaji katika sekta mbalimbali kuongeza uzalishaji zaidi hususani katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya bidhaa mbalimbali yanazidi kukua katika soko la ndani. Ameyasema hayo leo tarehe 18 Mei 2020 alipotembelea Kiwanda cha OK Plast Ltd kilichopo Vingunguti, Dar Es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazoendelea kiwandani hapo na kusikiliza changamoto zao.

Kiwanda hicho cha OK Plast Ltd ni moja ya viwanda vichache vinavyochakata skrepaza shaba na kuzalisha bidhaa za mwisho kama vile nyaya za aina mbalimbali za umeme pamoja na malighafi za viwanda vingine kama vile ingoti za betri, kathodi na rodi za shaba.

Wakati akimpatia maelezo ya uwekezaji wa kiwanda hicho, Meneja wa Kiwanda Bw. Fadl Ghaddar ameeleza kuwa hadi sasa wameshawekeza takribani Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ambapo amebainisha kuwa tangu waliposajili mradi huo Mwaka 2005 umekuwa ukijiendesha kwa mafanikio ikiwemo kuweza kuzalisha bidhaa zenye uhakika wa soko la hapa nchini huku wakiendelea kupokea oda za bidhaa kutoka nchi jirani hususani kutoka Kenya.

Meneja huyo aliongeza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kuajiri jumla ya wafanyakazi 600 ambapo kati yao 595 ni Watanzania na 5 tu ndiyo raia wa kigeni. Aidha, alifafanua kuwa wanajivunia kuweza kuendelea kutoa mafunzo ya ujuzi wa kushughulikia aina mbalimbali za metali kwa waajiriwa wao na hata wale wanaoamua kuacha kazi huondoka wakiwa na ujuzi wa kuweza kuanzisha karakana zao na kujitegemea. Kiwanda hicho kinalipa Kodi taribani Shilingi bilioni 2 kwa mwaka, alieleza. 

Hata hivyo, Bw. Ghaddar alibainisha kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni uhaba wa malighafi ya skrepa ya shaba jambo ambalo limepelekea Kiwanda kuzalisha chini ya uwezo wake ambapo kwa sasa huzalisha takriban tani 150 za bidhaa mbalimbali za shaba kwa mwezi huku uwezo wa kiwanda kuzalisha ukiwa tani zaidiya 500 kwa mwezi. Alieleza kuwa changamoto hiyo inatokana na ukweli kwamba licha ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya BICO ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuonesha kuwa kuna upatikanaji wa kutosha wa skrepa ya shaba hapa nchini kutosheleza mahitaji ya viwanda vya kuchakata malighafi hiyo, kuendelea kuuzwa nje ya nchi kwa skrepa kumesababisha uhaba wa malighafi hiyo kwa viwanda vinavyoihitaji hapa nchini. Hivyo, alishauri na kutoa ombi kwa Serikali kupitia kwa Waziri wa Uwekezaji kuliangalia suala hilo ili kulinda viwanda vya ndani kwa kuvihakikishia upatikanaji wa malighafi ya kutosha ili kuepuka kutumia fedha za kigeni kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri Kairuki aliupongeza uongozi wa Kiwanda hicho kwa kuhakikisha uzalishaji kiwandani hapo unaendelea kama kawaida licha ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo. Alipongeza pia hatua ya Kiwanda hicho kuitikia wito wa Serikali kwa wawekezaji wa kuajiri Watanzania kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na wazawa pamoja na kuweka program nzuri kwa wataalamu wa kigeni kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kwa wafanyakazi wa kitanzania. Alitumia pia fursa hiyo kuwapongeza kwa kulipa kodi za Serikali kwa mujibu wa Sheria na kuwataka wawekezaji wengine pia kuiga mfano huo ikiwa ni sehemu ya wajibu wao kwa Serikali.

Aidha alitoa wito kwa wawekezaji waliojisajili Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)  kuendelea kuwasilisha taarifa za maendeleo ya miradi yao kila baada ya miezi 6 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za usajili TIC ili Kituo kiweze kufahamu na kufuatilia kwa karibu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa wakati.

Waziri Kairuki anatarajia kuendelea na ziara ya kutembelea miradi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali katika Mikoa ya Dodoma na Singida kwa lengo la kusikiliza chanmagamoto zao  na kuhamasisha uzalishaji hususani wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa hapa nchini badala ya kuagizwa kutoka nje ya Nchi.

Monday, May 18, 2020

BUNGENI LEO 18.05.2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Bungeni jijini Dodoma, May 18, 2020.

Thursday, May 14, 2020

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA RELI YA KISASA (SGR)

*Asema umetoa ajira zaidi ya 18,000; utapunguza muda wa safari
* Asema nguzo za umeme 154 kati ya 160 zimeshasimikwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kusema kuwa mradi huo umesaidia kupungua tatizo la ajira kwa kuajiri wafanyakazi 18,700.

“Kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu, kumesaidia kupunguza ukosefu wa ajira kwa kutoa ajira 7,400 kwa kipande cha Dar hadi Morogoro. Kipande cha Morogoro hadi Singida kimetoa ajira 6,300 wakati mradi wa umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere nao pia umetoa ajira 5,000,” amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Alhamisi, Mei 14, 2020) baada ya kutembelea mradi huo na kuzungumza na wananchi aliowakuta kwenye stesheni ya Soga, iliyoko wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

Amesema faida nyingine ya mradi huo katika awamu yake ya kwanza, ni kupunguzwa kwa muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro. Amewataka wananchi hao wawe walinzi wa mradi huo kwa sababu utakapokamilika utawanufaisha na wao pia.

Reli hiyo itakuwa na vituo sita vya Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro, huku vituo vya Dar es Salaam na Morogoro vikiwa ndiyo vituo vikuu. “Kwenye vituo vya kushusha abiria vya reli hii, kutakuwa na huduma za kibenki na maduka, kwa hiyo wananchi hata kama hamsafiri, mtaweza kupata huduma na mahitaji yenu kutokea hapo,” amesema.

Akielezea maendeleo ya mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili, Waziri Mkuu amesema Serikali iliweka malengo ya kukamilisha mradi huo kwa wakati na ndiyo maana aliamua kwenda kuukagua.

“Katika awamu ya kwanza, ambayo inatoka Dar es Salaam hadi Morogoro (km. 300), mradi huu umekamilika kwa asilimia 77.91. Hii maana yake ni kwamba wamemaliza kazi hii kwa zaidi ya robotatu. Wametengeneza njia na kulaza mataruma na mimi nimekuja na hii treni maalum kwa karibu kilometa 20,” amesema huku akishangiliwa na wananchi hao.

“Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli alianzisha mradi huu na kuwaahidi Watanzania kwamba tunaweza kuujenga kwa fedha zetu. Vilevile, mradi huu ni utekelezaji wa agizo la Ilani ya CCM ambalo linaitaka Serikali ya awamu ya tano, iimarishe usafiri wa reli nchini.”

Amesema katika kutekeleza agizo hilo, Serikali ya awamu ya tano, mbali ya kujenga reli hiyo ya kisasa, imefanikiwa pia kufufua reli ya kutoka Dar – Tanga – Moshi ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 20. Huduma ya mizigo katika reli hiyo ilikuwa haifanyi kazi kwa miaka 12 na huduma ya kusafirisha abiria ilisitishwa tangu mwaka 1994.

Akielezea kuhusu awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa reli kutoka Morogoro hadi Makutupora, Dodoma (km. 422) ulianza mwaka jana mwishoni na sasa hivi umefikia asilimia 30 ya kazi, ambapo wanatarajia kuukamilisha ifikapo Juni, 2021.

Waziri Mkuu amesema sambamba na ujenzi wa reli hiyo, umeme pia umeanza kuwekwa ambapo nguzo 154 kati ya 160 zinazotakiwa kuwepo zimeshasimikwa. “Tumeweka miundombinu ya umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere, kutoka Kidatu na Kinyerezi. Nia yetu ya kupata umeme kutoka vyanzo vyote vitatu, ni kuhakikisha kuwa umeme upo saa zote.”

“Tuna uhakika wa kutumia umeme wa Kinyerezi na Kidatu au Kidatu na Mwalimu Nyerere au Mwalimu Nyerere na Kinyerezi na hata umeme ukikatika kabisa, mabehewa yetu yana uwezo wa kutunza umeme kwa dakika 45, na katika muda huo, ni lazima tutakuwa tumerejesha umeme kutoka chanzo kimojawapo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa reli hiyo na akawapongeza mafundi wa kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki ambayo inajenga reli hiyo. “Kampuni ya Yapi Merkezi imefanya kazi kama walivyosaini kwenye mkataba na Serikali, na ninaamini watakamilisha kazi kabla ya muda,” amesema.

(mwisho)

WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA KUZALISHA UMEME WA JNHPP

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Waziri wa Nishati Dkt. Medad Kalemani, wakati alipokagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Serikali na kampuni ya Yapi Merkezi kabla ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (watatu kushoto) akikagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, unaojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi, May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (watatu kushoto) akikagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, unaojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi, May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (watatu kushoto) akikagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, unaojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi, May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (watatu kushoto) akikagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, unaojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi, May 14, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Kaimu Mhandisi Mkazi, Injinia Lutengano Mwandambo, wakati  akikagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, unaojengwa na kampuni ya Yapi Merkezi, May 14, 2020.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Waziri wa Nishati Dkt. Medad Kalemani, wakati alipokagua hatua za utekelezaji wa mradi  wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha Megawati 2,115, May 14, 2020.