Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, kuwa imeweka mikakati ya Kudhibiti UKIMWI na Dawa za kulevya ili kuimarisha ustawi wa wananchi nchini.
Hayo
yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama,tarehe 29 Machi 2021, Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha kwa kamati hiyo,
taarifa ya Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 na makadirio ya Bajeti ya mwaka 2021/2022 ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania na Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya.
“Kazi hii ya kuwaokoa vijana na watanzania kwenye
UKIMWI na dawa za kulevya tumeshafanya vizuri. Tumewasaidia waraibu 10,565
ambao wanapatiwa matibabu katika kliniki za Methadone nchini. Tumeandaa mkakati
wa kuhakikisha kuwa waraibu hao hawarejei tena katika matumizi ya dawa za
kulevya na tunafanya hivyo kupitia Idara ya Kazi na Ajira.” Amesisitiza Mhe.
Mhagama.
Mhe. Mhagama amefafanua kuwa, Serikali
imetengeneza mtandao wa Asasi ambapo hadi sasa kuna takribani Asasi 52 nchi
nzima ambazo zinashirikiana na Serikali Katika shughuli za udhibiti wa
dawa za kulevya. Aidha, ameongeza kuwa tayari mwongozo wa namna Kamati za
UKIMWI za Halmashauri zitakavyoratibu shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya na
Asasi zilizopo kwenye Halmashauri husika
umeshaandaliwa.
Amesisitiza kuwa, serikali inaendelea kushirikiana na nchi nyingine kwenye kudhibiti
na kupambana na Dawa za kulenya kwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa Katika kukabiliana na
tatizo la dawa za kulevya, amesema Operesheni za Kupambana na
biashara ya Dawa za Kulevya zimefanyika kwa umakini, ambapo Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Februari
2021 wamekamatwa jumla ya watuhumiwa 5,374
wakiwemo wanaume 4,917 na wanawake 457.
Kadhalika,
amesema Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetoa mafunzo kwa waratibu wa
UKIMWI kwa Halmashauri 185 juu ya ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya takwimu
sizizo za kitabibu TOMSHA. Pia ameeleza kuwa ufuatiliaji
na usimamizi na Ukaguzi wa takwimu za kila robo mwaka umefanyika katika Mikoa
yote 26.
“Hadi Desemba mwaka
jana, utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kimataifa wa Kudhibiti na
Kupambana na UKIMWI wa 90-90-90, ulionesha mafanikio kwenye WAVIU milioni 1.4, sawa na asilimia 83 ya
WAVIU wote walikuwa wanatambua hali zao za
VVU. Tulifanikiwa WAVIU milioni 1.36 sawa na asilimia 98 walikuwa kwenye
tiba na matunzo ya ARV na jambo la faraja ni kuwa asilimia 92 ya waliokuwa
kwenye tiba ya ARV walikuwa na kiwango cha chini cha VVU mwilini.” Amesema Mhe.
Mhagama
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq amebainisha kuwa
kamati yake imeridhika na jinsi serikali ilivyozingatia ushauri wa kamati hiyo uliolenga kuimarisha jitihada
za kudhibiti dawa za kulevya na UKIMWI nchini. Amefafanua kuwa matatizo ya dawa
za kulevya na UKIMWI ni mtambuka na yanaathiri sekta mbalimbali hivyo serikali
haina budi kuendelea kushirikana na wadau katika kuhakikisha wanaimarisha
ustawi wa wananchi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi, Naibu Waziri
Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu) Mhe. Ummy Ngeriananga, Katibu Mkuu (Bunge
na Waziri Mkuu), Tixon Nzunda, Katibu Mkuu (Sera
na Uratibu), Dorothy Mwaluko, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa
za Kulevya. James Kaji pamoja na Wakurugenzi na Wataalam wa
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Dira ya
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ni “Kujenga jamii ya
Watanzania isiyotumia dawa za kulevya na kutoshiriki katika biashara ya dawa
hizo”. Aidha, Dira ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania ni: “Kuwa Taasisi yenye hadhi inayoongoza Tanzania katika kuelekea
kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na UKIMWI”.
MWISHO.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala
ya UKIMWI, Mhe. Fatma Tawfiq akieleza umuhimu wa Ofisi ya
Waziri Mkuu kushirikiana na wadau katika kuimarisha ustawi wa watanzania wakati kamati hiyo walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini
Dodoma
Makatibu wakuu na wakuu wa Taasisi za Ofisi ya Waziri Mkuu, wakifuatilia kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.
Baadhi ya Wakurugenzi na wataalamu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia
kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge
inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili
utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma,
Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko, akieleza mikakati waliyoipanga katika kudhibiti UKIMWI nchini wakati wa kikao cha Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Jijini Dodoma, tarehe 29 Machi 2021.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu)
Mhe. Jenista Mhagama akiwaongoza Manaibu Mawaziri, Makatibu wakuu, Wakuu wa
Taasisi, Wakurugenzi na Wataalamu wa Ofisi hiyo , wakati wa kikao cha Ofisi hiyo na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia masuala ya
UKIMWI, walipokuwa wakijadili utekelezaji majukumu wa Mamlaka
ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Tume ya Kudhibiti UKIMWI
Tanzania, Jijini Dodoma
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.