Tuesday, October 18, 2022

WATENDAJI WAASWA KUTUNZA VITENDEA KAZI VYA OFISI



Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bwn. Kaspar Mmuya ametoa rai kwa watendaji wa serikali kutunza vizuri vyombo vya usafiri walivyopewa ili viweze kuwasaidia katika utendaji wa kazi na  kudumu kwa muda mrefu.

Wito huo umetolewa wakati wa kukabidhi bajaji mbili kwa watumishi wa Ofisi ya Mpiga chapa wa serikali jijini Dar es saalam katika kuwajengea Mazingira mazuri watu wenye ulemavu ya utendaji wa kazi.

“Ofisi ya Waziri Mkuu moja ya jukumu lake ni kuwezesha watu wenye ulemavu kwa kusimamia Sera ya Watu wenye Ulemavu na Miongozo ya watu wenye Ulemavu”

Akitoa neno la shukrani Bwn. Ophin Malley ameshukuru  serikali kwa kuwatambua watu wenye ulemavu katika mazingira waliyonayo mahala pa kazi.

“Tunaomba kama itafaa tuweze kupatiwa baiskeli maalumu ili zituwezeshe kuturahisishia kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakati wa utendaji wa Kazi”

 

Wednesday, October 12, 2022

SERIKALI YAOMBA VIONGOZI WA DINI KUKEMEA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA

 


Serikali imetoa rai kwa viongozi wa dini kuendelea  kuhimiza jamii kuepuka uraibu wa matumizi ya dawa za kulevya na kujenga uelewa kuhusu madhara ya madawa ya kulevya.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti katika kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka 2022/23 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Mjini Dodoma.

 “Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za kulevya, itaendelea kushirikiana na Wizara nyingine katika kuona namna nzuri ya kuandaa maudhui ya mtandaoni ili kuelimisha vijana kuhusu athari ya dawa za kulevya kama ambavyo Tume ya Kudhibiti   UKIMWI inavyofanya”.

Tupo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo imetoa maelekezo mahususi kuhusu kushughulikia dawa za kulevya, Amesema Naibu Waziri.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya Dkt. Alice Karungi ameipongeza serikali kwa kiwango cha fedha kilichopelekwa kwenye Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinachoendana na kwa kiwango cha fedha kilichokadiriwa wakati wa bajeti.

“Zoezi la kuwasaidia vijana wetu waliopata nafuu ya uraibu wa dawa za kulevya kwa kupatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi; kama sehemu ya jitihada za Mamlaka, katika  kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, liwe endelevu”.

Naye Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila amesema mamlaka imeweka msukumo mkubwa katika kukabiliana dawa zinazotoka nje ya nchi, Heroin, Cocaine na Methamphetamine.

 “Bangi imekuwa ikitumika kwa wingi kwa sababu inapatikana kwa bei nafuu na zinalimwa katika maeneo ya kujificha sana”.

Tamaa ya kupata fedha imekuwa ikichochea wananchi kulima bangi kulinganisha na mazao mengine hata hivyo udhibiti unaendelea.

“Tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Klimo waweze kushauri Mwananchi badala ya kulima bangi walime zao gani ambalo litawasaidia kupata fedha nyingi.”

Naye Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Dkt. Leonard Maboko ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya UKIMWI na Dawa za Kulevya kwamba fedha za Global Fund zitatoka robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/23.

 

“Mradi wa Umoja wa Mataifa wa Kuhusisha UKIMWI kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi 2,132,610,000.00, tayari kiasi cha shilingi 1,090,849,597.00 zimepokelewa. Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) katika bajeti 2022/23 iliyoidhinishwa ya shilingi 1,880,000,000.00 fedha za ndani, tayari kiasi cha shilingi 469,992,000.00  zimepokelewa mwishoni mwa mwezi Septemba 2022 hivyo zitatumika katika robo ya pili ya mwaka (Oktoba – Desemba, 2022)”.

Naye Mhe. Asia Halamga ameomba serikali kubadili baadhi ya Sheria zinazowazuia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya iweze kufanya kazi zake kikamilifu.

“Fedha tunazotumia kutibu ni vyema tukazitumia kudhibiti ili tusiendelee kuumiza taifa na hasa vijana”.

 

MKUU WA WILAYA KOROGWE BASILLA: ELIMU YA MAAFA IPEWE KIPAUMBELE


 Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanukuzi ameziasa Kamati za Maafa kuendelea kutoa elimu katika maeneo yao ili kujiandaa na kukabili maafa pindi yanapotokea na kuweka mkazo katika maafa yanayoathiri maeneo ya Wilaya hiyo.

 

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina ya siku 5 ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii kwa wajumbe wa Kamati za Maafa Wilaya hiyo iliyohusisha Kata sita zinazoathiriwa na maafa ikiwemo Magoma, Foroforo, Kalalani, Dindira, Bungu na Kizara zilizopo Korogwe mkoani Tanga.

 

Semina hiyo iliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IMO) imewafikia zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika Kata hizo ikiwemo Viongozi wa dini, Wazee Mashughuli pamoja na Watendaji wa Kata na Vijiji wa Wilaya hiyo.

 

Mkuu wa Wilaya aliwaasa wajumbe hao kuendeelea kuwa mabalozi wazuri katika kutoa elimu juu ya kujikinga na madhara yatokanayo na maafa ili kiuendelea kuwa na jamii iliyosalama

 

“Yatumieni mafunzo haya kama nyenzo muhimu katika maeneo yenu kuhakikisha mnajilinda na maafa yanayoweza kujitiokeza katika maeneo yenu, kukabili maafa kunahitaji kujitolea kwa mtu mmoja mmoja ili kuwa na mazingira salama,”alisisitiza Mhe. Mwanukuzi

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado akieleza lengo la semina hiyo ni kutoa elimu ya masuala ya maafa kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi Kijiji ikiwa ni moja ya jukumu la idara hiyo ili kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa.

 

“Idara ya Menejimenti ya maafa imekuwa ikiendesha semina hizo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendelea kuwajengea uelewa wananchi kuhusu mzingo mzima wa menejimenti ya maafa unaohusisha kuzuia, kujiandaa kukabili, kukabiliana, kurejesha hali pindi maafa yanapotokea katika maeneo yao,”alisema Kanali Masalamado.

 

Aliongezea kuwa miongoni mwa maeneo yaliyofikiwa ni pamoja  na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwa kuzingatia imekuwa ikikabiliwa na maafa mbalimbali yakiwemo ya uhalibifu wa mazao unaosababishwa na uvamizi wa wanyamapori(tembo), ukame, pamoja na mafuriko.

 

Naye Afisa Afya kutoka Wilaya ya Korogwe Bw. Majaliwa Tumaini alieleza mada kuhusu ugonjwa wa ebola aliiasa jamii kuona umuhimu wa kujilinda na kulinda wengine kwa kuzingatia madhara yatokanayo na ugonjwa huu.

 

“Lazima tuchukue tahadhari zote muhimu kwani ugonjwa huu upo nchi jirani, kila mmoja awe mlinzi wa wenzake huku tukifuatilia maelekezo yanayotolewa na Wizara husika na wataalam wa afya,” alieleza

Tuesday, October 11, 2022

WADAU WA MAENDELEO WAHIMIZWA KUCHANGIA VIFAA VYA MISAADA YA KIBINADAMU WAKATI WA MAAFA.

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewahimiza wadau wa maendeleo na watu binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuchangia vifaa vya misaada ya kibinadamu wakati wa maafa.

Mhe. Ummy aliyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua ghala la kuhifadhi vifaa vya misaada ya kibinadamu wakati wa maafa Kanda ya Kaskazini  lililopo maeneo ya Chekereni, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro.

Alisema uungwaji mkono wa serikali kutoka kwa wadau unasadia wananchi kufikiwa na huduma kwa haraka kutokana na majanga yaliyojitokeza ambayo husabababisha madhara kama vifo, ulemavu wa kudumu, mali kuharibika pamoja na miundombinu.

“Nitoe wito kwa wadau na watu mbalimbali ambao wanaguswa kushirikiana na serikali kwa kutoa vifaa wafanye hivyo pengine ngaji ya Wilaya, Mkoa na hata kijiji ili tuwe navyo vya kutosha ili yanapotokea tunatoa msaada kwa haraka,” alihimiza Mhe. Ummy.

Pia Mhe. Ummy alisisitiza utunzwaji wa magahala hayo hatua itakayosaidia vifaa hivyo kudumu kwa muda mrefu na kuwa tayari kutumika pindi vinapohitajika katika maeneo yenye maafa.

Aidha aliupongeza uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa utayari wa kutoa msaada wa kibinadamu kwa wananchi wanaokumbwa na maafa kwa lengo la kuwasaidia kurejea katika hali yao ya awali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Kilimanjaro ambaye ni Afisa Mifugo katika Mkoa huo  Bwa. James Shao alisema ghala la Kanda ya Kasikazini linahudumia Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

 

Friday, October 7, 2022

KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA ZATAKIWA KUJA NA MIPANGO KUSAIDIA MAENEO YATAKAYOPATA KIWANGO KIDOGO CHA MVUA ZA VULI

 


Kamati za usimamizi wa Maafa zatakiwa kuandaa mipango ya dharura itakayoelekeza hatua za kuchukua kwa kila taasisi na wananchi kwenye maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambapo, mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mjini Dodoma. taarifa ya utabiri huo inahusu maeneo ya  Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. 

“kutakuwa na upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo mengi unaoweza kuathiri ukuaji wa mazao, kusababisha uwepo wa visumbufu vya mazao na magonjwa,” amesema Waziri.

Kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua               hususani katika maeneo mengi ya yanayotegemea mvua za Vuli hivyo kusababisha upungufu wa maji kwa matumizi mbalimbali.

“Mlipuko wa magonjwa unaweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama.”

Waziri ametoa rai kwa kamati za usimamizi wa Maafa katika ngazi zote kushirikisha wadau wa maafa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo ikiwemo kupanda mazao yanayokomaa mapema na kuvuna maji.

“Kamati za usimamizi wa maafa, zichukue hatua za kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na Kushirikiana na sekta za maji na umeme kuweka mipango yao ya tahadhari ili kuhakikisha kuwa usumbufu unaotokana na ukosefu wa maji na nishati unapewa ufumbuzi mapema”.

Waziri amehimiza Kuimarisha udhibiti wa maeneo ya hifadhi za wanyama pori ikiwa ni pamoja na kuzuia muingiliano  kadri inavyowezekana; sambamba na kuainisha na kuandaa rasilimali za usimamizi wa maafa na kila sekta kushiriki kikamilifu katika eneo lake.

Sunday, October 2, 2022

WAZAZI WAASWA KUENDELEA KUSIMAMIA MALEZI YA VIJANA


Wazazi wahimizwa kusimamia misingi ya malezi kwa vijana wanapohitimu kidato cha nne kwa kuhakikisha vijana hao wanaendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita ili kuendelea kuwafuatilia kwa ukaribu mienendo ya tabia zao.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika mahafali ya nane ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Catherine iliyopo Lushoto Tanga.

Elimu hii inaushindani mkubwa katika kazi, msome kwa ajili ya uelewa na msome kwa ajili ya kuja kushiriki udahili katika ushindani wa kupata kazi na uwezo wa kujitegemea.

“Katika kipindi hiki ambacho wanasubiria matokeo, wazazi msiwape uhuru vijana kwa sababu umri walionao bado ni mdogo na bado wanahitaji malezi. Wekeni utaratibu wa kutumia simu janja katika kipindi hiki ili waweze kuweka mkazo katika kutimiza malengo yao,” alisema Waziri.

Sitegemei kumwona mmoja wa wahitimu hawa akipotea katika maadili mabovu na matumizi ya madawa ya kulevya bali ni matumaini yangu wote mtasonga mbele na kufikia ngazi za juu kabisa za taaluma. Hii ni kwa manufaa yenu binafsi na taifa letu kwasababu bado tuna uhitaji mkubwa wa wataalamu na ninyi ni sehemu ya wataalamu tunaowahitaji hapo baadaye.

Naye Sr. Fokas Mjema, Msaidizi wa Mama Mkuu wa Shirika la Masister wa Usambara na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Catherine, amewashukuru walimu na wanafunzi kwa kufanya mitihani ya majaribio kwa bidii na ungalifu na kuwa makini.

“Wahitimu wetu wa kidato cha nne wanafunzi 65; wameandaliwa vizuri, tunategemea kutokana na maandalizi wapate ufaulu wa daraja la kwanza na ufaulu wa daraja la pili”

Akieleza namna shule ya Mtakatifu Catherine ilivyojiaanda na Mtihani wa Taifa Mwalimu wa Taalumu Nyandwi Mathias Marko amesema; shule inautaratibu wa kufanya mitihani ya majaribio, mitihani ya majaribio kwa vitendo, mitihani ya mwaka, mitihani ya kila wiki, mitihani ya ushirikano na shule nyingine na mazoezi.

“Tunatumia mitihani hiyo kufanya tathimini kwa kuangalia udhaifu ili kuwasogeza sehemu inayostahili,” alisema Mwalimu wa Taaluma.

Akitoa nasaha kwa niaba ya wazazi wengine, Dkt. Wambuka Rangi ametoa rai kwa wanafunzi kuendelea kuwa wachamungu ili kuepukana na matendo maovu ambayo yanapoteza ndoto hasa za watoto wa kike.

“Tunaomba muwe waadilifu na wasikivu kwa wazazi mtakapokuwa nyumbani, ilimuweze kufanikiwa katika maisha yenu ya baadae”