NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi amesema,
jitihada za pamoja kati ya Serikali, wadau mbalimbali nchini wakiwemo wananchi
ni muhimu katika kutokomeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini.
Mheshimiwa Katambi ameyasema
hayo Novemba 28, 2022 katika Ukumbi wa Sea View Beach Resort mkoani Lindi
wakati akifungua Kongamano la Kisayansi katika Wiki ya kuelekea Kilele cha
Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.
"Napenda kuwakumbusha
kuwa pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika mapambano dhidi ya UKIMWI
nchini ambapo idadi ya maambukizi mapya ya VVU pamoja na vifo vinavyotokana na
UKIMWI kupungua sana na idadi ya watu wanaoishi na VVU kupata tiba.
"Bado tunayo maeneo
ambayo juhudi zaidi zinahitajika. Maeneo haya ni pamoja na kuzuia maambukizi ya
VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na tiba kwa watoto chini ya miaka
mitano. Pia kuna baadhi ya makundi yako nyuma katika kufikiwa na huduma za VVU
na UKIMWI kama wanaume,vijana na makundi maalumu yalio katika hatari kubwa ya
maambukizi ya VVU,"amesema Mheshimiwa Katambi.
Pia amesema,kongamano hilo la
kisayansi limekuwa likifanyika kwa miaka mingi toka mwaka 2016 kama sehemu ya
maadhimishio ya kuelekea siku ya UKIMWI duniani.
Kupitia kongamano hili,
jumuiya ya wanasayansi wanapata nafasi ya kuungana na jamii kubwa zaidi katika
kutafakari na kubadilishana mawazo, uzoefu pamoja na mbinu mpya za kisayansi za
kupambana na janga la UKIMWI,
"Hivyo, kongamano la mwaka
huu ni muhimu sana kwa kuwa Dunia pamoja na Taifa letu limeweka muelekeo mpya
wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo kwa pamoja tumeamua kutokomeza
UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
"Ili kutekeleza azima
hiyo Dunia kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia UKIMWI
(UNAIDIS) limeandaa mkakati Mpya wa kuelekea lengo hilo (Global AIDS Strategy
2021-2026). Nasi kama taifa pia tumeandaa mikakati mipya ya Kitaifa na kisekta
(Mkakati wa Taifa wa Sekta zote NMSF V na Mkakati wa Sekta ya Afya HSHSP V) ili
kutekeleza azimio hilo,"amefafanua Mheshimiwa Katambi.
Pia amesema, kongamano hilo
linafanyika chini ya kauli mbiu ya Equalize (Imarisha Usawa) ambapo litatoa
nafasi ya wadau kujadili mbinu mpya na namna bora ya kuendeleza mapambano dhidi
ya UKIMWI katika huo muktadha mpya.
"Nimefahamishwa kuwa
kongamano hili la siku mbili litahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo
wanasayansi, watoa huduma za VVU na UKIMWI, wawakilishi mbalimbali wa jamii
zinazotumia huduma hizo,wasimamizi na wadau wa maendeleo pamoja na wajumbe toka
sekta mbalimbali.
"Inatarajiwa jumla ya
mawasilisho 26 yatatolewa kwa njia ya muhadhara na mengine mengi kama
mchapisho. Mawasilisho yote yamegawanyika katika mada kuu nane. Mgawano huu
utatoa nafasi ya mijadala kuelekezwa katika maeneo makuu ya muitikio wa VVU na
UKIMWI nchini,"amesema Mheshimiwa Katambi.
Wakati huo huo, Mhesshimiwa
Katambi amesema fursa hiyo itakuwa muhimu katika kuweka nguvu mpya kuhakikisha
mafanikio yaliyokwishapatikana mpaka sasa yanaendelezwa na makundi yaliyoachwa
nyuma yanafikiwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi ili kufikia malengo ya
kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
"Ninatambua kwamba katika
makongamano kama haya, huwa kunaweza kuwa na tofauti kubwa ya kiwango cha
uelewa wa mada pamoja na tofauti ya mitizamo. Nina waomba watoa mada kutumia
lugha nyepesi katika kutoa mada zao ili kurahisisha ujumbe kufikia wajumbe na
kupata uelewa wa pamoja na pia kwa wajumbe kuwa wasikivu pia wavumilivu pale
ambapo sayansi inaelekeza mambo ambayo ni tofauti na mitizamo yao.
"Kusikia mada ni jambo
moja na kutekeleza maelekezo ya kisayansi ni jambo tofauti. Ninapenda
kuwashauri kuwa, ili tuweze kufanya mageuzi katika mapambano dhidi ya VVU na
UKIMWI na kupata matokeo chanya, hatuna budi kuzingatia zaidi ushauri wa
kisayansi.
"Ninawaomba wote
tutakapomaliza kongamano hili kila mmoja wetu kupitia asasi yake kufanya
mapitio ya pamoja ya jinsi mada zilizowasilishwa hapa zinaweza kuboresha
utendaji kazi wao na kufanya marekebisho stahiki. Ushirikiano kati ya asasi
zinazotekeleza afua zinazofanana ni fursa muhimu ya kuanza kutekeleza mambo
yale tuliyojifunza katika kingamano hili,"amebainisha Mheshimiwa Katambi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.