Tuesday, December 6, 2022

DKT. GWAJIMA: ELIMU YA LISHE IPEWE KIPAUMBELE

Serikali imesisitiza utoaji wa elimu kwa jamii namna ya kuzingatia masuala ya lishe nchini ili kuwa na Taifa lenye afya bora na kujiletea maendeleo yake.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt.Doroth Gwajima wakati akimwakilisha  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa  wakati wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika uwanja wa shule ya Msingi Mukendo  Wilaya ya Musoma Mkoani Mara.

 

Akizugumza kuhusu Mkutano huo alisema, umewezesha washiriki kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha mwaka wa kwanza (2021/2022) wa utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa Lishe (2021/22 - 2025/26) na kusema kuwa tathmini hizo ni za muhimu kwani ndio kipimo cha kujua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango.

 

Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni“KUONGEZA KASI KATIKA KUBORESHA HALI YA LISHE KWA MAENDELEO YA RASILIMALI WATU NA UCHUMI” .

 

Waziri alisema katika kutekeleza mpango Juishi wa Lishe suala la elimu lina umuhimu wa kipekee kwa kila mmoja ili kufikia malengo.

 

Alifafanua kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaumbele juu ya jamii kupewa elimu ya namna ya kuzingatia lishe bora ili kuweza kuepukana na udumavu kwa watoto na kuwa na afya bora.

 

“Ili kupata matokeo chanya katika kuboresha hali ya lishe nchini ni muhimu kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya lishe. Pamoja na uhamasishaji kufanyika kabla ya mkutano na wakati wa  mkutano huu, natoa rai kwa Taasisi ya Chakula na Lishe na wadau wengine kuhakikisha tunabuni mikakati zaidi ya kufikisha elimu sahihi ya lishe kwa umma ili kusaidia jamii kuelewa changamoto,”Alisisitiza Dkt.  Gwajima

 

Aliekeza  kuwa,  upo  umuhimu  wa  kuwa  na  jitihada za makusudi ili kuhakikisha wadau wa sekta binafsi wanashirikishwa na kuwa na utaratibu mzuri wa kuchangia utekelezaji wa afua za lishe.

 

Aidha, Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuifanya nchi yetu kuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda ambapo alieleza kuwa Maendeleo haya hayawezi kupatikana iwapo hatutaimarisha kasi ya kujenga na kulinda kizazi chenye nguvu, afya njema na uwezo wa kufikiri.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde aliasema Wizara yake itaendelea kutoa kipaumbele katika kutenga fedha nyingi kwenye masuala ya lishe na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuchagiza ongezeko la upatikanaji wa chakula nchini.

 

"Uwekezaji katika kilimo utaleta matokeo chanya katika lishe, lazima tuwekeze katika uzalishaji wa mbegu, huduma za ugani, umwagiliaji na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ili kufikia malengo kama yalivyotarajiwa," alisema Mhe. Mavunde

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alisema kumekuwa na  chagamoto ya ulaji kwa kutozingatia  kauni za lishe bora inayosababisha changamoto za kifya kwa wengi.

“Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha ulaji wa nyama kwa wastani wa mtu mmoja kwa mwaka ni kilo 15 wakati kiwango kinachopendekezwa na FAO kwa mtu mmoja kwa mwaka ni wastani wa kilo 50, upande wa ulaji wa samaki wastani wa kilo nane na nusu kwa mtu mmoja kwa mwaka, kiwango hichi kipo chini kulinganisha kiwango kinachopendekezwa cha kilo 23 kwa mtu mmoja kwa mwaka, aidha ulaji wa mayai na kuku bado si wa kuridhisha," alisisitiza Ulega.

Aidha  wizara imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kuhamasisha hali ya ulaji nchini ambapo wanahamasisha ulaji na utumiaji mazao ya mifugo kwa kushirikina na wadau mbalimbali sambamba na kuongeza uzalishaji nchini.

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.