Serikali imeziagiza Taasisi zote zinazoendelea na ujenzi wa majengo ya Ofisi zao Jijini
Dodoma kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa kuzingatia taratibu zote za
ujenzi ikiwemo ubora, muda, bajeti iliyotengwa na thamani ya fedha ili kuleta
tija inayotarajiwa.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George simbachawene wakati wa hafla ya kukabidhi
Vibali vya Ujenzi wa Ofisi za Taasisi za Serikali Dodoma iliyofanyika katika Ukumbi
wa Hazina mapema.
Waziri Simbachawene
amesema, kila Taasisi ya Serikali ihakikishe inajenga majengo ya Ofisi zake ili
kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamishia Makao makuu yake Dodoma
na kuifanya Dodoma kuwa eneo lenye ufanisi.
“Taasisi zote zilizoelekezwa
kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba niliyoitoa leo zihakikishe zinatekeleza maagizo
hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa
utekelezaji wake,”alisema Mhe.Simbachawene.
Aliongezea kuwa, Mpango huu ni
utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 kama ilivyoainishwa
katika Ibara ya 151 chini ya kifungu (a), (b) na (c) vinavyoielekeza Serikali
kutunga Sheria ya kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi na kuhakikisha
kwamba majengo ya Wizara na Taasisi yanajengwa Dodoma badala ya Dar es Salaam.
Aidha Waziri ameagiza Ofisi ya Katibu Mkuu – Sera,
Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Mamlaka husika kuendelea kuratibu Mpango
wa Serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma pamoja na ujenzi wa miundombinu ya
kiuchumi na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii Dodoma.
Sambamba na hilo, Serikali
imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado
zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli
zao Jijini Dodoma kwa awamu.
“Katika
utekelezaji wa suala hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwamba Taasisi
42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2022/23; Taasisi 36 zitahamia
Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 na Taasisi 19 zitahamia katika mwaka
2024/25 wakati Taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo,
kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.” Alieleza.
Alisisitiza kuwa,
hatua hii itakamilisha sehemu kubwa ya Mpango wa Serikali wa kuhamia Dodoma
ambapo hadi sasa tayari Taasisi 65 zilishahamia Dodoma tangu mwaka 2016 hadi
2022.
Waziri ameziagiza Taasisi nyingine ambazo bado
hazijaanza maandalizi ya ujenzi wa Ofisi za serikali Dodoma ziwasilishe Ofisi
ya Waziri Mkuu Mahitaji ya Viwanja vya ujenzi wa Ofisi za taasisi Dodoma kwa
ajili ya uratibu wa pamojal.
Naye Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule,
ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya kuwezesha
taasisi kuwepo.
“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa kupanga
makao makuu ya serikali yetu yanakuwa ni mji wa kisasa na mji uliopangwa.”alisema
Mhe. Rosemary
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt, John
Jingu akitoa taarifa ya utekelezajia amesema Ofisi ya waziri Mkuu imeidhinisha
vibali 55 kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2018 kati ya hizo taasisi 20
zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na ujenzi na taasisi 19 zimeanza
maandalizi ya ujenzi.
“Majengo haya yanajengwa katika maeneo mbalimbali, na ujenzi huu
unazingatia mpango kabambe wa Jiji la Dodoma.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.