Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amepongeza kampeni maalum ya
kuchangia fedha katika utekelezaji wa afua za masuala ya UKIMWI nchini ya
Kilimanjaro HIV & AIDS Challenge 2023 kwa
kuzingatia mchango wake katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.
Ametoa pongezi hizo
mapema wakati wa hafla ya kuwaaga wapanda Mlima Kilimanjaro na
waendesha baiskeli kuzunguka mlima huo katika lango la Machame Mkoani
Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo kwa mwaka huu.
Mhe. Dkt. Kikwete
alisema kampeni hiyo ina mchango mkubwa katika kufikia Kampeni ya Kitaifa ya
kufikia malengo ya SIFURI TATU, yaani Sifuri ya maambukizo mapya ya Virusi vya
UKIMWI, Sifuri ya Unyanyapaa na Ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na Sifuri ya
vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa kuzingatia mchango wa kifedha unaopatikana na
kusaidia utekelezaji wa afua za UKIMWI nchini.
“Kazi iliyofanywa na
ndugu zetu GGM wameonesha njia wanastahili kuungwa mkono, hivyo basi, niziombe
Jumuiya za wafanyabiashara, makampuni na sekta binafsi pamoja na Watanzania
wote kwa ujumla, kuunga mkono kampeni ya Kill Challenge kwa
miaka ijayo,”alisema
Akieleza uzoefu wa
ushiriki wake katika kampeni hiyo alisema ni jambo muhimu kwa kuzingatia
mchango wa tukio hilo katika masuala ya Afua za UKIMWI na linamatokeo mengi
mazuri ikiwemo la kujijenga kiafya, kuchochea hali ya uzalendo kwa nchi yetu
pamoja na kuimarisha mahusiano kati yetu na mataifa mengine kwani wapo
washiriki wa mataifa mengine ikiwemo Afrika Kusini.
“Binafsi ninafarijika
kuendelea kuwa sehemu ya mafanikio haya, kwani leo ninashiriki kwa mara ya tatu
tukio kama hili adhimu ambapo niliwahi kushiriki pia mara ya kwanza tarehe 2
Mei, 2014 na tarehe 21 Julai, 2016, hivyo naipongeza TACAIDS pamoja na Geita
Gold Mining Limited ambao ndio waanzilishi na waratibu wa program hii ya
Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS, ni jambo la kuungwa mkono na
kupongezwa, hongereni sana,”alisema.
Aidha aliipongea
Serikali katika kupambana na maambuzi ya VVU na UKIMWI ambapo kupitia
program hii wadau wanapata fursa kuchangia fedha kwa ajili ya kusaidia jitihada
za Serikali na wananchi katika mapambano haya.
“Kwa namna ya kipekee
kabisa naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyojipanga kuongeza nguvu ya mapambano
haya kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa afua
za masuala ya UKIMWI Nchini.
Alitumia nafasi hiyo
kuwaasa washiriki kutimiza malengo kwa kushikamana, upendo na kuwa na umoja
katika zoezi hilo ili kukamilika kwa namna lilivyokusudiwa.
“Washiriki wote 61
ikiwemo wapanda mlima (Climbers) thelathini na sita na wanaouzunguka kwa
baiskeli ishirini na tano mmeonesha ushujaa wa hali ya juu kwa kujitoa kwenu na
kuwa tayari kupanda mlima na wengine kuendesha baiskeli mmefanya jambo kubwa na
zuri la kuigwa,”.
Aliongezea kuwa,
kushiriki zoezi hili ambalo si jepesi imedhihirisha kuwa bado ipo dhamira ya
dhati miongoni mwa Watanzania na wadau ya kuendeleza mapambano haya, na
yatafanikiwa iwapo pataendelea kuwa na dhamira ya dhati kwa kila mmoja wetu na
ushirikiano wa pamoja kufikia ushindi unaoutarajia.
Kwa upande wake Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu
Mhe. Ummy Nderiananga alipongeza namna zoezi lilivyoratibiwa na kutoa wito kwa
washiriki wote kuendelea kujitoa kwa kadiri inavyobidi huku akimshukuru Rais
Mtaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa program hiyo na
kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano na wadau mbalimbali wanaoshughulika na afua
za masuala ya VVU na UKIMWI nchini.
Awali akieleza kuhusu
kampeni hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini Dkt. Jerome
Kamwela alisema Tanzania imeendelea kuwa na mikakati madhubuti katika mapambano
dhidi ya VVU na UKIMWI na kueleza takwimu zinaonesha maambukizi yamepungua
kufikia asilimia 4.7 ambapo ni ishara kuwa jamii imekuwa na mwamko na uelewa
mpana kuhusu masuala haya.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.