Kamati za maafa Ngazi ya Mkoa zajengewa uwezo juu Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha
utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na
Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na
Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali ilianza kutekeleza hatua
za kuzuia madhara haya toka mwezi Julai 2023 wakati taarifa ya awali ya dalili
za uwezekano wa uwepo wa El Nino ilipotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania.
Kikao kazi hichi kinafanyika kwa siku mbili kuanzia
tarehe 25 hadi 26 septemba, 2023 na kuhusisha wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa
Maafa ngazi ya Mkoa wakiwemo; Wakuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Mkoa,
Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyekiti wa Halmashauri pamoja na washiriki kutoka
washiriki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, wawezeshaji kutoka Idara ya
Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi
la Polisi Tanzania, TMA na DarMAERT Pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali
na Viongzozi wa dini.
Alisema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa mikoa 14
inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza,
Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es
Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini mwa mkoa wa
Morogoro.
“Kikao kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa
Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo
imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au
Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na
kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha
hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.” alisisitiza Mhe. Nderiananga.
Naibu Waziri aliongezea kuwa, kazi hiyo imezingatia
uwajibikaji wa pamoja ambapo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshirikiana na Wizara za
kisekta na Taasisi za Serikali na Wadau kuendelea kuimarisha hatua ambazo
zinaendelea kuchukuliwa na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Mikoa
husika.
Ametumia nafasi hiyo kuzikumbusha kamati za maafa zote
kuendelea kujiandaa na kukabili maafa nchini kwa kuimarisha mifumo ya utendaji,
rasilimali zilizopo huku wakitambua masuala ya menejimenti ya maafa ni jukumu
la kila mmoja hivyo upo umuhimu wa kuunganisha nguvu ya pamoja.
“Ni jukumu letu sote katika nafasi zetu kama wajumbe
wa Kamati za Usimamizi wa Maafa kutekeleza kimamilifu hatua za kuchukua katika
sekta zenu kwa kuzingatia kuwa madhara yanaweza kuongezeka endapo hatua stahiki
hazitachukuliwa kwa wakati. Natarajia kuwa baada ya kikao kazi cha leo, Kamati
hasa ngazi ya Halmashauri zote za Mkoa zitaimarisha utekelezaji wa hatua za
kuzuia madhara ili kuhakikisha tunaokoa maisha na mali kwa ustahimilivu wa
taifa,”alisema.
Alizikumbusha Taasisi zinazohusika kuendelea kuwa
mstari wa mbele wakati wa tukio la maafa zinapaswa kujiandaa kikamilifu kwa
kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa
utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua
hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.
“Taasisi hizo ni pamoja na zile zinazohusika na huduma
ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma
zingine za kijamii. Aidha, taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi
pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji
zinakumbushwa kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi
haziathiriki wakati wa maafa. Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi
zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa
ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii”,Alisisitiza
Sambamba na hilo aliwaeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu
ili kuhakikisha juhudi zinazochukuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha uchumi na huduma za
kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa. Ni
dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa zitachangia katika juhudi zake katika
kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali pamoja na maelekezo ya
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 kwa manufaa makubwa kwa
wananchi na tija iliyokusudiwa.
“Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 kuhusu masuala ya Menejimenti ya maafa nchini
kifungu cha 107, kinaeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha
Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha Serikali inaendelea kusimamia kikamilifu
vyombo vinavyoshughulika na maafa kuwa na mpango wa utayari wa kuzuia,
kujiandaa, kukabili na kurejesha hali haraka pindi maafa yanapotokea kwa
kuchukua hatua mbalimbali” alibainisha Mhe. Nderiananga.
Kwa upande wake Mkuu
wa wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro ameeleza kuwa mkoa umejiandaa katika kukabiliana na maafa na kueleza
wataendelea kutoa elimu kwa umma juu ya uwepo wa mvua hizo huku akitahadharisha
wakazi wa Malinyi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ni maeneo
yanayoathiriwa na maafa ya mvua mara kwa mara.
Naye, Mkuu wa Wilaya
ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa ametahadharisha wakazi wa maeneo yanayoathiriwa
kwa wingi, kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam ikiwemo kuhama maeneo
hatarishi na kutotupa taka zinazosababisha kuziba kwa mifereji ya maji na
kuimarisha kingo zote.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.