Serikali imezitaka
taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi kuimarisha mifumo
mbalimbali kama ya usafiri, mawasiliano, nishati na maji ili
kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama
wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miundo mbinu ya mito mikubwa
na mifereji ikiwa ni hatua ya kujiandaa na mvua za El Nino zinazotarajiwa
kunyesha mapema mwaka huu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Kamati za
Usimamizi wa Maafa ngazi ya Mkoa katika Kuzuia na Kupunguza madhara ya El Nino
kilichofanyika Jijini Dar es salaam.
Mhe. Jenista amesema
matukio ya maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii
ambapo Serikali za Mitaa, kuanzia Kitongoji, Mtaa au Kijiji na Jiji, Manispaa,
Mji na Wilaya zinawajibika moja kwa moja.
“Hatua za kuzuia
madhara zinatekelezwa zaidi na viongozi na wataalam kwa kushirikiana na
wadau na wananchi katika maeneo haya. Tumekutana leo kukumbushana wajibu
muhimu mlio nao kwa kila mmoja kuwajibika katika eneo lake ili kuokoa
maisha na kulinda mali za wananchi. Tukumbuke kuwa Mkoa unaingia kusaidia
juhudi za Halmashauri husika pamoja na kushirikisha uratibu wa msaada
kutoka ngazi ya Taifa endapo madhara yatakuwa yamezidi uwezo wa
rasilimali katika eneo husika.
Pia
amewasisitiza wananchi kila mmoja kuchukua hatua katika eneo lake,
akisema mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi
yenye jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali
za jamii yetu kutokana na matukio ya maafa.
Katika hatua nyingine
amezitaka taasisi zinazohusika kuwa mstari wa mbele kuchukua tahadhari na
kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na
kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa
dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.
“Historia inaonesha
madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El Nino
utakaosababisha mvua kubwa ni pamoja na Mafuriko kuharibu miundombinu
mbalimbali, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali,
Maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na
shughuli zingine hususani uchimbaji madini, Magonjwa ya milipuko kwa binadamu
na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea,” Amesema Mhe. Jenista.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Dar es salaam,Albert Chalamila ameahidi kutekeleza maagizo yalyotolewa na
Waziri huyo katika kuhakikisha miundo mbinu yote ya maji pamoja na maeneo hatarishi
yanafanyiwa matengenezo ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza
wakati wa mvua za El Nino hivyo akawahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa
wakandarasi watakapofika katika maeneo yao kufanya maboresho hayo.
“Hakikisha
tunajidhatiti kutunza mazingira yetu na miundo mbinu hasa hii ya mito tunaweza
kupata kipindu pindu na jambo tunalokabiliana nalo kwa sasa hapa Tabata ni
wimbi la vibaka lakini tumeandaa timu za ulinzi kupitia ulinzi shirikishi
wa Sungusungu,”Ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo.
Akitoa maoni yake
mkazi wa Mji Mpya-Mnyamani ameiomba Serikali kuhakikisha inaweka miundo mbinu
imara ya vivuko na barabara katika maeneo ya mitaa ili kusaidia wananchi kuvuka
na kupata huduma wakati wa maafa.
Aidha Mkazi wa Tabata
Bw. Shelemia Gwassy ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu na Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara ya kushitukiza katika maeneo ya Tabata
na kukagua mito inayopitisha maji ikiwemo Mto Msimbazi, Mto Mpiji, Mto Ng’ombe
na Mfereji wa Jangwani huku akiiomba kuweka utaratibu mzuri wa uzoaji taka
katika makazi ya wananchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.