Tuesday, September 26, 2023

WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA EL NINO.

 


Serikali imezitaka taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi  kuimarisha mifumo mbalimbali kama ya  usafiri, mawasiliano, nishati na maji  ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miundo mbinu ya mito mikubwa na mifereji ikiwa ni hatua ya kujiandaa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha mapema mwaka huu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Kamati za Usimamizi wa Maafa ngazi ya Mkoa katika Kuzuia na Kupunguza madhara ya El Nino kilichofanyika Jijini Dar es salaam.

Mhe. Jenista amesema  matukio ya maafa yanatokea na kusababisha madhara katika ngazi ya jamii ambapo Serikali za Mitaa, kuanzia Kitongoji, Mtaa au Kijiji na Jiji, Manispaa, Mji na Wilaya zinawajibika moja kwa moja.

“Hatua za kuzuia madhara zinatekelezwa zaidi na viongozi na wataalam kwa  kushirikiana na wadau na wananchi katika maeneo haya. Tumekutana leo  kukumbushana wajibu muhimu mlio nao kwa kila mmoja kuwajibika katika  eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi. Tukumbuke kuwa  Mkoa unaingia kusaidia juhudi za Halmashauri husika pamoja na  kushirikisha uratibu wa msaada kutoka ngazi ya Taifa endapo madhara  yatakuwa yamezidi uwezo wa rasilimali katika eneo husika.

Pia  amewasisitiza wananchi  kila mmoja kuchukua hatua katika eneo lake, akisema  mfumo wa Serikali umezingatia wajibu wa sekta na taasisi yenye  jukumu kisera na kisheria kuchukua hatua ili kuokoa maisha na mali za jamii  yetu kutokana na matukio ya maafa.

Katika hatua nyingine amezitaka taasisi zinazohusika kuwa mstari wa mbele  kuchukua tahadhari na kujiandaa  kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.

“Historia inaonesha madhara yanayoweza kutokea katika sekta kutokana na uwepo wa El Nino utakaosababisha mvua kubwa ni pamoja na  Mafuriko kuharibu miundombinu mbalimbali, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali,  Maporomoko ya ardhi kuathiri makazi, mazingira, mashamba, usafiri na shughuli zingine hususani uchimbaji madini, Magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama na wadudu waharibifu wa mazao na mimea,” Amesema Mhe. Jenista.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,Albert Chalamila ameahidi kutekeleza maagizo yalyotolewa na Waziri huyo katika kuhakikisha miundo mbinu yote ya maji pamoja na maeneo hatarishi yanafanyiwa matengenezo ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Nino hivyo akawahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa wakandarasi watakapofika katika maeneo yao kufanya maboresho hayo.

“Hakikisha tunajidhatiti kutunza mazingira yetu na miundo mbinu hasa hii ya mito tunaweza kupata kipindu pindu na jambo tunalokabiliana nalo kwa sasa hapa Tabata ni wimbi la vibaka lakini tumeandaa timu  za ulinzi kupitia ulinzi shirikishi wa Sungusungu,”Ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo.

Akitoa maoni yake mkazi wa Mji Mpya-Mnyamani ameiomba Serikali kuhakikisha inaweka miundo mbinu imara ya vivuko na barabara katika maeneo ya mitaa ili kusaidia wananchi kuvuka na kupata huduma wakati wa maafa.

Aidha Mkazi wa Tabata Bw. Shelemia Gwassy ameishukuru Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa kwa kufanya ziara ya kushitukiza katika maeneo ya Tabata na kukagua mito inayopitisha maji ikiwemo Mto Msimbazi, Mto Mpiji, Mto Ng’ombe na Mfereji wa Jangwani huku akiiomba kuweka utaratibu mzuri wa uzoaji taka katika makazi ya wananchi.

 


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.