Wajumbe
wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa,
wakiongozwa na Mwenyekiti Fadhili Maganya, wameipongeza Serikali ya Awamu ya
Sita kwa ujenzi wa mji wa Serikali, Mtumba.
Bw.
Maganya ametoa pongezi hizo alipoongoza ujumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya
Wazazi ya CCM Taifa kutembelea Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
"Tunaona
namna Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wetu Dkt. Samia
Suluhu Hassan inavyotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ujenzi wa Mji huu
wa kisasa ambao sio tuu watu kuja kufanya kazi bali hata kukuza utalii wa ndani" amesema Bw. Maganya.
Aidha,
Bw. Maganya ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara, majengo ya kisasa na matumizi
ya samani zilizotengenezwa ndani ya nchi vinaonesha thamani ya fedha
zinazotolewa na Serikali na kuahidi kushirikiana na Serikali katika upandaji wa
miti ili kuwa sehemu ya kutimiza malengo ya utunzaji wa mazingira katika mji
huo.
Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema,
Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) itaendelea na uratibu wa ujenzi wa mji wa Serikali
kwa kiwango kinachohitajika na amewashukuru Jumuiya ya Wazazi Taifa kwa kutenga muda wa kutembelea Mji wa Serikali
ili kujionea kwa macho utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akiwakaribisha
Wajumbe hao, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Paul Sangawe amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu
inapokea wageni mbalimbali wanaotaka kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na
kuufanya Mji huo kuwa kivutio cha utalii.
