Friday, August 23, 2024

RAIS SAMIA AWAHAKIKISHIA WAKAZI WA TARAFA YA NGORONGORO KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Tafara ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro kuwa shughuli zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,  unaotarajiwa kufanyika Novemba, 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 zitaendelea kama ilivyokuwa awali kwa kuzingatia taratibu na mipaka ya Vijiji na Vitongoji iliyokuwepo awali kwenye maeneo yao.

Maagizo hayo yametolewa  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Oloirobi, ambapo amewataka wananchi hao kuondoa hofu na wasiwasi badala yake kuendelea kuishi kwenye maeneo yao kwa amani, kwa kuwa nchi yao ya Tanzania ni Nchi ya amani na utulivu, inayowajali wananchi wake, kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na usawa.

Akiwasilisha ujumbe huo, amesema kuwa, Mhe. Rais amepokea kero na malalamiko kutoka kwa Viongozi na Vyombo vya habari na kuwaagiza askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutowanyanyasa wananchi pamoja na kuheshimu Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo, kwani Mhe. Rais Samia bado anatambua uwepo wa Serikali za Vijiji na Vitongoji vya maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro.

Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda licha  ya kuwashukuru wananchi kwa uvumilivu na imani yao kwa Serikali, amemuhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atasimamia maelekezo yote yaliyotolewa kwake, akiahidi pia kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizokuwa zimesimama ama kusuasua hasa katika Sekta ya Afya na Elimu zinarejea katika ubora wake na kwa viwango vinavyohitajika.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania CP Awadh Juma Haji pamoja na Viongozi wengine wa Serikali na wa Chama Cha Mapinduzi CCM.

 

Read More

Tuesday, August 20, 2024

WAZIRI MHAGAMA AKABIDHI OFISI KWA WAZIRI LUKUVI


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi katika maeneo ambayo atahitaji kupata taarifa za ziada wakati wa kuratibu shughuli za serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu.

Mhe. Jenista amesema hayo, Jijini Dodoma wakati wa makabidhiano ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) kwa Mhe. William Lukuvi aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.

Aidha, Waziri Mhagama amewashuruku watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu pamoja na Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano waliotoa wakati alipokuwa katika Ofisi hiyo.

“Naomba niwashukuru kwa dhati Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano Mkubwa mlionipa, Watumishi wa ofisi hizi wako tayari kufanya kazi kwa moyo na kukupa ushirikiano ili kuhakikisha kwamba malengo yale tuliojiwekea ndani ya serikali yanatekelezwa”

“Tumefanya kazi usiku na mchana kama ni uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ni pamoja na watumishi waliopo kwenye Ofisi hii katika uratibu wa shughuli za serikali,” alibainisha Waziri Mhagama.

 Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema alikabidhi Ofisi hiyo kwa Waziri Mhagama 2014 na kurudi Mwaka 2024 hivyo amekaa nje ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9) na kabla alishawahi kuitumikia kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9).

“Nimeondoka 2014 na kurudi 2024 na kukabidhiwa Ofisi na Waziri niliyemkabidhi wakati huo ambaye ni Waziri Mhagama, aidha nimefanya kazi kwa karibu na Mhe. Mhagama wakati nikiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Mhe Mhagama akiwa Katibu wa Chama Bungeni hivyo ni Mapenzi ya Mungu tumekutanishwa tena watu walewale tunaofahamiana, niwahakikishie tutaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu na Watumishi wote ili kuhakikisha kwamba tunafanya kazi zetu vizuri,” alisema waziri Lukuvi.

 Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewapongeza Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwa nafasi walizopewa.

 “Sisi watumishi wenu tunapenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza majukumu yetu lakini kuwatumikia wananchi wa Tanzania,” alisema Katibu Mkuu.

Read More

NAIBU WAZIRI UMMY: USHIRIKIANO DHIDI YA MAPAMBANO YA DAWA ZA KULEVYA KUENDELEZWA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema, katika kuhakikisha tatizo la Dawa za Kulevya linatokomea nchini Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar wataendeleza ushirikiano katika mapambano hayo.

 Mhe. Ummy ameyasema hayo Jijini Dar Es Salaam wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi la Kusimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar na ujumbe kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) kwa lengo la kutembelea na kujifunza masuala mbalimbali ya namna ambavyo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inavyofanya kazi.

 “Nikuhakikishie Mwenyekiti tutaendelea kudumisha mashirikiano yetu kati ya Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar pamoja na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Wizara zote kuhakikisha kwamba tunaboresha mahusiano yetu baina yetu kwaajii ya kufanya kazi hii nzuri ambayo baadae yanamalipo mbele ya Mwenyezi Mungu kwasababu kazi hii siyo yetu peke yetu lakini pia kwa nafasi zetu tuendelee kuwajibika na kufanya kazi zetu” alisema Naibu Waziri Ummy.

 Sambamba na hayo Mhe. Ummy amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa kuendelea kuziwezesha Mamlaka zote mbili katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya nchini.

 “Niwapongeze Viongozi wetu ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi Zanzibar Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa Juhudi za kuhakikisha Mamlaka zote zinapata fedha pamoja na Rasilimali zingine kwa ajili ya kuimarisha mapambano haya ya Dawa za Kulevya” aliongeza Naibu Waziri Ummy.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi la Kusimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar Mhe. Machano Othman Said amesema, kutokana na mabadiliko ya maendeleo yaliyopo Bara kamati iliamua kuja kujifunza na kupata uzoefu wa namna Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) inavyofanya kazi kwa ajili ya kutokomeza suala la Dawa za Kulevya.

 “Mheshimiwa Naibu Waziri sisi tunakuja sana Bara na tumeona mabadiliko ya maendeleo ambayo yanayofanywa na Dkt. Samia lakini na ninyi mnakuja Zanzibar na mnaona mabadiliko makubwa ya maendeleo yanayofanywa chini ya Dkt. Hussein Mwinyi sasa leo kamati yangu imeamua ije kuangalia wenzetu wanafanya kazi vipi Chini ya Mamlaka”

 “Sisi Zanzibar Kanali Nassor na wenzake wanajitahidi sana kwa sababu miaka minne au mitano nyuma suala la Dawa za Kulevya Zanzibar lilikuwa halipewi uzito mkubwa tulikuwa tunakitu kinaitwa tume lakini kwa sasa ninafurahi kuwa ripoti tunazopata kupitia Kanali Nassor na timu yake kuwa kuna mahusiano mazuri ya kazi na hicho ndicho kilichotufanya tuje kujifunza namna mamlaka inavyofanya kazi” alibainisha Mhe. Machano

 Kamati ya Baraza la Wawakilishi linalosimamia Ofisi ya Viongozi Wakuu Zanzibar imefanya ziara hiyo ya kikazi ya kutembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa namna Mamlaka hiyo inavyofanya kazi zake.

 

Read More

Friday, August 16, 2024

NAIBU WAZIRI UMMY, APOKEA JEDWALI LA UCHAMBUZI LA SHERIA NDOGO

 


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga amepokea Jendwali la Uchambuzi la Sheria Ndogo za Mwaka 2024 katika Mkutano wa Kumi na Tano, Kikao cha sita cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zimewasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo Mhe. Ramadhan Suleimani Ramadhan.

Tukio hilo limefanyika katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma Leo ambapo amesema mafanikio ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) yanatokana na ushirikiano ambao umekuwa ukitolewa na Kamati ya Bunge ya Sheria ndogo.

“Naomba niwahakikishie kamati; nimepokea jedwali hili na tutawasilisha kwa Wizara zinazohusika ili zije zilete majibu, naomba tuendele kupata ushirikiano wakati wizara hizo zitakapokuja kuwasilisha,” alisema Naibu Waziri Ummy.

Read More

Sunday, August 4, 2024

WAZIRI MHAGAMA, “WANANCHI JITOKEZENI KUSHIRIKI UCHAGUZI”

 


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa Wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuhakiki kumbukumbu zao katika Daftari la kudumu la Mpiga Kura.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati alipomuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, leo katika ibada ya shukrani ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Mariamu Lituhi - wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma.

Amewaomba wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa kwa yeyote mwenye sifa za kushirikina na wananchi kuongoza, kutosita kuomba kuchaguliwa.

Waziri amesema, “tuendelee kuiweka nchi yetu kwenye maombi, tumlilie Mungu tuvuke salama kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na tuvuke salama kwenye Uchaguzi Mkuu ili Tanzania iendelee kubaki kuwa kisiwa cha Amani.”

Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa Kanisa Anglikana Tanzania katika Maendeleo ya Taifa letu Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.

Aidha Waziri Mhagama ametumia tafakari ya ujumbe wa Mungu kupitia kinywa cha Nabii Hagai sura ya kwanza, aya ya nane (Hagai 1:8) aliposema, “Sasa, basi, nendeni milimani mkalete miti, mlijenge upya hilo hekalu, nipate kulifurahia na kutukuzwa”.

Awali katika taarifa ya risala iliyosomwa na Bi, Shukrani  Eliya Kilumbo alisema ujenzi wa kanisa ulianza Mwaka 2011 na mpaka sasa kimetumika kiasi cha Millioni 84 na inakadiriwa kiasi cha shilingi milioni 150 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mt. Mariamu.

Tunashukuru taaisisi mbalimbali na watu wote ambao wako hapa kwa kazi hii kubwa ya kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu aliowaagiza kupitia ujumbe wa Mtume Paulo kwa wafilipi 4,8;9

Katika ibada hiyo ya shukrani kiasi cha Milioni 52,300,000 kilikusanywa ikiwemo fedha taslimu na ahadi zitakazosaidia katika ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mt, Mariamu Lituhi katika wilaya ya Nyasa.

 

Read More