Waziri wa Afya Mhe. Jenista
Mhagama ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi katika maeneo ambayo atahitaji
kupata taarifa za ziada wakati wa kuratibu shughuli za serikali chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu.
Mhe. Jenista amesema hayo, Jijini
Dodoma wakati wa makabidhiano ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu)
kwa Mhe. William Lukuvi aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.
Aidha, Waziri Mhagama
amewashuruku watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),
Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu pamoja na Watumishi wa Ofisi Binafsi
ya Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano waliotoa wakati alipokuwa katika Ofisi
hiyo.
“Naomba niwashukuru kwa dhati
Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri
Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano Mkubwa mlionipa, Watumishi wa ofisi
hizi wako tayari kufanya kazi kwa moyo na kukupa ushirikiano ili kuhakikisha
kwamba malengo yale tuliojiwekea ndani ya serikali yanatekelezwa”
“Tumefanya kazi usiku na
mchana kama ni uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais Mhe. Dkt
Samia Suluhu Hassan ni pamoja na watumishi waliopo kwenye Ofisi hii katika
uratibu wa shughuli za serikali,” alibainisha Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi amesema alikabidhi Ofisi hiyo
kwa Waziri Mhagama 2014 na kurudi Mwaka 2024 hivyo amekaa nje ya Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9) na kabla alishawahi kuitumikia kama Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa (9).
“Nimeondoka 2014 na kurudi
2024 na kukabidhiwa Ofisi na Waziri niliyemkabidhi wakati huo ambaye ni Waziri
Mhagama, aidha nimefanya kazi kwa karibu na Mhe. Mhagama wakati nikiwa Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Mhe Mhagama akiwa Katibu wa Chama Bungeni
hivyo ni Mapenzi ya Mungu tumekutanishwa tena watu walewale tunaofahamiana,
niwahakikishie tutaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu na Watumishi wote ili
kuhakikisha kwamba tunafanya kazi zetu vizuri,” alisema waziri Lukuvi.
Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewapongeza Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kuaminiwa na kuteuliwa kwa nafasi walizopewa.
“Sisi watumishi wenu tunapenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza majukumu yetu lakini kuwatumikia wananchi wa Tanzania,” alisema Katibu Mkuu.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.