Waelimisha rika Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) watakiwa kutumia mbinu mbadala na
zinazokwenda na mazingira ya sasa katika kufikisha elimu ya afya kwa watumishi
wenzao kazini huku wakijitolea kwa uzalendo na weledi ili kuendelea kuwa na mazingira
mazuri ya utendaji wa kazi kwa kuzingatia afya zao.
Hayo yamebainishwa Kaimu
Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Eleuter Kihwele kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim James Yonazi hii leo, wakati
wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa waelimisha rika mahala pa kazi,
yanayofanyika mjini Morogoro.
Kihwele amesema kuwa mafunzo
hayo yanalenga kuwajengea uwezo waelimisha rika katika utoaji wa elimu, hasa
katika kipindi hiki ambapo jamii inakumbwa na ongezeko la magonjwa
yasiyoambukizwa pamoja na changamoto nyingine za kiafya.
“Mafunzo haya yatakuwa na mada
muhimu. Zingatieni ili kuwawezesha watumishi wenzenu kupata uelewa wa kina
kuhusu masuala ya VVU na UKIMWI pamoja na magonjwa yasiyoambukizwa,” alisema
Bw. Kihwele.
Aidha, amepongeza maandalizi
ya mafunzo hayo, akisisitiza kuwa yatatoa mwanga na mwelekeo mpya wa
kuhakikisha Ofisi ya Waziri Mkuu inakuwa mfano wa kuigwa katika kueneza elimu
ya afya kwa watumishi wake.
Kwa mujibu wa Kihwele, mafunzo
kwa waelimisha rika hufanyika kila mwaka ili kutathmini utekelezaji wa mwongozo
uliopo, kubaini changamoto na kuja na mikakati bora ya kudhibiti magonjwa
katika Idara na Vitengo husika.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Sehemu ya Menejimenti ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora;Bi. Mwanaamani Mtoo, ameipongeza Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa kuendeleza utekelezaji wa mwongozo wa waelimisha rika kwa
mafanikio makubwa.
“Sisi kama wasimamizi wa
rasilimali watu, tunawapongeza kwa hatua mliyoifikia. Kuendeleza juhudi hizi ni
hatua muhimu ya kudhibiti maambukizi ya VVU na UKIMWI pamoja na magonjwa
yasiyoambukizwa kazini,” alisema Bi. Mtoo.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge na Uratibu imeendelea kuweka kipaumbele katika afya na ustawi wa
watumishi wake, ikiwemo kutoa mafunzo ya stadi za afya kwa waelimisha rika na
kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko ya kiafya katika maeneo yao ya kazi.
Read More