Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. James Kilabuko amezindua rasmi Mwongozo
wa Kitaifa kwa Watoa Huduma za Maendeleo ya Biashara katika hafla iliyofanyika
kwenye Hoteli ya Four Points by Sheraton, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza hii leo wakati wa
uzinduzi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Naibu Katibu Mkuu
huyo amesema kuwa Mwongozo huo unaweka msingi wa mabadiliko makubwa ambayo
yatawawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati ikiwa ni pamoja na
wafanyabiashara wakubwa kukuza biashara zao na kuchangia kikamilifu kwenye
uchumi wa Taifa.
“Uwepo wa Mwongozo huo
unalenga kuweka viwango, mwelekeo na uratibu wa huduma zinazotolewa kwa
wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini, hivyo umekuja kwa
wakati sahihi na tunaamini utaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa,” alisema
Dkt. Kilabuko.
Aidha alitumia nafasi hiyo
kumpongeza Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya katika
kuhakikisha mazingira ya wafanyabiashara na wawekezaji nchini yanaendelea kuwa
bora.
“Kwa umuhimu wa pekee napenda
kumshukuru kwa dhati, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa jitihada anazofanya katika kufungua uchumi na
kuchochea biashara na uwekezaji nchini.Rais wetu ameboresha mazingira ya
biashara nchini na kuchochea kuanzishwa kwa shughuli za kiuchumi nyingi katika
sekta mbalimbali. Shughuli hizo pia zinahitaji huduma za maendeleo ya biashara
ili kuwa shindani.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wanamanchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng'i
Issa ameleeza kuwa Mwongozo wa Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa Watoa Huduma
za Maendeleo ya Biashara Tanzania unalenga kuboresha utoaji wa huduma za
biashara ikiwa ni pamoja na: ushauri, mafunzo, msaada wa kiufundi, ujuzi,
uatamizi, uhusiano baina ya wafanyabiashara, mawasiliano, na usimamizi wa
biashara.
“Tunategemea, Mwongozo huu
unakwenda kutoa dira ya namna bora ya utoaji wa huduma za biashara Tanzania
zinazoweza kuboresha biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja
mmoja na Taifa kwa ujuml,” alisema Bibi. Beng’i.
Alifafanua kuwa, mwongozo huo
utaleta matokeo chanya na kuwasihi watoa huduma za maendeleo ya biashara nchini
kutumia Mwongozo huu kama nyenzo katika kuwahudumia wafanyabiashara wadogo na
wa kati wanaotekeleza shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.