Monday, December 1, 2025

DAWA ZA KUFUBAZA MAKALI YA VVU (ARV) ZIPO KWA ASILIMIA 100- WAZIRI LUKUVI

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. William Lukuvi, amewahakikishia Watanzania kuwa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARVs) zinapatikana kwa asilimia 100 nchini na zinatolewa bila malipo kwa watu wote wanaoishi na VVU (WAVIU).

Amesema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambapo kwa mwaka 2025 yamefanyika chini ya kaulimbiu: “Imarisha Mwitikio, Tokomeza UKIMWI”.

 Waziri Lukuvi amesema upatikanaji wa dawa hizo umeendelea kuimarika, huku idadi ya WAVIU wanaotumia Dawa za ARV ikiongezeka kutoka asilimia 98 mwaka 2024 hadi asilimia 98.5 mwaka 2025, hatua inayochochea kupungua kwa athari za UKIMWI na kuboresha afya za wananchi.

 Aidha, Waziri Lukuvi amebainisha kuwa Serikali imeongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma za tiba na matunzo kwa WAVIU ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za VVU na UKIMWI nchini. Vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo 7,805 mwaka 2024 hadi vituo 8,203 mwaka 2025.

 Ameongeza kuwa, huduma za ufuatiliaji wa matibabu kwa WAVIU zinaendelea kuimarishwa, huku serikali ikiboresha upatikanaji wa huduma za maabara kwa kuongeza mashine za kupima wingi wa VVU mwilini. Kwa sasa, zipo mashine kubwa 50 kutoka 43 mwaka 2024, na mashine ndogo 127, hivyo kufanya kuwa na jumla ya mashine 177 zinazoendelea kutoa huduma nchini.

 Katika tamko lake, Waziri Lukuvi amesisitiza kuwa Siku ya UKIMWI Duniani ni muhimu kwa kutathmini hali na mwelekeo wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini na kimataifa, kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya, kuwakumbuka waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, na kuwaenzi watu wanaoishi na VVU pamoja na yatima wanaotokana na athari za UKIMWI.

 Amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa ajenda ya kudhibiti UKIMWI inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi zote za uongozi na utungaji sera


Read More