Wednesday, January 17, 2018

SIJARIDHISHWA NA UJENZI WA KITUO CHA SIRARI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.
Kufuatia hali hiyo amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  afike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma akiwa na mkandarasi aliyejenga kituo hicho.
“Serikali haiwezi kuvumilia ujenzi wa hovyo kiasi hiki, namtaka Kamishna wa TRA aje ofisini kwangu Januari 25, 2018 pamoja na mkandarasi aliyejenga kituo hiki akiwa na nyaraka zote za ujenzi wa jengo hilo.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) mara baada ya kumaliza kukagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Waziri Mkuu amesema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.
Waziri Mkuu amejionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia sheria na wajiepusha na biashara za magendo.
Waziri Mkuu amesema magendo yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa nchini kwa njia za magendo itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri kilichotumika.
Pia Waziri Mkuu ametembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Borega, ambapo amewasisiza wananchi wasimamie elimu ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.
Amesema Serikali imeweka sheria kali kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au kumoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.
Read More

WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA MIAKA MITATU


*Ni wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambao umedumu kwa miaka mitatu.
Ametoa uamuzi huo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Amesema amesitisha mpango huo wa ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kwa kuwa imepangwa kujenga katika eneo ambalo lipo mbali na wananchi.
 “Ninazo taarifa kuwa mnataka kujenga katika eneo ambalo litaigharimu Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya fidia na pia lipo mbali na makazi ya wananchi.”
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuruhusu ujenzi huo ufanyike katika eneo ambalo ni mbali ya makazi ya wananchi kwa kuwa watashindwa kufuata huduma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itapeleka wataalamu watakaofanya uchunguzi na bainisha eneo sahihi la kujenga Halmashauri hiyo kwa kutumia ramani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kutotamani fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kwamba wasipokuwa makini na fedha hizo zitasababisha wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini. ”Je mpo tayari kuchukuliwa hatua.?

Amesema Serikali inapeleka fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi na si kuwanufaisha watu binafsi.

Pia amewataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe wabunifu na wajue halmashauri zao zinahitaji nini ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo.
Waziri Mkuu ambaye leo ameendelea na ziara yake Mkoani Mara kwa kutembelea wilaya ya Tarime  ambapo baada ya kuzungumza na watumishi alikagua hopitali ya Tarime na kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha Sirari.
Read More

Tuesday, January 16, 2018

WAHUJUMU WA MIRADI YA MAJI MARA KUCHUKULIWA HATUA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itawachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhujumu ujenzi wa miradi ya maji mkoani Mara.

Hatua hiyo imetokana na kutoridhishwa na utekelezwaji wa ujenzi miradi ya maji katika baadhi ya halmashauri za mkoa huo,hivyo kuwacheleweshea wananchi kupata huduma hiyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 16, 2018) wakati alipokagua mradi wa maji wa Utegi uliopo katika kijiji cha Mika wilayani Rorya.

Amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo  inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Waziri Mkuu amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

“Nitafuatilia katika maeneo yote ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji kinalingana na thamani halisi ya miradi husika.”

Waziri Mkuu amesema anakerwa na Halmashauri ya wilaya ya Rorya kutosimamia vizuri miradi ya maji inayotekelezwa katika wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kutozingatia sheria.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya wanaoshi wilayani Tarime wawe wamehamie Rorya ifikapo Februari 15, 2018.

“Atakayeng’ang’ania kuishi Tarime hadi siku hiyo atakuwa amejiondoa kazini mwenyewe. Lazima watumishi wote waishi kwenye vituo vyao vya kazi Rorya ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.”

Pia Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutojihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ulimaji wa bangi pamoja na uvuvi haramu na badala yake wafanye shughuli halali za kuwaingizia vipato.
Read More

WAZIRI MKUU AMKABIDHI MHANDISI WA MAJI KWA NAIBU WAZIRI TAMISEMI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemkabidhi Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Mhandisi Obetto Sasi kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Josephat Kandege baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Ametoa uamuzi huo jana jioni (Jumanne, Januari 16, 2018) wakati aliposimamishwa na umati wa wananchi kwenye mji Mdogo wa Shitari alipokuwa njiani kuelekea kwenye kijiji cha Bubombi wilayani Rorya.

“Hatuwezi kuwa na mtumishi wa aina hii ambaye kila eneo tunakutana na changamoto za maji huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya Serikali kutoa fedha, hivyo namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa alete mhandisi mwingine wa maji.”

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Rorya na kukagua mradi wa maji katika mji Mdogo wa Shirati na kuona namna ya kuutekeleza.

Amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo  inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Maliwa alimueleza Waziri Mkuu kwamba changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mkoa huo inatokana na watendaji wa idara hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kiutendaji.
Wilaya ya Rorya inatekeleza miradi 11 ya maji ya bomba kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RWSSP) katika vijiji vya Kinesi, Randa, Utegi, Mika,Kirogo, Nyihara, Kisumwa,Nyamkonge, Nyambori, Gabimori na Marasibora.
Read More

Monday, January 15, 2018

ATAKAYEBAINIKA KUTAFUNA SH. MILIONI 320 ZA IMARA SACCOS ACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Musoma Bibi Yunia Wiga kufuatilia upotevu wa sh. milioni 320 za Imara SACCOS na atakayebainika kuhusika ashughulikiwe.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 15, 2018) alipopokea malalamiko ya wanachama wa SACCOS hiyo kupitia mabango waliyoyawasilisha katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini Musoma.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku sita, alimuagiza ofisa huyo kukutana na uongozi na wanachama wa SACCOS hiyo leo mchana na kisha kumpa majibu juu ya upotevu wa fedha hizo pamoja na sh. milioni 40 za hisa ifikapo Januari 20, 2018.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bibi Fidelica Myovella kuhakikisha anatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi mbalimbali waliopisha miradi ya maendeo katika Manispaa hiyo.

Waziri Mkuu alisema siyo vizuri kwa halmashauri kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kama barabara, standi na kisha kukaa muda mrefu bila ya kuwalipa fidia zao.

Aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha daladala cha Bweri ambao hawajalipwa fidia zao tangu mwaka 2013. Mkurugenzi huyo aliahidi kuanza kulipa madeni hayo kuanzia mwezi Januari, 2018.

Awali, Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini, Bw Vedastus Mathayo aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza baadhi ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni ikiwemo ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Bw. Mathayo alisema wananchi wa jimbo hilo kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ahadi hiyo.

Mbali na mradi wa maji pia Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo ya ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami pamoja na ukarabati wa kiwanja cha ndege unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Waziri Mkuu alisema ahadi zote zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 na zile zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli zitatekelezwa, hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Read More

MAJALIWA:SERIKALI KUTASUBIRI KUWAUNDIA TUME WEZI, MAFISADI

*Asisitiza kwamba atakayebainika atashughulikiwa hapo hapo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini wasijihusishe na vitendo vya wizi, ufisadi kwani Serikali haitosubiri kuwaundia tume za kuwachunguza bali itawashughulikia hapo hapo.

Amesema Serikali haikotayari kuwavumilia watumishi wanaojihusisha na wizi, ubadhilifu, rushwa na uzembe, hivyo ni vema viongozi waliopewa dhamana wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Januari 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Musoma mkoani Mara akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani hapa.

“Fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zinalenga kutatua kero za wananchi na si kuwanufaisha wachache wenye tamaa. Kama ni za ujenzi wa zahanati ijengwe na atakayezitafuna Serikali haitosita kumchukulia hatua.”

Waziri Mkuu asiwasisitiza watumishi wa umma kufanya kazi kwa mujibu wa sharia kwa sababu vitendo vya wizi, uzembe vinachangia kupunguza kasi ya kuwaletea maendelea maendeleo Watanzania.

Alisema lengo ni kuhakikisha azma ya Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi hususan ni wale wa hali ya chini inatimia, hivyo aliwaagiza viongozi wa halmashauri wakiwemo Madiwani kusimamia vizuri miradi ya maendeleo.

Pia Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa idara na watendaji wengine wa halmashauri kuacha tabia ya kukaa ofisini na dabala yake waende vijijini kwa ajili ya kuwafuata wananchi na kushirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

Waziri Mkuu alisema watendaji hao wanatakiwa waachane na tabia ya kuwasubiri wananchi wawapelekee malalamiko yao kwa sababu baadhi yao hawana uwezo wa kufika katika ofisi zao.
Read More

TUTAKAMILISHA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MUSOMA -MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amsema Serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980.

Atoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 15, 2018) wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kuwasili mkoani Mara kwa ajili ya ziara yake ya kikazi.

Waziri Mkuu amesema Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa awamu, ambapo wataanza na eneo la mapokezi na vyumba vya madaktari.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 ili ujenzi uendelee. Ujenzi huo ulianza mwaka 1980, ulisimama mwaka 1987 kuanza tena 2010.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua uwanja wa ndege wa Musoma mkoani Mara ambao unatarajiwa kukarabatiwa na kuwekwa lami.

Amesema kukamilika kwa ukarabati huo wa kiwanja hicho kutafungua fursa za utalii ndani ya mkoa huo ambao umezungukwa na vivutio vingi.

Amesema Serikali imedhamilria kukarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma ili kuboresha huduma za usafiri wa anga.

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kukarabatiwa ni Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea.
Waziri Mkuu amesema viwanja hivyo kwa sasa vinakarabatiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao wanajenga kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyostahili.

Awali, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaila alisema ukarabati huo utafanyika kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itahusisha upanuzi wa uwanja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

Alisema barabara ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa km. 1.6 na upana wa mita 33 ni ya changarawe, hivyo kusababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua.

Pia, Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma na kwamba ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

“Shule hii ilipewa sh bilioni 1.28 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nimekagua jengo la utawala, madarasa, mabweni, jiko, maabara na bwalo, nimeridhika na kazi iliyofanyika.”

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 kongwe ambazo Serikali iliamua kuzikarabati ili ziweze kurudi kama zamani na kuendelea kutumika.

Hata hivyo Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Musoma kushirikiana na uongozi wa shule hiyo katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili.

Miongoni mwa changamoto hizo ni malipo ya watumishi wasaidizi wakiwemo wapishi, walinzi na madereva, ambapo aliitaka kuchukua jukumu la kuwalipa watumishi hao badala ya kuacha jukumu hilo kwa Mkuu wa Shule.
Read More

Sunday, January 14, 2018

WAZIRI MKUU AUVUNJA MFUKO WA KUENDELEZA KAHAWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na wadau wa zao la Kahawa kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao hilo, kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, mjini Dodoma. Januari 14, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha mfano wa Kahawa iliyofungwa vizuri kwa soko la Kimataifa, inayotengenezwa na Kampuni ya Kitanzania ya AMIMZA Coffee, wakati alipokutana na wadau wa zao la Kahawa kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao hilo, kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, mjini Dodoma. Januari 14, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwenyekiti wa AMIMZA Coffee Products ya Tanzania, Amir Hamza, baada ya kukutana na wadau wa zao la Kahawa kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao hilo, kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, mjini Dodoma. Januari 14, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, baada ya kukutana na wadau wa zao la Kahawa kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao hilo, kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, mjini Dodoma. Januari 14, 2018.

*Amuagiza CAG kufanya uchunguzi tangu kuanzishwa kwake


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF) na amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza mwenendo wa mfuko huo tangu ulipoanzishwa.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Januari 14, 2018) wakati akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao la kahawa alichokiitisha, mjini Dodoma. 
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba uundwaji wa mfuko huo si wa kisheria bali ni wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

“Wakati Serikali inapambana kupunguza makato ya hovyo kwa wakulima, kumbe huku kuna chombo cha kuwachukulia fedha wakulima hii haikubaliki.”

Pia aliagiza kufungwa kwa ofisi za CDTF ili kupisha uchunguzi na baada ya CAG kukamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti, kazi zote zilizokuwa zinafanywa na mfuko huo zitafanywa na Bodi ya Kahawa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa  majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo yanaingiliana na yale ya Bodi ya Kahawa, ambayo ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya zao hilo, hivyo hakuna haja ya kuwa vyombo viwili vinavyofanya kazi moja.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amepiga marufuku wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wanavijiji na badala yake kahawa yote itauzwa kwa njia ya minada.

“Kahawa itauzwa katika minada tu na utaratibu wa kutoa vibali kwa wanunuzi wa kahawa kwenda kununua kwa wananchi vijijini marufuku kuanzia sasa, kama kuna watu wamepeleka fedha zao wazirudishe kwani hazitafanya kazi.”

Amesema Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie uuzwaji wa zao hilo na kuwachukulia hatua wote watakaokutwa wananunua kahawa kwa wakulima. “Anayetaka kahawa akanunue mnadani na si kwa wanavijiji lengo ni kuhakikisha mkulima anapata tija.”

Pia ameziagiza halmashauri zote zinazolima kahawa nchini kuanzisha vitalu vya miche ya kahawa na kisha kuigawa bure kwa wakulima, pia Maofiza Kilimo wawaelimishe walkulima wote wenye miti mikongwe waanzisha mashamba mapya.

Kuhusu suala la utafiti wa zao hilo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo itumie vyuo vyake vya kilimo ianzishe vituo vyake vya utafiti vitakavyofanya kazi ya utafiti wa zao hilo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Joseph Kakunda amesema watahakikisha maagizo hayo yanafanyiwa kazi, ambapo aliwaagiza Wakuu wa mikoa yote 16 inayolima kahawa pamoja na wakuu wa wilaya wake 52 wahakikishe wanafuta mara moja vibali vya ununuzi wa kahawa katika vyanzo vyao vya mapato.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma kilihudhuliwa na Waziri wa Kilimo Dkt. Chales Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Kakunda.

Wengine ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,, Bibi Maimuna Tarishi, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe, Wakuu wa mikoa 16 wanaolima kahawa na wakuu wa wilaya,Mrajis wa Vyama vya Ushirika Nchini, Dkt. Tito Haule, Makatibu tawala wa mikoa inayolima kahawa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa na wajumbe wa bodi hiyo,,Mkurugenzi wa bodi ya Kahawa Tanzania, Wakurugenzi wa Halmashauri,
Read More

Thursday, January 11, 2018

TUMIENI TAMASHA LA BIASHARA KUKUZA BIASHARA YA UTALII-MAJALIWA




WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar kuhakikisha inatumia Tamashara la Biashara la Zanzibar kama chachu ya kukuza biashara ya Utalii kama ilivyo kwa Dubai Shooping Festival na matamasha mengine Duniani.

“Natambua kwamba kazi ya kulipandisha hadhi zaidi tamasha letu hili si ndogo , hata hivyo ninayo imani kubwa kwamba  si tu uwezo wa kufikia malengo hayo mnayo bali pia mnaweza.”

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akifungua Tamasha la Nne la Biashara la Zanzibar lililofanyika kwenye viwanja vya Maisara katika mkoa wa Mjini Magharib, wilaya ya Mjini.

Tamasha hilo lilifunguliwa jana ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kuelekea katika sherehe za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yalitokea Januari 12, 1964.

Alisema Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko inatakiwa kutumia fursa ya uwepo wa tamasha hilo katika kuhakikisha inakuza biashara ya Utalii kwa kuwa linajumuisha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali.

Waziri Mkuu alisema Tamasha la Biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na huduma pamoja na kukuza uchumi wa nchi, pia linatoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara au watoa huduma na wateja wao.

”Hali hii humuwezesha mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake inavyokubalika kwenye soko, mapungufu yaliyopo kwenye bidha husika pamoja na kuelewa maboresho anayotakiwa kuyafanya katika bidhaa au huduma.”

Waziri Mkuu alisema kuwa tamasha hilo linaweza kutumika kama nyenzo muhimu katika kuanzisha mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya mteja  na mfanyabiashara, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kuwa na masoko ya uhakika.

Pia Waziri Mkuu alisema kufanyika kwa tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 katika ibara ya 84 (f).

“Ilani imeweka wazi azma ya Serikali ya kuanzisha na kuendeleza ujenzi wa kiwanja cha maonyesho ya biashara cha kimataifa na kuhakiisha ushiriki wa wajasiriamali wa Zanzibar  katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ndani na nje ya nchi.”

Baada ya kufungua tamasha hilo Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja yakiwemo ya taasisi za umma pamoja na wajasiriamali ambao wanatoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Uturuki, Misri, Uganda na Burundi.

Awali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema tamasha hilo lenye washiriki zaidi ya 200 limeandaliwa na wizara yake pamoja na TanTrade.

Balozi Amina aliseka kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka 2018 ni ‘wekeza kwenye viwanda kwa uchumi na ajira’ inalengo la kuhamasisha wadau kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda.
Read More

Wednesday, January 10, 2018

WAZIRI MKUU ARIDHISHWA NA USAFIRISHWAJI WA MBOLEA

*Aitaka TFC kuwa na mikakati madhubuti

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na usafirishaji wa mbolea kutoka wa wasambazaji wa pembejeo nchini kwenda kwa wakulima.

Pia ameitaka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kuwa na mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakati wote nchini.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akikagua usafirishaji wa mbolea kwenye maghala makubwa matatu jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kuona wakulima wote nchini wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea kwa wakati ili kilimo kiweze kuwaletea tija.

Amesema TFC inatakiwa ianze maandalizi ya usambazaji wa mbolea mapema kwani Serikali inataka wakulima wapate pembejeo miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo Dkt. Charles Tizeba akutane na wadau na kufanya mapitio ya gharama za usafirishaji wa mbolea.

Amesema lengo la mapitio hayo ni kuhakikisha mkulima aliyeko kijijini anapata  mbolea hiyo kwa gharama nafuu bila ya kumuathiri mfanyabiashara.

Pia amemtakaDkt. Tezeba ashirikiane na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Mwigulu Nchemba ili kuhakikisha malori yanayobeba mbolea yanafika katika mikoa husika kwa wakati.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo awasiliane na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbawala ili malori yanayobeba mbolea yakifika kwenye vituo vya mizani yapewe kipaumbele.

“Si kwamba yaongeze uzito hapana, bali yapewe kipaumbele cha kupima haraka ili yaweze kuwahisha mbolea kwa wakulima kwani tayari msimu umeshaanza.”

Naye Waziri wa Kilimo, Dkt. Tizeba alisema watahakikisha mbolea ya kutosha inakuwepo nchini na kwamba wakulima wote wanaipata kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Maghala aliyoyakagua Waziri Mkuu ni ghala la Mohammed Enterprises lililoko Mbagala, ghala la  Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) lililoko Kurasini na ghala la Premium lililoko Vingunguti ambako kote amekuta malori yakipakia mbolea kwa ajili ya uisafirisha katika mikoa mbalimbali nchini.
Read More

Tuesday, January 9, 2018

DKT.SHEIN AZINDUA SOKO LA KINYASINI


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Mohamed Shein amefungua  Soko Jipya la Kinyasini lililojengwa na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) ili kutatua changamoto za kukosekana kwa soko la kisasa katika Mkoa wa Kaskazini litakalowasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kuendesha biashara zao.

Mhe. Rais Shein amesema soko hilo litawagusa na kuwafikia  watu wenye kipato cha chini kuinuka kiuchumi kwa kuwanufaisha   Wajasiliamali wadogo wadogo vijijini pamoja na wafanyabiashara; Asasi ndogo ndogo za kifedha zinazotoa huduma vijijini; Vyama vya Msingi vya Ushirika/ Asasi za vijijini zinazojishughulisha na usindikaji wa mazao na masoko ya mazao kwa kushirikisha wanawake katika  makundi yote.

Katika uzinduzi huo uliofanyika Januari 09, 2018 Mkoa wa Kaskazini katika eneo la Kinyasini, Mhe.Rais alisema kujengwa kwa   soko hilo kuna manufaa makubwa kwa wakulima wadogo wakiwemo wafugaji, wavuvi na wafanya kazi za mikono.

“Soko hili litakuwa lenye tija kubwa kwa wananchi wa Zanzibar bila kujali maeneo wanakotoka. Soko hili ni letu sote, lisingeweza kujengwa kila mahali, au hewani lazima lingewekwa mahali, hivyo eneo hili la Kaskazini lilipata fursa hii, hivyo niwaombe liwe la wananchi wote wa Zanzibar.”Alisema Mhe.Rais
Sambamba na hilo Mhe. Rais alieleza kuwa kujengwa kwa soko hilo ni moja ya matunda ya Muungano na kuwataka Wananchi kuuenzi na Kuulinda Muungano huo.

“Miradi hii inayohusisha Bara ni moja ya mafanikio na matokeo makubwa ya Muungano wetu na hatuna budi kuuenzi”Alisisitiza Dkt.Shein

Katika hatua nyingine,Mhe. Rais aliitaka Halmashauri husika kuendelea kuweka mikakati mizuri ya kulitunza na kuliendeleza ili liweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa Wazanzibar wote.

“Niwaombe Halmashauri Kuona njia nzuri za kuendeleza kazi hii iliyofanywa na Programu hii na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi kama ilivyokusudiwa”Alisisitiza Mhe.Rais

Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuzingatia mafanikio ya mradi huu ikiwemo kusaidia kupambana na umasikini na kuleta tija.
“Kuwepo kwa soko hili kutasaidia kupambana na umasikini na kuongeza mapato, hivyo washiriki watunze miundombinu hiyo pamoja na kuongeza thamani ili kuleta tija.”Alieleza Mhe.Mhagama .
Naye Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Hamad Rashid Mohamed alimalizia kwa kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya MIVARF kuona umuhimu kuwajengea soko lenye ubora na litakalo tatua changamoto za kukosa soko la uhakika.
“Soko hili la Kinyasini  moja kati ya masoko 16 yaliyojengwa na Programu hii katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo litasaidia kuondokana na umasikini na wananchi kujikwamua kiuchumi”   
Programu hii ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inatekelezwa katika Halmashauri 62 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za Zanzibar, ikiwa  imegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo,  na Uvuvi Zanzibar.Programu ilianza utekelezaji wake Mwaka 2012.
Read More

Sunday, January 7, 2018

SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TUCTA KUONGEZA TIJA NA UFANISI SEKTA YA KAZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira,Vijana  na watu wenye ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama amesema serikali itaendelea  kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya  Wafanyakazi Nchini (TUCTA) katika kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi kwa kushughulikia masualaya wafanyakazi nchini

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo tarehe 7 Januari 2018, jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na viongozi hao wa TUCTA, walipokutana kwa ajili ya kujadiliana na kushauriana juu ya mazingira bora na wezeshi ya wafanyakazi, sekta ya kazi na ajira  nchini .

“Hatuwezi kupata tija na ufanisi katika sekta ya kazi bila vyama vya wafanyakazi  kushughulikia  malalamiko na manunguniko ya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi hasa katika mikataba  ya ajira na stahiki zao kwa mujibu wa sheria .TUCTA msipo simamia haya hata serikali tutashindwa kutimiza wajibu wetu kikamilifu. Serikali itaendelea kushughulikia masuala  ya wafanyakazi na sekta ya kazi kwa kuzingatia miongozo, kanuni na sheria za kazi  na ajira katika kutafuta suluhu ya masuala  ya kazi” alisema Mhagama.

Mhagama aliwahakikishia TUCTA kuwa serikali itayashughulikia madai yote ya wafanyakazi ambayo yanazingatia  sheria. Aidha Mhagama aliwataka TUCTA kuvitaka vyama vya wafanyakazi kufanya vikao na wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi  na wawapatie elimu juu ya masuala ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya tafsiri sahihi ya sheria za kazi  tulizonazo nchini.
Kwa upande wake Rais wa TUCTA, Tumaini  Nyamghokya ameishukuru serikali kwa ushirikiano wanaoupata toka serikalini  kupitia majadiliano ambayo yamesaidia migogoro ya wafanyakazi kupungua katika maeneo ya kazi.  ushirikiano huo umekuwa ni mhimili mkubwa kati ya serikali, waajiri na wafanyakazi.

Mkutano huo  ulihudhuriwa  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi  utawala bora, George Mkuchika, Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazina Ajira), Anthony Mavunde na Katibu Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa  na Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira)  Erick Shitindi.

Msingi wa serkali na Shirikisho la Vyama vya  Wafanyakazi Nchini (TUCTA) kukutana kwa majadiliano na mashauriano unatokana na nchi ya Tanzania kusaini mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), ukiwemo mkataba namba 98 wa mwaka  1949,ndio uliweka mazingira hayo  ya serikali,waajiri na wafanyakazi kukutana ili kuweka dhana ya kuaminiana na  kuleta tija na ufanisi katika sekta ya kazi na ajira.


Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi na Ajira)  Erick Shitindi akieleza masuala ya sekta ya kazi  wakati wa mkutano wa Shirikisho la Vyama vya  Wafanyakazi Nchini (TUCTA) na   serikali leo tarehe 7 Januari 2018 ,jijini Dar es Salaam.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya  Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Tumaini  Nyamghokya akifanunua masuala ya wafanyakazi  wakati walipokutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira,Vijana  na watu wenye ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama leo tarehe 7 Januari 2018,jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira,Vijana  na watu wenye ulemavu) Mhe.  Jenista Mhagama akisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na  Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA) wakati alipokutana na shirikisho hilo leo tarehe 7 Januari 2018, jijini Dar es salaam. 

Read More