WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar kuhakikisha inatumia Tamashara la Biashara la Zanzibar kama chachu ya kukuza biashara ya Utalii kama ilivyo kwa Dubai Shooping Festival na matamasha mengine Duniani.
“Natambua kwamba kazi ya kulipandisha hadhi zaidi tamasha letu hili si ndogo , hata hivyo ninayo imani kubwa kwamba si tu uwezo wa kufikia malengo hayo mnayo bali pia mnaweza.”
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatano, Januari 10, 2018) wakati akifungua Tamasha la Nne la Biashara la Zanzibar lililofanyika kwenye viwanja vya Maisara katika mkoa wa Mjini Magharib, wilaya ya Mjini.
Tamasha hilo lilifunguliwa jana ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kuelekea katika sherehe za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yalitokea Januari 12, 1964.
Alisema Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko inatakiwa kutumia fursa ya uwepo wa tamasha hilo katika kuhakikisha inakuza biashara ya Utalii kwa kuwa linajumuisha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali.
Waziri Mkuu alisema Tamasha la Biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na huduma pamoja na kukuza uchumi wa nchi, pia linatoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara au watoa huduma na wateja wao.
”Hali hii humuwezesha mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake inavyokubalika kwenye soko, mapungufu yaliyopo kwenye bidha husika pamoja na kuelewa maboresho anayotakiwa kuyafanya katika bidhaa au huduma.”
Waziri Mkuu alisema kuwa tamasha hilo linaweza kutumika kama nyenzo muhimu katika kuanzisha mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya mteja na mfanyabiashara, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kuwa na masoko ya uhakika.
Pia Waziri Mkuu alisema kufanyika kwa tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 katika ibara ya 84 (f).
“Ilani imeweka wazi azma ya Serikali ya kuanzisha na kuendeleza ujenzi wa kiwanja cha maonyesho ya biashara cha kimataifa na kuhakiisha ushiriki wa wajasiriamali wa Zanzibar katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ndani na nje ya nchi.”
Baada ya kufungua tamasha hilo Waziri Mkuu alitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja yakiwemo ya taasisi za umma pamoja na wajasiriamali ambao wanatoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Uturuki, Misri, Uganda na Burundi.
Awali, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Balozi Amina Salum Ali alisema tamasha hilo lenye washiriki zaidi ya 200 limeandaliwa na wizara yake pamoja na TanTrade.
Balozi Amina aliseka kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka 2018 ni ‘wekeza kwenye viwanda kwa uchumi na ajira’ inalengo la kuhamasisha wadau kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda.
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.