Friday, January 5, 2018

WAZIRI MKUU AKEMEA MADUDU USHIRIKA MBINGA

*Aagiza uchunguzi ufanyike kuanzia leo, maafisa wa MBICU, MBIFACU kikaangoni
*Apiga marufuku ununuzi wa kahawa kwa mfumo wa MAGOMA
*Aitisha kikao cha wadau wa kahawa Dodoma Jan. 14

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amebaini madudu kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika vya Mbinga (MBICU na MBIFACU) na kuagiza uchunguzi ufanyike kuanzia leo.

“Nikiondoka hapa jukwaani, viongozi wote wa zamani na wa sasa waripoti kwa Mkuu wa Wilaya, na OCD hakikisha ofisi za chama hazifunguliwi hadi kesho asubuhi (leo) kazi itakapoanza, ili wasije kubadilisha nyaraka kwenye ofisi yao. Timu yangu ya uchunguzi iko hapa Mbinga, kesho waende wote kwenye ofisi hizo,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Januari 5, 2018) wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Mbinga, kwenye viwanja vya CCM, mjini Mbinga.

“Natambua kuwa MBICU ilishakufa ikiwa na madeni makubwa na mkaunda tena MBIFACU, ambayo nayo inasuasua, lakini viongozi wote hawa watafutwe, waje waonane wa timu  yangu na waeleze fedha za chama zimeenda wapi na kama walizikopea zilifanya nini,” alisisitiza.

Alisema timu hiyo ya uchunguzi itakiangalia chama hicho na kukifumua chote, na wote wakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kinidhamu. “Tunataka MBICU na madeni yenu yaliyoko kwa Msajili wa HAZINA yajulikane, tunataka turudishe hoteli yetu, mashamba yetu na majengo yetu,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imeamua kuboresha ufanisi katika mazao matano ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaliingizia Taifa fedha za kigeni.

“Mazao haya tutayasimamia kuanzia kilimo hadi uvunaji na utafutaji wa masoko. Nimeshafuatilia mazao ya korosho, tumbaku na pamba. Na sasa nimeanza na zao la kahawa na nimeamua kuanzia huku Mbinga,” alisema.

Alisema Serikali imedhamiria kuimarisha zao la kahawa katika mikoa yote inayolima zao ikiwemo Ruvuma, Mbeya, Kagera, Kigoma na maeneo mengine.

“Na nikimaliza ziara hii, nimeitisha kikao cha wadau wa zao la kahawa mjini Dodoma ifikapo Januari 14, 2018. Nimewaita Wakuu wa Mikoa, wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa ushirika, Maafisa kilimo na wadau wote kutoka mikoa yote inayolima kahawa hapa nchini, tukutane na kupeana maelekezo juu ya usimamizi wa zao hili,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kwamba kuanzia msimu ujao, zao la kahawa litauzwa kwa mnada chini ya mfumo wa ushirika. “Kuanzia msimu ujao, kahwa yote utauzwa kwa mnada, mnunuzi yeyote akitaka kununua kahawa aende kwenye mnada, tukikukuta mtu ananua kahawa kwa mkulima tutamkamata,” alisema na kuamsha shangwe kwa wananchi hao.

Alisema kuna watu wamekuwa wanapita na kununua kahawa kwa mfumo wa ‘magoma’ ambapo huwalaghai wakulima kwa kuwapa noti chache za sh. 10,000. “Huu mfumo wa magoma ni wa kuwaibia wananchi, hatutaki tena kuuona. Hakuna tena magoma hapa Mbinga,” alisisitiza.

“Bei ya mnada ndiyo fedha ya mkulima na sasa, Serikali tumeondoa tozo 17 kwenye zao hili kwa sababu tunataka tuone mkulima afaidike na zao hili,” alisema.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Nyasa ambako atazungumza na watumishi na madiwani, ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, atakuwa mgeni rasmi kwenye tamasha la utalii na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.